ANGALIA LIVE NEWS

Sunday, March 10, 2013

Maalim Seif: Hatutomvumilia mwanachama atakayejihusisha na makundi kwa kujitafutia uongozi


Katibu Mkuu wa CUF Maalim Seif Sharif Hamad akizungumza katika ufunguzi wa mkutano mkuu wa CUF Wilaya ya Mjini uliofanyika ukumbi wa Jamat-Khan Mjini Zanzibar

Wakati Chama Cha Wananchi CUF kikijiandaa na uchaguzi mkuu wa ndani ya chama hicho kuanzia mwezi mei mwaka huu, kimesema hakitomvulia mwanachama atakayejihusisha na makundi kwa kujitafutia uongozi…
Katibu Mkuu wa Chama hicho Maalim Seif Sharif Hamad ameeleza hayo leo wakati akifungua mkutano mkuu wa CUF Wilaya ya Mjini uliofanyika ukumbi wa Jamat-Khan mjini Zanzibar.

Amesema mwanachama yeyote atakayebainika kujihusisha na makundi kwa kutafuta uongozi, kamwe chama hakitomvumilia na anaweza kupoteza sifa ya kugombea kuchaguliwa nafasi aliyoiomba.
Amefahamisha kuwa kila mwanachama ana haki ya kugombea nafasi yoyote ndani ya chama na kuwahimiza kufanya hivyo bila ya woga, lakini wasijihusishe na makundi katika kugombea nafasi hizo.
“Anayetaka kugombea nafasi ya Mwenyekiti Taifa, Katibu Mkuu na nafasi nyengine zote ruksa, lakini hatutaki makundi kwani makundi ndio yanayoua chama, na mimi nikiamua kugombea tutashindana kwa kura”, alieleza Maalim Seif ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar.
Amesema chama cha CUF taifa kimejipanga kusimamia chaguzi hizo ili ziwe huru na haki, na kuhakikisha kuwa kila mwanachama anataka kugombea nafasi ya uongozi anapatiwa fursa hiyo.
Akizungumzia kuhusu uhai wa Chama hicho Maalim Seif amesisitiza haja ya kufuatwa kikamilifu kwa katiba ya chama hicho, ikiwa ni pamoja na kuitishwa vikao kwa mujibu wa katiba.
Ameeleza kuwa vikao ni muhimu katika kuimarisha uhai wa chama, kwani ndivyo vyenye haki ya kujadili na kutoa maamuzi juu ya maendeleo ya chama, sambamba na kuwahimiza kuendeleza Jumuiya za chama hasa za vijana na wanawake.
Katibu Mkuu huyo wa CUF amekemea tabia ya wanachama kupikiana majungu na kuwataka kutumia vikao halali vya chama kukosoana na kurekebishana.
Kushambuliwa kwa Kibanda na matukio ya kihalifu nchini
Katika mkutano huo Maalim Seif amelaani vikali kitendo cha kushambuliwa  kwa Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania ambaye pia ni mhariri mtendaji wa kampuni ya New Habari Absalom Kibanda hivi karibuni jijini Dar es Salaam.
Amesema Kibanda ni mwandishi mzuri, makini na mweledi, na kwamba kitendo hicho cha dhulma na cha kinyama kimempotezea hadhi mwandishi huyo anayetegemewa na taifa.
Ameliomba jeshi la polisi kufanya uchunguzi wa kina kuwabaini waliohusika na tukio hilo ili waweze kuchukuliwa hatua za kisheria.
Nchimbi hakuitendea haki Zanzibar
Akizungumzia kuhusu matukio ya kihalifu yaliyotokea Zanzibar likiwemo la kuuwawa kwa Padri Evarist Mushi, Maalim Seif amesema Waziri wa mambo ya ndani Emannuel Nchimbi hakuitendea haki Zanzibar kwa kutamka kuwa ni kitendo cha ugaidi, na badala yake ameidhulumu Zanzibar kiuchumi.
Amesema sekta kuu inayotegemewa kwa uchumi wa Zanzibar ni Utalii, hivyo kuitangazia dhama ya ugaidi ni kuidhulumu na kuipotezea fursa zake.
Ameiomba serikali ya Jamhuri wa Muungano wa Tanzania kuziweka bayana taarifa za uchunguzi wa tukio hilo ili wananchi waweze kuzifahamu na hatimaye kuweza kuisafisha Zanzibar na dhana ya kigaidi.
Daftari la kudumu la wapiga kura
Maalim Seif amewataka vijana kushajihishana kufuatilia upatikanaji wa vitambulisho vya Mzanzibari mkaazi, ili waweze kusajiliwa katika daftari la kudumu la wapiga kura.
Amesema bado vijana wengi hawana ZAN ID huku wakiwa wameshatimiza umri wa kupatiwa vitambulisho hivyo, na kuwataka kuongeza juhudi kuvitafuta ili waweze kupatiwa haki hiyo ya kikatiba itakayowawezesha kupiga kura katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.
Amerejea kauli yake ya kuwahimiza Wazanzibari kuendeleza umoja wao, na kutokubali kuingizwa katika malumbano, ili kuinusuru Zanzibar kurejeshwa ilikotoka.

No comments: