Nawazungumzia baadhi ya mashemeji ambao wamekuwa ni chanzo cha ndoa nyingi kuingia kwenye migogoro kama siyo kuvunjika kabisa.
Mashemeji ninaotaka kuwazungumzia leo ni wale wa kiume wasiojiheshimu ambao wamekuwa na tabia za kuwazoea kupitiliza wake wa kaka zao na kufikia hatua ya kutaka wapewe huduma wasizostahili kupewa.
Wanawake walioolewa wanafundishwa kuwaheshimu sana mashemeji zao lakini heshima hiyo si kwa kila shemeji. Kuna wengine kwa jinsi walivyo hawastahili kuheshimiwa hata kidogo. Hawa ni wale ambao wamekuwa na mazoea ya kijinga.
Kwa hawa si ajabu wakafikia hatua ya kuomba nao wapewe penzi. Ndiyo! Ninapoandika makala haya kuna kesi ambayo ipo kwa mpangaji mwenzangu inayohusiana na hiki ninachokisema. Huyu jamaa ni mtu wa kusafiri sana lakini mdogo wake huwa anakuja pale nyumbani na kupewa chakula na shemeji yake.
Mara kadhaa mwanamke huyo amekuwa akilalamika kuwa shemeji yake huyo amekuwa na mazoea mabaya kwani kuna wakati anamsifia kuwa ni mzuri na hata kufikia hatua ya kumshikashika huku akimwambia: “Dah! Kaka anafaidi kweli.”
Mashemeji kama hawa ndiyo ninaotaka kuwazungumzia leo. Unapobahatika kuingia kwenye ndoa, si kila mtu wa upande wa mumeo au rafiki wa mumeo unatakiwa kumchekeachekea eti ili kuilinda ndoa. Kuna wengine unatakiwa kukaa nao mbali kwani ukikaa kihasara, watakuomba mchezo.
Waliowahi kufanya hivyo ni wengi na baadhi yao waliomba wapewe penzi na wake wa kaka zao lakini wakanyimwa na hadi leo hawana uhusiano mzuri na ndugu zao.
Kiukweli kuna wanaume ambao hutakiwi kuwazoea, kuna wale ambao wanataka kuutumia ukaribu wa kishemejishemeji kukuingiza vishawishini. Atakuwa anakuletea zawadi kama shemeji, anakutumia vocha kama shemeji lakini kumbe anakulainisha tu na kwamba kuna siku atakutamkia mambo yake ya kijinga.
Hili liwe fundisho kwa wake za watu hasa wale ambao ni wanywaji wa pombe. Shemeji yako anaweza kukuambia anataka kukuchukua kwenda kukupa ofa ya bia. Kwa kuwa mumeo hayupo na kwa uroho wako unaweza kukubali kumbe nia yake akuleweshe kisha ale ‘tunda’ la ‘mumeo’.
Achana na hilo, shemeji yako si mtu wa kumvalia khanga moja. Wapo wanawake ambao sijui wana akili za aina gani. Unaweza kumkuta kakaa sebuleni huku kavaa khanga moja, anakuja shemeji yake, anaendelea kukaa pale akiamini eti hakuna tatizo kwa kuwa ni shemeji.
Itaendelea wiki ijayo.
Global Publishers
1 comment:
haaa kuna aina ya baba wakwe na wajomba wakwe nao wa kukaa nao mita 100
Post a Comment