ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, March 27, 2013

MIMBA NI KIGEZO CHA KUOANA?-3


NAZUNGUMZIA mambo ambayo hutokea sana kwenye jamii yetu. Ni kawaida na hutokea mara kwa mara. Ni juu ya msichana kupata mimba kabla hajaingia kwenye ndoa. Ana ‘boyfriend’ wake, kwa bahati ‘nzuri’ anashika mimba...kinachofuata baada ya hapo mara nyingi huwa ni msichana kuwaza au kutaka kuolewa na hata kuhamia kwa mwanaume wake.
Si kwa upande wake pekee, bali hata wazazi au walezi wake, huwa hawataki kusikia kitu chochote zaidi ya msichana kwenda kwa mwanaume mwenye ‘mzigo’ uliopo tumboni mwa mwanamke huyo.
Yapo mengi sana ya msingi ya kujadiliana kabla ya kuchukua uamuzi huo. Pengine hujawahi kufikiria athari ambazo msichana anaweza kuzipata au kujiweka kwenye hatari kutokana na uamuzi huu wa wazazi au binti mwenyewe. Ngoja leo nizungumze na wazazi sambamba na walezi. Twendeni pamoja...

WAZAZI/WALEZI
Kwanza kabisa wazazi na walezi wanapaswa kufahamu kwamba, jukumu la kumlinda na kumpa mwongozo sahihi binti yao ni lao (hasa mama). Tuacheni woga na kuendelea kudhani watoto wetu ni wadogo mpaka tunaposhtukia mimba matumboni mwao.
Wasichana wenye umri wa miaka 14-16 siku hizi ni wakubwa...wanajua kila kitu. Kizazi hiki cha Sayansi na Teknolojia kipo wazi sana. Hujifunza mambo mengi peke yao huko kwenye mitandao.
Vunja ukimya, zungumza na binti yako kuhusu uhusiano, magonjwa na ujauzito. Mpe mwongozo sahihi, usimtishe, mweleze ukweli kuhusu mapenzi. Mwanaume akimfuata na ‘uongo’ wake, inakuwa rahisi kwake kujua na kumkabili.
Tatizo tunawaacha mabinti zetu tukiamini ni wadogo na kuogopa kuwaeleza ukweli, mwanaume akimtokea na maneno matamu anayoyasikia kwenye filamu za Kizungu, haraka anakubali, ukija kushtuka mtoto ana mimba!
Ikitokea bahati mbaya mwanao amepata mimba kabla ya wakati, usitumie ukali – usimfukuze nyumbani. Kaa naye chini, tumia sauti ya taratibu na uzungumze naye juu ya mimba yake. Atakueleza ukweli.
Tumia wazee wenzako kukutana na wazee wa upande wa pili ili kujadiliana kuhusu suala hili. Usimfukuze aende kwa mwanaume huyo. Siyo sahihi. Suala la kuishi pamoja linahitaji maridhiano ya ndani kabisa. Si kulazimishana. Anaweza kupata athari nyingi sana kwa kumlazimisha aende kwa mwanaume ambaye pengine hajawa tayari kuwa naye.
Wape muda, kutaneni na kijana na mumsikilize lengo lake. Kama ni jambo la ‘bahati’ mbaya na hawakuwa na mipango ya ndoa, basi asikilizwe, alee mimba na mtoto wake. Kama ni kuoana wataoana tu.
Ni kuwapa nafasi na kuwafanya waone kitendo walichokifanya ingawa hakikuwa sahihi lakini si aibu wala dhambi kubwa mbele ya jamii. Si ajabu siku zijazo, wakati mapenzi yanaendelea kuchanua, vijana hawa wakaamua kuungana katika ndoa. Inawezekana na mifano ipo mingi kwenye jamii yetu.

ATHARI ZA KUJIPELEKA
Kwa kiasi kidogo sana, hebu twende tukaone athari za binti kujipeleka kwa mwanaume au kwa kutaka mwenyewe au kwa kulazimishwa na wazazi au walezi wake.
Yapo mengi, lakini kubwa zaidi ambalo nataka kulizungumzia hapa ni kutokupata mapenzi ya dhati. Kwa sababu mwanaume atakuwa anajua ‘amesukumiwa’ hatakuwa na mapenzi ya dhati kwa mwanamke wake hata kama ni kweli mwanzoni alikuwa akimpenda.
Ni rahisi kunyanyaswa na hatakuwa huru kwa mwanaume wake. Wakati mwingine hutokea mwanaume kupoteza kabisa hisia za mapenzi kwa mwanamke wake na hivyo kukaribisha usaliti kwenye uhusiano wao.
Msingi wa yote, suala la kuishi pamoja ni la maridhiano. Lazima wote wawili wawe tayari kwa hilo. Ridhaa ikikosekana wakati mwingine husababisha hasira na mwanaume huweza kuamua kumtelekeza mwanamke wake kwa makusudi na kukimbilia sehemu nyingine.
Kimsingi wazazi wawe makini na jambo hili, wanaweza kudhani wanawasaidia mabinti zao kwa kuwatengenezea maisha bora ya mbele kumbe wanawaingiza kwenye mwanzo wa mateso katika maisha yao yote.
Wiki ijayo itakuwa sehemu ya mwisho, zaidi nitakazia kwenye athari za utoaji mimba na njia bora zilizokubalika za kujikinga na mimba. Wewe ni rafiki mzuri sana kwangu lakini utakuwa mzuri zaidi kama wiki ijayo utakuwa hapa kumalizia mada hii, USIKOSE!

Joseph Shaluwa ni Mshauri wa Mambo ya Mapenzi anayeandikia Magazeti ya Global Publishers. Ameandika Vitabu vya True Love, Let’s Talk About Love na All About Love vilivyopo mitaani.

1 comment:

Anonymous said...

Hiyo ni kweli kabisa,wanawake wengi sana wanadhani mtu akikupa mimba ndio atakuoa au unajipeleka kwake 99.5% kwa kweli utaumia wewe mwanamke kwasababu kama unavyosema hapo juu wanawake wengi WANASUKUMIZIA huo ni UKWELI,ooooo nikipata mimba ya DJ LUKE atanioa,haaaahaaaahaaaa,dada,dada,dada utakamatwa wewe hutomkamata bwana,kisha hutopanda mapenzi asilimia 100 nakuhakikishia kama hamkuwahi kudiscuss wala nini wewe tageti yako kuzaa la LUKA tu,sasa kitakunukia kwasababu yeye hajajipangaaaaaa na lazima atakua na wake wa nje na utasha anakupiga chini na mtoto wako anamuoa kidawa,lol.Utakimbilia chadisapoti,chadisapoti sio jibu kama ukitafakali,yeye alipe pesa tu,wewe amani huna kutwa hospitali na mtoto bebi sita shule na kazalika sasa pesa ya chadi sapoti haina samani hapoooooo utu ni samani mama utahangaika mwenyeweeee sasa yeye ahangaike nini wakati anakulipa pesa/madada ni nwakati wa kuamka ZINDUKA.MIMBA SI KIGEZO CHA KUOLEWA.Angalieni sana.Acheni kusukumizia wanaume mimba hamuolewi wengi wenu.Halafu noma inakuja ushazaa na jamaa anakubwaga anaoa mwingine na wewe unabaki unatoa mimacho wa kukuoa huna labda upate mwanaume aliyedivozi au ana watoto ka wewe au uwe na bahati tu asiwe na mtoto lakini mostly kuna masimango hata ya ndugu,nani akuoe ushazaa nje ya ndoa?huu ni ukweli DJ usibania komenti yangu ya ukweli na haina matusi wala chuki ila ni ukweli mtupu,hii topic imenigusa sana.Asante sana mpwa.