ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, March 20, 2013

Mchakamchaka Taifa Stars; Samata, Ulimwengu watua TZ kwa mtiti wa Morocco J’Pili

Mshambuliaji wa Taifa Stars, Mbwana Samata akijaribu kumtoka beki Said Nassor ‘Cholo’ wakati wa mazoezi ya kujiandaa ya mechi ya kimataifa ya kufuzu fainali za Kombe la Dunia dhidi ya Morocco. Picha na Jackson Odoyo.

Dar. Wapachika mabao wa Timu ya Taifa (Taifa Stars), Mbwana Samata na Thomas Ulimwengu wanaocheza soka la kulipwa katika Klabu ya TP Mazembe ya DR Congo, wamewasili nchini na kujiunga na nyota wengine wa timu hiyo tayari kwa maandalizi ya mechi dhidi ya Morocco.
Stars na Morocco (Simba wa Atlas) zitakwaana katika pambano la kusaka tiketi ya kuzufu fainali za Kombe la Dunia litakalopigwa Jumapili hii kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Kutua kwa washambuliaji hao kunafanya idadi ya wachezaji walioripoti kambini kufikia 20 kati ya 23 walioitwaa baada ya mshambuliaji Khamis Mcha aliyekuwa na kikosi cha  Azam FC nchini Liberia naye kuripoti jana mchana.
Mshambuliaji John Bocco na makipa Mwadini Ally na Aishi Manula, ambao pia walikuwa Liberia na kikosi cha Azam FC walitarajiwa kuripoti jana jioni.
Akizungumza mara baada ya kuwasili, Samata alisema ushindi dhidi ya Morocco ni lazima, hivyo Watanzania wasiwe na hofu na timu yao na wao wako tayari kuliongoza jahazi hilo la ushindi.
‘‘Tumekuja kuungana na wachezaji wenzetu wa Timu ya Taifa, tumekuja kuhakikisha timu yetu inashinda na tuna kila sababu ya kushinda maana tunacheza nyumbani,’’ alisema Samatta ambaye aliifungia Tanzania bao la ushindi dhidi ya Cameroon mapema mwaka huu.
Alisema kuwa wao wako fiti na hawana tatizo lolote na wanajiunga na kambi usiku huohuo waliowasili na kuanza mazoezi kama ratiba ilivyo pangwa na hivyo Watanzania wajiandae kushangilia ushindi. Stars na Morocco zipo Kundi C katika kinyang’anyiro hicho ambacho pia kuna timu za Ivory Coast na Gambia.
Mwananchi

No comments: