ANGALIA LIVE NEWS

Monday, March 18, 2013

MAKUNDI YA WANAUME NA MITAZAMO YAO YA KIMAPENZI KWA WANAWAKE -8


KILA kundi nalichambua kwa mapana yake, najenga hoja kwa mifano ili iwe rahisi kwako msomaji wangu kuelewa. Wiki iliyopita, niliishia kwenye kipengele cha “BAHATI MBAYA” ambayo inawakabili wanaume wa kundi la tatu ambao wana sifa ya gubu.
Pamoja na yote ya hatari yanayoweza kujiri, ukweli ni kwamba janga lao namba moja ni familia kukumbwa na maradhi ya moyo. Kutokana na tabia yake ya kuishi kwa wasiwasi, humsababishia msongo wa mawazo mara kwa mara, mwisho kukumbwa na shinikizo la damu.
Kadhalika mwenzi wake. Papara zake humsababishia mwenzi wake maumivu, mateso na wasiwasi, hivyo kumfanya naye kuingia kwenye hatari ya kupata maradhi ya moyo. Vilevile, wote wawili wanaweza kuingia kwenye hatari ya kuugua kisukari (athari ya muda mrefu).
Baadhi hukimbiwa baada ya wanawake wao kushindwa kuhimili vishindo vinavyosababishwa na gubu zao. Wanapoachwa, hubaki wakilalamika huku na huko bila kujitazama wao wenyewe na kutambua udhaifu wao.
Mara nyingi husalitiwa. Hii husababishwa na tabia zao. Wanawake huona kero, hivyo kuhitaji utulivu. Wanapokutana na wanaume wa pembeni, hata kama nao ni walewale, ila katika siku za kwanza huonekana wana afadhali, hivyo kuwachia wazi mapenzi yao kwa matarajio ya kupata utulivu.
Wakati mwingine, mwanamke baada ya kusaliti kwa muda ndipo hubaini kama hata mwanaume wa nje ambaye anatoka naye ni aina ileile. Hii ndiyo sababu ya baadhi ya wanawake kutamka: “Wanaume wote ni damu moja, baba mmoja na mama mmoja.”
Ninao mfano wa Rehema, yeye aliniambia: “Kutokana na usumbufu wa mume wangu, niliamua kufanya kazi kwa bidii ili nami nimiliki vitu vyangu. Kwani kila siku alikuwa ananinyanyasia gari lake, eti linanipa kiburi.
“Wakati mwingine alinitukana nikaumia, pale aliposema huwa nawapa lifti wafanyakazi wenzangu wa kiume kwa sababu ni mabwana zangu. Kuna siku alinitukana kabisa kuwa huwa nafanya mapenzi kwenye gari alilonipa yeye.
“Nikatamani nimiliki gari langu mwenyewe, kwa hiyo nilichokifanya nilijiendeleza na masomo, yaani nilifanya kazi na kusoma kwa wakati mmoja. Nilijiwekea malengo kwamba baada ya chuo nitapandishwa cheo na kipato kitaongezeka, hivyo malengo yangu yatatimia.
“Chuo kikaleta mzozo, kila siku natukanwa. Asubuhi naingia kazini, jioni chuo natoka usiku. Kila ninaporudi ananiburuza mpaka chumbani, ananivua nguo na kunifanyia vitendo vya kishenzi kwa madai kuwa ananikagua kama nilifanya mapenzi na mwanaume.
“Siku nyingine alidai nimetoka kufanya mapenzi. Nikiwa katika hedhi, alinivua pedi mpaka aone damu ndiyo aridhike. Akidai eti naweza kufanya mapenzi na kuvaa pedi ili kumuongopea. Niliumia sana, hasa kitendo cha yeye kunisingizia nimefanya mapenzi wakati sijafanya.
“Pale chuoni nilikutana na mwanaume anayeitwa Rama. Aliyagundua matatizo yangu, akawa ananishauri, nikiwa mnyonge aligundua na kunifariji. Nikatokea kumpenda sana, maana alinipa faraja ambayo ni msamiati kwa mume wangu.
“Miezi saba tangu nianze chuo, nilijikuta naanza uhusiano wa kimapenzi na Rama.

Itaendelea wiki ijayo.

Global Publishers

No comments: