ANGALIA LIVE NEWS

Monday, March 4, 2013

MTANGAZAJI MORO AVAMIWA NA MAJAMBAZI, AJERUHIWA

Na Dunstan Shekidele, Morogoro
MTANGAZAJI mahiri wa Top Redio ya mkoani hapa, Edward Abeid Mganga amenusurika kifo baada ya kuvamiwa na majambazi sita waliokuwa na silaha za jadi ambazo ni mapanga, marungu na visu.

Majambazi hao walimvamia mtangazaji huyo saa 11 alfajiri ya Ijumaa iliyopita eneo la Kiwanja cha Ndege mkoani hapa, alipokuwa akielekea kazini akiwa anatembea kwa miguu.
Akizungumza kwa tabu na gazeti hili akiwa nyumbani kwake, Sabasaba Mganga alisema baada ya kuvamiwa na majambazi hao walimkaba, kumjeruhi tumboni kwa kitu chenye ncha kali na kumshushia kichapo kisha kumpora huku wakimtishia kummaliza kwa silaha zao za jadi.
“Baada ya kunipiga sana na kunipora nilianguka chini na kupoteza fahamu, niliokotwa na wasamaria wema na wakanipeleka ofisini kwangu, nilipofika meneja alinikimbiza Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro.
“Cha ajabu tangu nilipofikishwa hospitalini saa 12 asubuhi, sikupewa huduma yoyote mpaka saa 5 tulipoamua kwenda hospitali binafsi ambapo nililazwa na kutoka leo (Jumamosi) baada ya kupata nafuu,” alisema mtangazaji huyo.
Ofisa mmoja wa polisi ambaye hakutaka kutajwa jina kwa kuwa siyo msemaji alisema wanaendelea na upelelezi ili kuwanasa waliomfanyia unyama huo.
GPL

No comments: