ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, March 19, 2013

Nini Hatma ya Jumuiya za Watanzania na Siasa za Vyama Vingi Ughaibuni?


Wapendwa Watanzania wenzangu tunaoishi nje ya Tanzania kwa wakati huu, napenda kuwashukuru kwa moyo wenu wa umoja, upendo na mshikamano mliokuwa nao kama Watanzania. Suala la upendo, umoja na mshikamano kwa watanzaia sio suala la kutafutiza  ni suala lionekanalo wazi popote walipo watanzania.  Umoja. ucheshi, utani, matumizi mazuri ya lugha yetu ya Kiswahili ni mambo ambayo kwetu kama Watanzania tunayaona madogo lakini ni mambo ambayo wezetu kutoka bara la Afrika na mabara mengine wanayaona ni ya pekee kwetu.  Ndio maana hapa hapa napenda kuwapongeza ndugu zetu wa Washington-Marekani walioamua kwa moyo mmoja kufungua darasa la Kiswahili kwa watoto ambao aidha wazazi wao ni Watanzania au kwa wale ambao wameona hizi tunu tulizo nazo Watanzania.  Watanzania bila kificho sisi ni wamoja, wapenda watu na wachangafu muda wote.

Nilipata bahati ya kusoma na Wakenya, Waganda na Wakongo, kwa bahati mzuri ndugu zetu hawa wanabahati ya kujua lugha ya Kiswahili. Jambo moja ambalo walikuwa wanashangaa ni ni jinsi gani ninavyotumia lugha hii kwa maisha ya kawaida. Mfano nilipokuwa nataka kumwomba mtu kunichukulia kitu nilisema ‘…..naomba unipatie kitabu kile’ au ‘samahani naomba ….’ au nashukuru kwa…’ ndugu zangu hawa walikuwa wanashangaa kwanini natumia lugha ya namna hiyo. Na jambo dogo kama hilo linatufanya watanzania kuwa wa pekee na kuendeleea kuwa mfano mzuri kwa wengine. Hiyo ndio sifa ya Mtanzania.


Kwa uzuri na umoja wetu ambao asili yake uwezi kuitenganisha na Watanzania wenyewe, yaani ni kitu kilichomo ndani mwetu. Tumekua na kulelewa katika asili ya umoja na mshikamano. Kwa mantiki hiyo Watanzania wanapotoka Tanzania na kwenda kwenye nchi za kigeni mara nyingi uendeleza umoja na mshikamano huo. Toka nilipoanza kusoma mitandao ya kijamii nimeshuhudia jumuiya mbali mbali za Kitanzania toka sehemu mbali mabli hapa duniani. Nikitaja chache, Jumuiya ya Watanzania huko Italia, Uingereza, Uholanzi, Ubeligiji, Afrika ya Kusini, Ujerumani na hapa tulipo yaani Marekani kuna Jumuiya ya Watanzania New York, Washington hali maarufu DMV, Midwest, Texas (Dallas, na Huston)  na Jumuiya nyingi nyinginezo za Kitanzania.

Cha kufurahisha zaidi,kupitia jumuiya hizi za kitanzania , Watanzania wamekuwa wakikutana kama Watanzania na kujadili yaliyo ya Kitanzania. Tumekutana wakati wa misiba, sherehe mbali mbali kama harusi, siku zetu za kuzaliwa, Eid al Fitr, Eid Mubarak, Noeli, Pasaka, Siku ya Tanzania Kupata uhuru, Mapinduzi Zanzibar, Mei Dei, na matukio mengineyo kama Rais wetu mpendwa akifika kutusalimia, au kiongozi yeyote kutoka nyumbani Tanzania.

Mambo hayo yote mazuri tunayafanya kama Watanzania, wenye kupendana, kushikamana na kushirikiana. Kwani tufanyapo hayo matukio uwa kwa namna moja au nyingine yanatuleta pamoja kama Watanzania tuliopo nje ya Tanzania na kutuunganisha na Watanzania wenzetu walioko Tanzanzia.

Lakini ndugu zangu watanzania, hivi karibuni kwa muono wangu kuna kitu kinaibuka kati yetu na kama tusipokuwa makini hatima ya jambo hili laweza kuondoa uzuri wote ambao nimeulezea toka mwanzo. Hakuna hata siku moja kwa miaka minne iliyopita nilipokuwa kwenye jumuiya za Watanzaia aidha hapa Marekani au  Ulaya nilipokwisha ulizwa WEWE NI CHAMA GANI?au WANAOTAKA KADI ZA CHAMA FULANI WANIONE BAADAE. Ndani ya miaka ya hivi karibuni maswali haya yameanza kuulizwa kwa uwazi kabisa bila kificho katika JUMUIYA ZA WATANZANIA. Swali kwa ninyi ndugu zangu Watanzania, ni  nini nia ya maswali haya au kauli hizi kwenye jumuiya zetu?

Ngoja nitoe mifano ya matukio mawili yanayoyambatana na hiki ninachokielezea,  yaani Umoja wa Watanzania kwa upande mmoja na Vyama vya Siasa kwa upande mwingine. Mwaka jana tulisikia mugogoro mkubwa uliojitokeza kati ya Wanajumuiya ya Watanzania huko Washington-DMV, na mgogoro huo ulichochewa na kile kilichosemekana na kuchanganya kazi ya Vyama vya Siasa na Jumuiya ya Watanzania, wale viongozi wenye tamaa ambao wanataka kuwa pande mbili mbili yaani awe kiongozi wa Chama cha siasa na huku  ni kiongozi wa Jumuiya ya Watanzania. Baba wa Taifa alisema watu hawa ‘..waogopeni kama ukoma…’ Hawa si Watanzania wa kweli ndugu zangu, ni watu waliojawa na tamaa, ningewaomba muwafukuzie mbali haraka sana kabla hawajatuharibia uzuri wa umoja na mshikamano wetu Watanzania. Watu hawa ni kama ugonjwa wa kansa, unakula ndani kwa ndani.

Mfano mwingine ni uchaguzi wa juzi wa Viongozi wa Chama kimojawapo cha siasa huko huko DMV, jamani jamani ni aibu Watanzania. Yaani tumeingiwa na tamaa kiasi hicho. Au raha yenu ni kutambulishwa kwenye mikutano mikuu ya vyama hivyo kama Diaspora. Maana baadhi yenu tuliwaona mkitambulishwa huku mkiinua pua zenu juu.  Acheni  ujinga huo mara moja. Tuacheni tuendelee kushikamana kama watanzania, acheni kutugawa Watanzania, pelekeni tamaa  zenu huko, au ondokeni mara moja kwenye jumuiya zetu. Ni aibu na uchuro kwa jumuiya zetu Watanzania.

Historia inatuonesha kwamba vyama vya siasa vilivyoanzishwa nje ya nchi husika  au vilivyokuwa na mwendelezo mpaka nje ya nchi yaani kuwa na matawi nje ya  nchi vilikuwa vyama vya kimapinduzi. Na mifano ya vyama hivyo tunayo, kama Chama cha Mapinduzi Haiti kilianzishwa nchini Marekani, Chama cha Mapinduzi cha Cuba kilichopata msukumo kutoka Urusi, Umoja wa Vijana wa Uturuki ulioanzishwa huko Mashariki ya Kati kwa ajili ya mapinduzi huko Uturuki, na vingi vinginevyao. Vilianzishwa au vilifungua matawi yao nje ya nchi zao ili  kuamashisha  ukombozi wa nchi zao. Watanzania kitu gani tunataka kukomboa kwa hivi vyama vya siasa?

Ndugu zangu vyama vya siasa vya nini kwenye Jumuiya zetu za Kitanzania huku ughaibuni? Najua Tanzania ni nchi huru, ni nchi ya kidemokrasia, na inayotoa fursa kwa kila Mtanzania kuanzisha chama cha siasa huko Tanzania na si kwingineko. Ndugu zangu mlioingiwa na shetani huyu wa vyama uondoeni uchuro kwenye jumuiya zetu na tuacheni na umoja wetu watanzania. Ndugu zangu tupo ugenini , kinachotuleta pamoja ni Utanzania na wala si chama cha siasa. Mnaotaka vyama vya siasa rudini Tanzania mkagombee uongozi wa kisiasa. Na sisi wapenda umoja na wanaopenda kuimarisha jumuiya zetu za kitanzania watupeni nje watu hawa.

Watanzania tutaendelea kuwa pamoja endapo kila mmoja wetu anayependa kutambulishwa kama Mtanzania kupigana kwa nguvu zote ili kuondoa ugonjwa unatuingilia  taratibu kwenye jumuiya zetu, ugonjwa wa kutaka tuanze kutambulishana kwa kadi za vyama vya siasa. Nafungua ukurasa kwa kila Mtanzania aliyopo Ughaibuni kutoa maoni na kutafakari kwa makini jambo hili.

Umoja na Mshikamono Daima!!!!!  Asanteni Ndugu zangu Watanzania

12 comments:

Anonymous said...

Kwa kweli nakubaliana na wewe kwa kiasi kikubwa. Nilikuwa najiuliza hili swali kila siku, nini maslahi haswa ya hili jambo. Sikuona ni jinsi gani ukiwa huku unaweza kusaidia chama chako kule Tanzania. Nilichoona ni jinsi gani sote tukiwa kama Watanzania tunaweza kufanya nini kuleta mabadiliko Tanzania bila kujali itikadi za chama. Kama kweli umeamua kuikomboa Tanzania "kisiasa" basi unatakiwa uiongie kwenye "field" na siyo kupiga kelele ukiwa mbali. Askari mzuri ni yule aliyeingia vitani akashinda, na siyo kukaa mbali na kusema eti ulikuwa vitani. Watanzania tuliopo ughaibuni tunahitaji "Utanzania" na siyo "U-CCM" wala U-Chadema. Isifke mahali tukashindwa kualikana nyama choma kwasababu ya itikadi zetu. Au ifike mahali hata mkeo au mumeo mnanuniana kwasababu za itikadi. Mungu ibariki Tanzania

Anonymous said...

Ndugu yangu umeongea vizuri sana. Nakushukuru sana kwa muda wako mwingi na upeo wako wa kuona mbali. Inawezekana ikawa siyo tatizo sana kuanzisha vyama vya siasa ughaibuni na wakati huohuo kuheshimu zile jumuiya zinazotuunganisha watanzania wote. Cha kushangaza hapa DMV ni kuwa watu wana-take things 'personal'. Kiongozi wa chama cha siasa anajiona yuko juu ya uongozi wa jumuiya, kitu ambacho kwakweli hakipendezi. Wakati mwingine tupanga hata shughuli za vyama vya siasa siku ambyo wanajukuiya walishapanga kukutana na kufanya shughuli yao. Mashindano ya nini ndugu zangu watanzania? Tupendane na tuwe kitu kimoja. Tuhudhurie shughuli za jumuiya bila kujali kuwa sisi ni viongozi wa vyama vya siasa au la. Tupo mbali na nyumbani ndugu zangu. Ni sisi hawahawa ndiyo tutakaozikana.

Anonymous said...

Naungana na wewe mdau katika hili.

Anonymous said...

WEWE NANI ALIKUAMBIA UKIWA KWENYE CHAMA FULANI BASI WEWE SIO MWANA JUMUIYA ?/SIASA ZA HAPA NI KITU KIZURI SANA KWANI HAPA WAPO WATANZANIA WENGI SANA NA NI KHAKI KABISA MTU KUPENDA CHAMA CHAKE NA KUWA WAZI JUMUIYA NI YA KILA MTANZANIA NA KUCHAGUWA CHAMA NI UPENDELEO WA MTU NI VITU AMBAVYO HAVIINGILIANI WALA MTU ALAZIMISHWI KABISA WEWE HAUPENDI SIASA MWAMBIE MTU SIPO NA CHAMA CHOCHOTE KWANINI UNAONA NI KITU KIBAYA

Anonymous said...

KWANZA ULIVYOANZA KUWEKA CCM KWANZA UMENIFURAHISHA KWELI KUWA UNATAMBUWA CCM NI NUMMBER ONE BIG UP CCM

Anonymous said...

We're ndugu uliandika swala hili,yaani nakuunga mkono moja kwa moja,Mimi naona njaa inasumbua Watu,sasa hivi vyama ambapo asilimia kubwa ya Watu ,hats Havana uwezo wa kwenda nyumbani Tanzania ,ili wakapige kura za Hivyo vyama vyao,Jamani wengi waliopo hapa waliondoka nyumbani sababu maisha magumu ,Fanyeni jitihada za kutatua njaa kule bongo,sio kuanzisha chuki na uadui wa siasa ,Umoja ni Nguvu,Utengano ni Udhaifu.

Anonymous said...

Ndugu mtoa maada,

Ahsante kwa maoni yako ambayo kwa kiasi fulani yanamtizamo chanya. Hata hivyo, ingawa ninakubaliana na wewe kuwa si vizuri kuchanganya shughuli za jumuia za kitanzania zisizo za kisiasa zilizo nje ya nchi na shughuli za vyama vya kisiasa, katu sikubaliani na wewe kwamba matawi ya vyama vya kisiasa nje ya Tanzania ni sawa na ugonjwa wa kansa. Kama mtizamo wako ni sahihi, basi shughuli za vyama vya kisiasa popote pale, ndani au nje ya Tanzania, ni hatari kwa umoja na mshikamano wa watanzania na ingebidi zisiendeshwe. Mtizamo huo ni wa kidikteta. Kuwa mwanachama wa chama cha kisiasa, ndani au nje ya nchi, ni political orientation ya mtu kama ambavyo mtu anaweza akawa muumini wa dini ya kiislam au kikristo akiwa ndani au nje nchi. Kuna hatari kwamba siku moja utasema watanzania tuishio ughaibuni hatuna sababu ya kuwa waumini wa dini yoyote. Kitu muhimu kwetu ni kwamba shughuli za jumuia za kitanzania (zisizo za kidini au kisiasa) zisichanganywe na shughuli za kisiasa au kidi. Period.

Anonymous said...

Wow, naungana na mtu aliyeandika mada hii. Kwanza nikupongeze kwa muda wako pia unaonekana una upeo sana wa kufikiri...nimeipenda sana hii. Mimi naishi hapa Boston nadhani Jumuiya zetu ni muhimu sana kuliko hivi vyama.

Anonymous said...

Where's the freedom of association? How does this differ from dictatorship? How is religious affiliation different than political affiliation in this context or should we prepared for a next proposal that we dump our religious affiliations?

Anonymous said...

MHHHH MAKUBWA HAYA WAJEMENI, KWELI SIASA NA JUMUIYA HAVIWEZI KAA AU WEKWA MAHALI PAMOJA KAMA HUJUI KUPAMBANUA MAMBO. JUMUIYA NI MKUU KULIKO SIASA, NISAWA NA LUGHA YETU YA KISWAHILI NI KUU KULIKO LUGHA ZA MAKABILA MBALI MBALI PALE TZ. UKIELEWA HAPA WEWE JUMUIYA HUTAPATA SHIDA MTOTO KATI YA WATOTO WAKO WENGI AKIJIDAI NA KUKUDHARAU ATIII!!!. JK NYERERE ALIFANYA KAZI KUBWA SANA HAPA DUNIANI HASA PALE TZ, TO LET SO MANY DIFFERENT PEOPLES( TZS ) TO COME TOGETHER AS ONE!!!!!!. HIVYO NI SAWA NA KUSEMA SIASA NA JUMUIYA VYAWEZA KAA PAMOJA SABABU NI MZAZI NA MTOTO.
SIASA ANAMIPAKA YA KUWALETA WATZ PAMOJA, ANATAKIWA KUWALETA WANACHAMA WAKE TUU TENA WANAOPENDEZWA NAE NA KUMPENDA YEYE BALI JUMUIYA ANAUWEZO WA KUWALETA WOTE BILA MIPAKA YOYOTE ILE. ILA HUYU JUMUIYA WA DMV NAE ANAJISHUSHA HADHI HASA KWA KUJIENDESHA KAMA MTOTO (SIASA) HASA ANAPOTANGAZA KWAMBA ANA WATU HAI NA WASIO HAI. TAFADHALI BUNI MBINU MPYA ZA KUJIENDESHA ZISIZO ZA KISIASA, JIENDESHE KAMA SERIKALI. SIASA ENDELEA NA LIBENEKE LAKO LA UONGO MWINGI HUKU NAWE MZAZI ( JUMUIYA) USILALE USINGIZI, SABABU WEWE NI KIMBILIO LA WOTE. MTOTO HAKUI KWA WAZAZI WAKE.
MUNGU IBARIKI TZ NA WATU WAKE AMENI.
Ni mimi mzee wa siku

Anonymous said...

Ni wakati kweli tukaelezana na kukumbushana yaliyotuleta huku siasa haina nafasi kabisa ughaibuni

Anonymous said...

Ndugu mtoa mada..kwanza umeanza vizuri na imeweza kuonesha manufaa ya umoja wa kitanzania, lakini imemaliza vibaya kwa kukashifu na kuhukumu baadhi ya Watanzania hao hao uliyokuwa unawasifia hususan wanaCCM. Sasa kwa taarifa yako Vyama vya Siasa ughaibuni sasa ni wakati wa mwafaka kwa sababu idadi ya Watanzania wanaoishi nje ya nchi (Diaspora) imefika karibu 2Million, sasa wewe huoni umuhimu wa kuhusisha hii idadi kubwa kwenye mustakabali wa taifa letu? Njia nzuri ya kuwahusisha ni kupitia Vyama vyao vya siasa kwani ndiyo njia nzuri ya kupata mawazo mbadala, kuwahusisha wataalam waliyo bobea kwenye fani zao, kutafuta viongozi wenye maona (exposure), kupata watanzania wawekezaji n.k haya yote yanaweza kuwa faida ya kusogeza vyama vya siasa nje. Vile vile lazima uelewe kuwa hii pia ni njia nzuri ya kusukuma mahitaji yetu kama uraia pacha, upigaji kura n.k kwani chama kinachotawala kinaweza shawishiwa na wanachama wake kutekeleza sera kama hizo. Hivyo basi usikimbilie kuhukumu bali jaribu kupanua upeo wako.