ANGALIA LIVE NEWS

Monday, March 4, 2013

MAKUNDI YA WANAUME NA MITAZAMO YAO YA KIMAPENZI KWA WANAWAKE -6

KATIKA matoleo kadhaa huko nyuma, nimeelezea makundi mawili ya wanaume. Sifa, tabia, tathmini ya kimapenzi na kadhalika.

KUNDI LA TATU
Hili linagusa aina ya wanaume wenye gubu. Wale wanaoishi kwa wasiwasi dhidi ya wapenzi wao. Unapolichunguza gubu kwa macho yakinifu, unapata majibu kuwa chanzo chake ni wivu. Uzuri ni kwamba huko nyuma nilishaeleza kinagaubaga hasara na faida za wivu.

Niendelee kukiri kuwa wivu ni muhimu kwa sababu hutafsiri upendo. Kama mwandani wako hakuonei wivu, maana yake hana mapenzi ya kweli au ana matatizo ya kihisia. Itambulike kuwa lipo tabaka la watu ambao mguso wao kimapenzi ni mdogo mno.Hata hivyo, hao si wakati wake kuwachambua leo. Hapa nazungumzia wale wenye wivu kupindukia mpaka kufikia hatua ya kuonekana wana gubu. Kimsingi nao ni watu hatari sana kwenye maisha ya uhusiano. Mke anaweza kufanya jema kwa ajili yake lakini yeye akapokea ndivyo sivyo.

Tatizo kubwa la mtu mwenye gubu ni kuwa anapokuwa na mwenzi wa maisha yake, hatambui kama aliyenaye ni binadamu. Anadhani ni malaika, matokeo yake jambo dogo linaweza kuondoa amani ya nyumbani kabisa. Hajulikani muda wa kutabasamu wala kukasirika.

Akirudi nyumbani mapema badala ya nyumba kuwa na amani ndiyo kwanza inageuka ya moto. Makosa ya watoto au jirani, yanaweza kumgharimu mke na kufanya hata yale mambo mazuri ambayo wangeyajadili kifamilia na kuyapatia ufumbuzi, kuyeyuka au kuwekwa kiporo.
Ni vizuri kutambua mwanaume wako yupoje na kama sifa zake zinamfanya aunde kundi hili, unatakiwa ujiandae au uwe na namna bora ya kuishi naye. Siku zote, uwe ni mtu mwenye kutazama mbele na kuwa na ufahamu kwamba zipo aina tofauti za wanaume.

Mara nyingi ni watu ambao jambo dogo hulikuza na kulifanya lidumu kwa muda mrefu. Daima hawaishiwi visa lakini chanzo chake kikubwa ni wivu. Hawakai wakawaamini wanawake wao, badala yake huishi kwa wasiwasi.

Anaweza kutumia fedha kwa ajili tu ya kuwalipa watu waweze kumfuatilia mwenzi wake. Si ajabu kufanya matukio ambayo yanaweza kukufanya ujiulize: “Kama hamwamini mpenzi wake ni kwa nini anaendelea naye?”
Kuna mfano huu; Rehema ni mwanamke mwenye watoto wawili. Ni msomaji wangu, siku moja alinipigia simu kueleza matatizo ya mume wake. Aliniambia kwamba mumewe ana tabia chafu sana.

“Pale alipo hana jema ambalo naweza kumfanyia. Nikimnunulia zawadi atauliza pesa nimepata wapi? Anafahamu kuwa nina kazi lakini hataamini kama nimemnunulia kutokana na fedha zangu, yeye atang’ang’ania nimehongwa.

“Nikizungumza na simu, lazima afuatilie ninayezungumza naye ni nani. Mbaya zaidi ameshawatukana karibu wafanyakazi wenzangu wote wa kiume. Kila aliyeonesha ukaribu na mimi wa kikazi, alipogundua alimpigia simu na kumtukana.
GPL

No comments: