Waziri Mkuu Raila Odinga
Mombasa. Waziri Mkuu Raila Odinga Jumatatu alidai kwamba muungano wake wa Cord ulishinda uchaguzi wa Machi 4 kwa kupata kura 5.7 milioni dhidi ya zile za muungano wa Jubilee ulioongozwa na Uhuru Kenyatta 4.5 milioni.Alidai kwamba uchaguzi huo ulikuwa na udanganyifu mkubwa kuliko ule wa mwaka wa 2007 ambao pia alidai alishinda kwa kura 60,000 mbele ya zile za Rais Mwai Kibaki.
Akiwahutubia wafuasi wa Cord waliokuwa na furaha maeneo ya Hola Changamwe mjini Mombasa Odinga alisema Wakenya wameamua kwamba haki yao watailinda. Akitoa mfano wa busara ya mfalme Solomon kwenye Biblia ambaye alitoa hukumu kwamba, mtoto mchanga atakwe na kila mmoja wa wanawake wawili waliokuwa wakizozana juu yake atwae nusu ya mwili, Odinga alisema wakati huu haiwezekani kuendeleza dhuluma.
“Mfalme Solomon aliamua kwamba mtoto akatwe katikati na akina mama wawili waliokuwa wakizozana kila mmoja achukue nusu. Lakini yule mama wa kweli akasema afadhali mtoto apewe yule mama mlaghai kuliko kumuona mwanawe akiuawa. Hivyo ndivyo ilivyokuwa kwangu mwaka wa 2007”, alisema.
Odinga aliuongoza umma kwa kuimba, “rejesha mtoto wetu, rejesha mtoto wetu, rejesha mtoto wetu” na kuwataka Uhuru na makamu wa rais-mteule William Ruto kung’atuka uongozini mara moja.
“Namwaambia ndugu yangu Uhuru kwamba yeye bado ni mdogo na kwamba baba yake alikuwa Rais wa nchi hii kwa miaka 15. Ajue Wakenya hawawezi kuongozwa kwa nguvu. Uhuru huwezi kujilazimisha juu ya Wakenya”.
Alisema Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) ilifanya dhambi kubwa kuliko ile ya ECK ya marehemu Samuel Kivuitu mwaka wa 2007.
“Nawaahidi Wakenya kwamba mtaona maajabu kutoka mahakamani. Wizi na ulaghai na ufisadi na ujanja vilikithiri mno wakati wa uchaguzi huo ulioibiwa”, alisema.
Alisema endapo kutakuwa na uchaguzi awamu ya pili, Cord itapinga usimamizi wa IEBC na kutaka kamati huru kusimamia uchaguzi huo.
Alisema alitembelea Mkoa wa Pwani kuwashukuru wapigakura “kwa kupigia kura Cord na mimi kwa fujo”. Aliwaambia wabaki watulivu huku Mahakama Kuu ikiendelea na kesi hiyo ambayo alisema anaamini Cord itashinda.
Mwananchi
No comments:
Post a Comment