NINA furaha kwa sababu nina afya njema na wewe Mungu umeendelea kunipigania. Umekuwa mwaminifu kwangu siku zote na mwepesi wa kunihurumia na kunisamehe. Nimekukosea mara nyingi lakini huhesabu, hakika neema zako ni za milele.
Marafiki zangu leo tunafikia mwisho wa mada yetu iliyozunguka hapa kwenye uwanja wetu kwa majuma manne yaliyopita. Jambo la kufurahisha zaidi kwako ni kwamba, leo tunakwenda moja kwa moja kuona mbinu za kujipandisha thamani.
Huko nyuma tumejifunza mengi, dalili na madhara ya kushushwa thamani. Kimsingi thamani hushushwa na mhusika mwenyewe kutokana na tabia zake. Nilifafanua vizuri sana katika matoleo yaliyopita.
Mbinu zifuatazo kwa hakika zitakusaidia sana kukuweka juu kithamani kwa mpenzi wako. Utakuwa bora na utapewa kipaumbele katika kila jambo. Habari njema kwako katika hili ni kwamba, utamuweka mwenzako katika mawazo ya kuishi pamoja na wewe. Karibu tujifunze marafiki zangu wapendwa.
KUWA MSHAURI
Nataka niseme wazi kabisa kwamba, wasichana wengi hujidharau na pengine huhisi kuwa hawawezi kuwa na mawazo mazuri kwa wenzao. Sikia nikuambie; kama kuna jambo lenye thamani katika maisha ya uhusiano ni pamoja na kusaidiana mawazo.
Wakati mwingine msichana anaweza kuwa na mawazo mazuri lakini akaogopa kuyatoa kwa sababu tayari yeye si wa thamani tena. Mfano, wasichana wengi wanapenda sana kupiga ‘mizinga’ kwa wapenzi wao, wengine ikiwa ni muda mfupi tu baada ya kuanzisha uhusiano. Ukiwa namna hiyo huwezi kuwa na thamani.
Nimekutana na kesi nyingi sana za namna hiyo. Wapo wanaoomba ushauri kuwa wapenzi wao hawawatunzi, wakiomba pesa hawapewi, kwani siku zote kabla yake ulikuwa unaishi vipi? Jifunze kuishi kwa kujitegemea.
Mwanaume anakuwa na amani zaidi kama akitoa fedha au kumsaidia mpenzi wake kwa uamuzi wake – siyo kuombwa. Tafsiri inayokuwa nyuma yake ni kuhonga. Kama anakuhonga ana haja gani ya kukuweka kwenye ratiba zake za mbele?
Kwa hakika hawezi kuwa na sababu hiyo. Ili kuepusha yote hayo na kujiweka katika nafasi ya kuwa mshauri wake mkuu, badilisha tabia yako. Jambo hili ni vyema likaanzia mwanzo kabisa wa uhusiano.
ACHA MAISHA YA VIFICHO
Baadhi ya watu wanapenda kufanya mambo yao gizani. Anaishi maisha ya kificho na wakati mwingine anadanganya maisha yake halisi na kuonesha picha nyingine kabisa mbele ya mpenzi wake. Hili ni tatizo.
Mwanaume ukianza kuonesha dalili kwamba penzi lenu ni la siri au unaficha ukweli wa familia yako nk, anakutoa thamani. Mwoneshe mwenzako ulivyo. Usifiche mambo yako. Mathalani una tatizo fulani la kimaisha, usimfiche, mwambie mapema.
Kumwambia kutamfanya kwanza aone unampenda, humfichi na una malengo naye ya baadaye. Ni wazi kwamba kama ungekuwa humpendi na huna malengo naye ya baadaye ungemficha maisha yako.
Kuwa wazi kutamfanya akupandishe thamani maradufu akijua kuwa amekutana na mtu sahihi. Jitahidi kuwa wazi kwa kadiri uwezavyo ili uendelee kujipandisha thamani zaidi na zaidi.
MSAIDIE
Kipengele muhimu ambacho hudhihirisha mapenzi ya dhati na kuingia ndani kwa haraka zaidi ni kusaidiana. Yapo mambo mengi ya kusadiana lakini najua wengi mmekwenda moja kwa moja kwenye fedha.
Msaada au kusaidiana siyo kwenye fedha pekee. Kati ya mambo ya msingi zaidi ya kumsaidia mwenzako ni pale anakupokuwa mhitaji. Mathalani anaweza kuwa na tatizo na fedha, lakini lazima ujiulize ni kwa ajili ya nini?
Usije ukampa fedha ya kwenda disko au kulewa baa ukadhani utakuwa umejipandisha thamani, la hasha! Nazungumzia juu ya mambo ya msingi kabisa ambayo mwenzako atayakumbuka siku zote na kukuzidishia thamani yako.
Jitahidi kumsaidia kadiri unavyoweza utakuwa juu kithamani, si tu kwamba ataona penzi lako la dhati kwake bali pia atafahamu kuwa mwanamke aliyenaye si wale wa kusubiri kupelekewa tu!
SASA UNAWEZA KUJIWEKA KATIKA KILELE CHA THAMANI
Vipengele vilivyopita bila shaka vimekupa mwanga mpya katika maisha yako ya kimapenzi. Sina shaka sasa kwamba, utakuwa umejiweka katika kilele cha thamani. Mpenzi wako hawezi kukudharau na atajua anaishi na mwanamke sahihi.
Ni suala la kujifunza, kuelewa na kuchukua hatua. Kazi yangu ya kuandika imeishia hapa katika mada hii, sasa kazi imebaki upande wako, kuamua kuchukua au kuacha kama ulivyosoma. Nitakuwa hapa tena wiki ijayo na mada nyingine nzuri zaidi, USIKOSE!
Joseph Shaluwa ni Mshauri wa Mambo ya Mapenzi anayeandikia Magazeti ya Global Publishers, ameandika Vitabu vya True Love, Let’s Talk About Love na All About Love vilivyopo mitaani.

No comments:
Post a Comment