MDAU wa safu hii, bado naendelea kukudadavulia mada hii ya makundi ya wanaume na mitazamo yao ya kimapenzi kwa wanawake. Tuwe pamoja...
“Anapofika nyumbani hanisalimii, mpaka akague kwanza simu, aone simu zilizoingia na kutoka, asome SMS zote. Aangalie orodha ya majina niliyosevu, anapokuta jina la kiume anafuta, anaowaacha ni kaka zangu na baba peke yake.
“Endapo atakuta jina la kike jipya kwenye simu yangu, atapiga ili kuhakikisha kama kweli huyo ni mwanamke. Yaani haniamini hata kidogo. Yeye simu yake anailinda mpaka kero. Chooni anaingia nayo. Hajiamini na haniamini.”
TATHMINI KIMAPENZI
Ni wagonjwa wa kupenda. Ila siyo aina nzuri ya kuwa nao katika uhusiano kwa sababu ni kero. Mwanaume wa kundi hili anaweza kukubughudhi kipindi ambacho ulikuwa unahitaji sana faraja kutoka kwake.
Ni kweli anapenda lakini kasoro yake kubwa ya kutojiamini, humfanya ashindwe kutoa huduma nzuri kwa mwenzi wake. Kasoro kubwa iliyopo ndani ya mwanaume wa kundi hili ni kwamba hudhani kwamba anapoonesha wivu wa kupindukia ndipo utaamini anakupenda.
Unaweza kumvumilia kutokana na udhaifu wake lakini anaweza kukuharibia hata kazi. Jiulize kuwa anatukana wafanyakazi wenzako, kuna siku atamtolea lugha chafu hata bosi wako. Kama sivyo, haohao wafanyakazi wenzako watakupa vipi ushirikiano kazini?
Mtu mwenye gubu kwa kawaida huwa na hasira za haraka, hiyo humfanya awe na mkono mwepesi. Ninayo mifano mingi ya wanawake waliodhalilishwa mbele za watu kutokana na vipigo kutoka kwa waume zao.
Unahitaji mwanaume ambaye atakuamini ili uishi kwa furaha. Mwanaume wa sampuli hii hawezi kukupa utulivu pale unapouhitaji. Wakati wowote, anaweza kuifanya baridi kugeuka moto. Pigania amani na furaha yako kwanza.
Hayawezi kuwa mapenzi kama ndani yako huna amani wala furaha. Mtakuwa mnaishi kwa kutimiza wajibu ila si kwa furaha iletwayo na mapenzi. Asilimia kubwa ya wanawake waliodumisha uhusiano wao na wanaume wenye gubu, walianza kwa kulia mfululizo mpaka wakageuka sugu.
BAHATI MBAYA
Janga lao namba moja ni familia kukumbwa na maradhi ya moyo. Kutokana na tabia yake ya kuishi kwa wasiwasi, humsababishia msongo wa mawazo mara kwa mara, mwisho kukumbwa na shinikizo la damu.
Kadhalika mwenzi wake. Papara zake humsababishia mwenzi wake maumivu, mateso na wasiwasi, hivyo kumfanya naye kuingia kwenye hatari ya kupata maradhi ya moyo. Vilevile, wote wawili wanaweza kuingia kwenye hatari ya kuugua kisukari (athari ya muda mrefu).
Baadhi hukimbiwa baada ya wanawake wao kushindwa kuhimili vishindo vinavyosababishwa na gubu zao. Wanapoachwa, hubaki wakilalamika huku na huko bila kujitazama wao wenyewe na kutambua udhaifu wao.
Mara nyingi husalitiwa. Hii husababishwa na tabia zao. Wanawake huona kero, hivyo kuhitaji utulivu.
Itaendelea wiki ijayo.
Global Publishers
No comments:
Post a Comment