Nakwenda kwenye mada; nazungumzia suala la mimba au ujauzito kwa maneno mengine. Hivi, hujawahi kusikia msichana akilazimishwa kuolewa kwa sababu amepata mimba? Je, hujawahi kusikia msichana aking’ang’aniza ndoa baada ya kuwa amepata mimba?
Bila shaka ni mambo ambayo umekutana nayo katika jamii inayokuzunguka. Kama halijawahi kukukuta moja kwa moja basi hata kwa ndugu, jamaa au rafiki zako. Hilo ndilo nililolipa nafasi ya kulijadili leo katika ukurasa huu.
KWA NINI TUNAJADILI?
Kwa bahati mbaya sana wengi wetu tumekuwa na tabia ya kujadili mambo ambayo tayari yameshakuwa matatizo. Hapa namaanisha kwamba, baada ya tatizo kutokea ndipo tunapotafuta ufumbuzi.
Mfano, wasichana wengi siku hizi huwa hawajali sana suala la matumizi ya kondom kwa sababu tu tayari ameshafahamiana na patna wake kwa muda wa miezi miwili mitatu – tayari wameshaaminiana!
Jambo hili siyo sawa kabisa na ndiyo maana leo tunajadili jambo hili. Unajua wanawake wakati wakikubali kukutana na wenzi wao bila kinga wala tahadhari yoyote huwa hawafikirii kabisa suala la kupata ujauzito lakini ikishatokea ndiyo wanatafuta utatuzi.
Ndugu zangu, kuna utatuzi gani hapo zaidi ya kuzaa? Hapo sasa ndipo linapoibuka suala la baadhi kukimbilia kutoa! Athari zake hapo ni nyingi na leo sitazingumzia kwanza.
UPO USHAHIDI
Tusiende mbali sana, ngoja nikupe ushuhuda huu; wasichana tisa kati ya 10 wanaonipigia simu kuomba ushauri, katika maelezo yao huwa wanaeleza wazi kuwa hawatumii kinga yoyote wala tahadhari ya kujihami na mimba.
Sababu nyingi zinazotolewa na wasichana hao ni kwamba wanaaminiana. Wengine huthibitisha kuwa wameshafanya hadi kipimo cha ukimwi hivyo hakuna shaka ya kutumia kinga. Ukiuliza kuhusu mimba, hubaki kujiumauma!
TAZAMA SASA...
Baada ya hayo yote niliyoeleza hapo juu, twende kwenye kiini chenyewe sasa. Hapa namzungumzia mwanamke ambaye tayari ameshapata ujauzito kabla ya ndoa. Ni mimba ya boyfriend tu. Hapa ndipo mahangaiko yanapoanzia.
Msichana anahaha, tena mbaya zaidi wazazi au walezi wake wanakuwa wameshatambua kuwa binti yao ni mjamzito. Swali la kwanza binti kuulizwa na wazazi wake litakuwa: “Hiyo mimba ni ya nani?”
Akimtaja tu baasi! Atapelekwa mkuku huko au atafukuzwa na kutakiwa aende kwa mwanaume wake au busara itatumika kuzikutanisha familia mbili lakini lengo likiwa moja, vijana hao waunganishwe.
NI SAHIHI?
Kwa hakika siyo sahihi hata kidogo. Kwa maamuzi ya haraka mzazi anaweza kuona njia nyepesi ya kumuondolea aibu nyumbani kwake ni kumuoza au kumpeleka binti yake kwa mwanaume aliyempa mimba lakini athari zake ni nyingi – tutaziona baadaye.
Suala la kuoana ni maridhiano ya ndani kabisa. Inawezekana vijana hao kwa kudanganyana kwao au kwa kutokuwa makini kumewafanya wajikute tayari wapo kwenye matatizo. Inawezekana kipaumbele cha uhusiano wao haikuwa ndoa.
Vijana wanapaswa kupewa muda wa kutafakari kwanza tatizo ambalo limejitokeza ambalo kwa hakika limetokea kwa uzembe wao wenyewe. Nasema uzembe kwa sababu kwanza hairuhusiwi watu walio nje ya ndoa kukutana kimwili.
Pili, pamoja na kukiuka utaratibu huo hawakuwa makini kujikinga na upatikanaji wa mimba hiyo. Hilo ni tatizo lao ambalo wanapaswa kujadiliana pamoja. Si ajabu uhusiano unaweza kuwa mzuri kwa binti kupata matunzo mazuri na baadaye kujifungua kisha taratibu nyingine (kwa hiyari yao) za ndoa zikafuata wote wakiwa na furaha na tendo hilo.
Si jambo zuri mwanamke kujipeleka kwa mwanaume kwa sababu tu amepata mimba. Vilevile si sahihi kumfukuza binti au kumlazimisha mwanaume aliyempa mimba aishi naye tena wakati mwingine bila ya ndoa kwa sababu tu amepata mimba.
Wiki ijayo nitakuwa hapa ambapo nitafafanua athari ambazo zinaweza kujitokeza ikiwa binti ataolewa/ataishi kilazima kwa mwanaume aliyempa ujauzito. Pia nitatoa ushauri kwa wanawake juu ya nini cha kufanya ili kujiweka salama katika hatari ya kupata mimba zisizotarajiwa.
Joseph Shaluwa ni Mshauri wa Mambo ya Mapenzi anayeandikia Magazeti ya Global Publishers, ameandika Vitabu vya True Love, Let’s Talk About Love na All About Love vilivyopo mitaani.
2 comments:
Wanawake wenzangu tuliangalie hilo.mie binafsi nilizaa na jamaa mtoto wa kwanza,tukawa tunaishi wote bila ndoa nikitegemea iko siku,mara mtoto wa pili!!heeeh ndoa kimya,sasa yaliyonikuta,nimezaa watoto wawili na bwana kaniacha kaoa mwingineee,nimebaki gaaa,hii ni habari yangu ya kweli,kwahiyo kuzaa nje ya ndoa si vizuri na kuzaa ukitegemea kuolewa sahau hilo,ni wachache sana wana bahati hiyo.Ila nashukuru mungu ananitunza na wanangu.Lakini bado mpweke.Kumbuka kuzaa na mtu sio kuolewa nae,
Wanawake wenzangu tuliangalie hilo.mie binafsi nilizaa na jamaa mtoto wa kwanza,tukawa tunaishi wote bila ndoa nikitegemea iko siku,mara mtoto wa pili!!heeeh ndoa kimya,sasa yaliyonikuta,nimezaa watoto wawili na bwana kaniacha kaoa mwingineee,nimebaki gaaa,hii ni habari yangu ya kweli,kwahiyo kuzaa nje ya ndoa si vizuri na kuzaa ukitegemea kuolewa sahau hilo,ni wachache sana wana bahati hiyo.Ila nashukuru mungu ananitunza na wanangu.Lakini bado mpweke.Kumbuka kuzaa na mtu sio kuolewa nae,
Post a Comment