ANGALIA LIVE NEWS
Wednesday, March 20, 2013
LEO NDIO MWISHO; OMBA UWAKILISHI KWENYE MABARAZA YA KATIBA SASA - MNYIKA
LEO tarehe 20 Machi 2013 ni siku ya mwisho ya wananchi kuwasilisha maombi ya kuwa wajumbe wa mabaraza ya katiba ya ngazi ya wilaya ambayo yana wajibu muhimu wa kupitia rasimu ya katiba na kutoa maoni iwapo imezingatia maoni ya wananchi yaliyokunywa katika hatua ya wananchi binafsi na makundi mbalimbali katika jamii.
Nawakumbusha ambao bado hamjawasilisha maombi na mna dhamira ya kutimiza wajibu huu wa kiraia na kikatiba kwa kuwasilisha barua ya maombi kwa watendaji wa mitaa/vijiji.
Kuna nafasi nane kwa kila mtaa kwa Dar es salaam, nne kwa maeneo mengine ya Tanzania Bara katika makundi yafuatayo; mwanamke, kijana, mtu mzima na mtu mwingine yoyote: kwa Zanzibar tatu kwa kila shehiya.
Sifa ni raia, miaka 18 au zaidi mwenye kujua kusoma, kuandika, hekima, busara, uadilifu, uwezo wa kujieleza na kupambanua mambo ambao najua wengi mnazo. Sifa nyingine ni kuwa mkazi wa kudumu kwenye mtaa au kijiji ambayo haimaanishi kwamba ni lazima uwe mwenye nyumba, hata wapangaji mnaruhusiwa kuomba. Sio lazima uwe mwanachama wa chama chochote cha siasa na uteuzi wa awali utafanywa na mkutano mkuu wa mtaa wenu au kijiji chenu ambao wajumbe ni wakazi wote wa mtaa/kijiji husika.
Wakati huo huo, tuendelee kutaka kwamba baada ya wananchi kufanya uteuzi wa awali kwenye mitaa/vijiji vyao kidemokrasia tume ya mabadiliko ya katiba ifanye kazi kwa uhuru kuthibitisha uteuzi huo waingie moja kwa moja kwenye mabaraza ya katiba badala uteuzi mwingine wa ‘kuchakachua’ kufanywa na kamati za maendeleo za kata ambazo zimehodhiwa na chama kimoja.
John Mnyika (Mb)
20/03/2013
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment