Uongozi wa Sekondari ya Seminari ya Kiislamu Katoro, Wilaya ya Bukoba, mkoani Kagera, umesema Tume ya Waziri Mkuu ya kuchunguza matokeo mabaya ya kidato cha nne, haitaleta majibu sahihi kama haitawahusisha wakuu wa sekondari nchini.
Akizungumza ofisini kwake juzi, Mkuu wa shule hiyo, Sheikh Fakharudin Mustafa alisema tume haiwezi kuwa na jipya, kwani wenye majibu sahihi ya matokeo mabaya ya kidato cha nne ni wakuu wa shule. Hata hivyo, Sheikh Mustafa alisema wakuu wa shule hawajahusishwa kwenye tume iliyoundwa na Waziri Mkuu.
Alisema majibu yanayotafuta yangeweza kupatikana kwa siku moja kwa kuwakutanisha wakuu wa sekondari nchini na kwamba, hakuna tume iliyowahi kuundwa na kuleta majibu yasiyo na mkanganyiko.Pia, Sheikh Mustafa alisema hakuna haja ya kuwasingizia walimu na wanafunzi kwa matokeo mabaya ya mwaka jana, wakati Serikali haijarekebisha mfumo mbovu uliopo kwenye Baraza la Mitihani katika usahihishaji na upangaji matokeo.
Alisema kama waziri angekuwa ni kiongozi anayewajibika hakutakiwa kupokea matokeo yenye kasoro, badala yake angeunda tume kutafuta ukweli wa tatizo na kupata ufumbuzi wake
Pia, alitaka Baraza la Mitihani kuwa wazi katika utendaji kuanzia usahihishaji hadi upangaji madaraja ya kufaulu na kwamba, suala hilo halifahamiki hata kwa wakuu wa sekondari.
Mwananchi
No comments:
Post a Comment