ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, March 28, 2013

Rais Tucta ang’olewa

Mambo siyo shwari ndani ya Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (Tucta) kutokana na kutimuliwa kwa Rais wake, Ayoub Omar.
Omar alilithibitishia gazeti hili jana kuwa aliondolewa wadhifa huo kwenye kikao cha Kamati ya Utendaji cha Tucta kilichofanyika Machi 25, mwaka huu.
Alisema kuwa alivuliwa wadhifa huo baada ya kuundiwa zengwe na viongozi wenzake waliodai asingeweza kuendelea na wadhifa huo kwani hakuwa na sifa.
Katiba ya Tucta inaelekeza kuwa kiongozi wake lazima awe mwajiriwa katika sekta ya umma au ile ya binafsi.
Omar alisema kuwa viongozi wenzake walikuja na ajenda kuwa hakuwa na kazi kwani alikuwa amestaafu kwenye Kiwanda cha Mbolea cha Mbeya alikokuwa anafanya kazi.
“Ni kweli nilistaafu pale Kiwanda cha Mbolea lakini nilipata ajira sehemu nyingine baada ya muda mfupi,” alieleza Ayoub, ambaye kwa sasa anafanya kazi kwenye Kampuni ya Nuru Enterprise.
Ayoub alisema alisikitishwa na kitendo kile kwani anaona ni zengwe tu kwani ana sifa za kuongoza kwa kuwa ni mwajiriwa.
“Mimi naheshimu uamuzi wao ila niliwapelekea vielelezo kuwa mimi ni mwajiriwa lakini walikataa,” aliongeza Ayoub, ambaye anaendelea na wadhifa wake kama Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi wa Viwandani (Tuico).
Katibu Mkuu wa Tuico, Nicolaus Mgaya alipoulizwa kuhusu suala hilo, alikanusha vikali kuenguliwa kwa mwenyekiti wake.
Gazeti hili, hata hivyo, linafahamu kuwa suala hilo limesababisha mgawanyiko mkubwa ndani ya Tucta.
Mwananchi

No comments: