Rabat, Morocco. Kipigo cha mabao 3-1 walichokipata Morocco kutoka kwa Taifa Stars Jumapili kimezua sokomoko nchini humo na kumweka kwenye mazingira magumu kocha Rachid Taoussi pamoja na vyombo vya habari.
Kocha wa zamani wa Morocco, Badou Zaki akizungumza na kituo cha redio cha jijini Casablanca “Radio Mars” alisema uchaguzi wa wachezaji wa Taoussi umechangia kwa sehemu kubwa kufungwa na Tanzania 3-1 katika mchezo wa kusaka kufuzu kushiriki Fainali za Kombe la Dunia 2014 zitakazofanyika nchini Brazil.
Zaki alisema alishangazwa na kikosi cha mwisho kilichoteuliwa na Taoussi kwa ajili ya mchezo dhidi ya Tanzania, huku akisema kipigo walichokipata walistahili kabisa kutokana na uteuzi mbovu wa wachezaji.
Kocha huyo aliongeza kuwa uteuzi wa wachezaji haukuangalia uzoefu, ila walichagua wachezaji chipukizi waliohitaji kufanya kazi ya ziada ili kuwa kwenye kiwango cha kucheza mashindano muhimu kama haya.
“Uteuzi dhidi ya Tanzania ulionekana kuwa na shaka na kushangaza zaidi,”alisema kocha Zaki.
Pia kocha huyo alivilaumu vyombo vya habari kwa kushinikiza kutumika zaidi kwa wachezaji wanaocheza soka la ndani ya Morocco.
Pia kocha huyo alivilaumu vyombo vya habari kwa kushinikiza kutumika zaidi kwa wachezaji wanaocheza soka la ndani ya Morocco.
“Tunapaswa kujua siyo kila mchezaji wa ndani yupo tayari kwa ajili ya kucheza mechi za ushindani wa kiwango cha juu, kucheza mechi za mashindano ya kufuzu kushiriki Kombe la Dunia, “alisema kocha Zaki.
Naye Waziri wa Vijana na Michezo wa nchi huyo, Mohamed Ouzzine aliandika kwenye ukurasa wake wa Facebook akisema, “hiki ndicho tulichokuwa tukijaribu kukitafuta kwa zaidi ya mara moja.
Tunazungumzia matokeo haya na kusahau mfumo wetu mbovu. Hiki ndicho tulichokuwa tunakisema kila siku kwenye Bunge kwamba hakuna juhudi zozote zinazofanywa kuisaidia Morocco kupata matokeo mazuri. Hii ni kwa sababu hatujafanya juhudi za makusudi kutengeneza msingi wetu na tuna safari ndefu mbele yetu.”
“Mkutano mkuu wa shirikisho la soka utakaa mwezi ujao, baada ya hapo tutakuwa na mwanzo mpya na damu mpya,” aliongeza Waziri huyo.
Mwananchi
No comments:
Post a Comment