ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, March 6, 2013

Wanne mbaroni uchochezi wa kidini nchini

Kamanda wa Polisii Jeshi la Polisi Kanda maalum ya Dar es Salaam, 
Suleiman Kova
Jeshi la Polisi Kanda maalum ya Dar es Salaam, linawashikilia watu wanne kwa tuhuma za kujihusisha na uchochezi wa kidini.

Kamanda wa Polisi wa Kanda hiyo, Suleiman Kova, alisema jana jijini Dar es Salaam kuwa watu hao walikamatwa katika msako maalum wa kushtukiza.

Aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Kombo Hassani Zuberi (32), mkazi wa Mburahati Barafu, ambaye inadhaniwa kuwa ndiye kiongozi wa mtandao wa uchochezi maeneo mbalimbali nchini.Wengine ni madereva Basote Hassan Tandala (24) mkazi wa Gongo la Mboto, Mohamed Hassan Shariff (33), mkazi wa Tabata Bima na Salum Athman Mahambi (46) , mkazi wa Tunduma mkoani Mbeya.

Kamanda Kova alisema mtuhumiwa Kombo ni miongoni mwa waliokuwa wanatafutwa kwa muda mrefu na kuwa katika upekuzi nyumbani kwake alikutwa na nyaraka mbalimbali alizokuwa akisambaza Tanzania Bara na Visiwani.
“Kundi hili pamoja na watu wengine ambao bado wanatafutwa limebainika kuwa na mtandao na mawakala sehemu mbalimbali nchini, Jeshi la Polisi linaendelea na msako mkali jijini na nchini kote, ili kuwabaini wanaojihusisha na uchochezi kwa lengo la kuleta vurugu na uvunjifu wa amani,” alisema.
CHANZO: NIPASHE

No comments: