Kocha mkuu wa Simba, Patrick Liewig
Kocha wa Simba, Patrick Liewig amesema uchovu wa ziara ndefu waliyoifanya kwa kutumia basi lao unaweza kuathiri matokeo ya timu hiyo katika mechi yao leo ya Ligi Kuu ya Tanzania Bara dhidi ya Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Kaitaba hapa Kagera.
Simba ilisafiri kwa basi walilopewa na wadhamini kampuni ya bia ya TBL kupitia bia ya Kilimanjaro katika ziara ya mechi za kirafiki iliyoanza kwa kucheza dhidi ya CDA mkoani Dodoma ambayo walishinda 1-0, ikaenda Singida walikoshinda 4-0 dhidi ya Singida United na kisha ikatua mkoani Tabora ambako ilitoka sare ya 1-1 dhidi ya Rhino Rangers, kabla kabla ya kuelekea Kagera.
Liewig alisema mjini hapa jana kuwa uchovu wa safari unaweza ukawaathiri lakini atawategemea vijana wake ambao damu yao bado ni changa.
Wachezaji kutoka katika timu ya taifa (Taifa Stars) iliyoshinda 3-1 dhidi ya Morocco katika mechi ya kuwania kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia 2014 jijini Dar es Salaam Jumapili, walisafiri kwa ndege juzi na waliungana na wenzao jana baada ya kushindwa kufanya hivyo juzi kutokana na uwanja wa ndege wa Bukoba kujaa maji kwa sababu ya mvua zinazoendelea kunyesha mjini hapa na hivyo wakalazimika kulala mkoani Mwanza hadi jana walipokuja hapa.
Kwa namna Liewig alivyopanga vikosi vyake katika mazoezi ya jana jioni kwenye Uwanja wa Ntungamo pembeni kidogo ya Kagera mjini, ilionekana huenda Mrisho Ngassa leo ataanzia nje. Amri Kiemba naye alifanya mazoezi ya peke yake jana.
Ngassa na Kiemba ndiyo wachezaji pekee kutoka Stars walioonekana kuwa katika hatihati ya kuanza katika kikosi cha Simba leo.
Nyota wengine wa Stars, kipa na nahodha Juma Kaseja, mabeki Shomari Kapombe na Nasor Masoud 'Chollo' na kiungo Mwinyi Kazimoto walifanya mazoezi na kikosi cha kwanza cha Mfaransa huyo.
Kocha msaidizi, Jamhuri Kiwhelu 'Julio' alisema timu yake leo ina kibarua kigumu mbele ya wenyeji wao lakini anaamini Wekundu wa Msimbazi wataondoka na pointi zote tatu.
Alisema kuwa Kagera Sugar inayonolewa na Abdallah 'King' Kibadeni ni timu ngumu hasa inapocheza kwenye uwanja wake wa nyumbani lakini wamejipanga kuibuka na ushindi.
"Wenzetu pia wamejiandaa kama ambavyo na sisi tumejiandaa hivyo natarajia mchezo mgumu kesho (leo), hata hivyo nawaamini wachezaji wangu na 'inshallah' tutaibuka na ushindi," alisema Julio.
Julio aliongeza kuwa ushindi katika mchezo wa leo utawaweka wachezaji wake kwenye nafasi nzuri ya kuifunga Toto African katika mechi yao inayofuata Jumamosi dhidi ya Toto African kwenye Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza.
Mabingwa watetezi wa ligi hiyo, Simba ambao msimu huu unaonekana si mzuri kwao, wanashika nafasi ya tatu katika msimamo wakiwa na pointi 34, ambazo ni 14 nyuma ya vinara na mahasimu wao wa jadi Yanga. Azam inashika nafasi ya pili kwa kuwa na pointi 37. Simba na Azam zimecheza mechi 19, moja pungufu ya Yanga, ambao watacheza mechi yao ya 21 Jumamosi dhidi ya Polisi mjini Morogoro.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment