ANGALIA LIVE NEWS

Sunday, March 24, 2013

Rage akwepa tena mkutano Simba

Mwenyekiti wa Simba, Ismail Rage, ambaye alipigiwa kura ya kutokuwa na imani na wanachama zaidi ya 600 wiki iliyopita, ameendelea kupiga dana dana kutaja tarehe ya mkutano mkuu wa klabu hiyo.

Baadhi ya wanachama wa Simba ambao hawaridhishwi na mwenendo mbovu zaidi wa timu yao ya soka tangu katikati ya miaka ya 1980, waliitisha mkutano wa dharura mwishoni mwa wiki iliyopita na kutangaza mapinduzi ambayo hayakuwa na nguvu hata hivyo.

Mkutano mkuu wa dharura wa wanachama huo uliitishwa kwa nguvu kufuatia kitendo cha Rage kukwepa kuitisha mkutano mkuu kama alivyoombwa na wanachama hao tangu timu yao ifungwe bao 1-0 na Mtibwa Sugar kwenye ligi kuu ya Bara Februari 24.

Kipigo hicho kilikuwa ni moja ya matokeo mabovu mfululizo yaliyoanzia mwishoni mwa duru la kwanza la ligi kuu, mwaka jana, na kuendelea kwa sare mbili na kipigo kimoja katika mechi tano za kwanza za duru la pili ikiwamo ya Mtibwa.

Akizungumza jijini jana, Rage ambaye uongozi wake umeshapoteza makamu mwenyekiti na mjumbe mmoja wa kuchaguliwa wa kamati ya utendaji ambao walijiuzulu aliwataka wanachama kutulia na mpaka Jumatano atakapotangaza tarehe ya mkutano mkuu.

Rage aliyerejea kutokana matibabuni India alisema

"Jumatano nitatoa tamko la lini mkutano utafanyika.

"Wanachama wasiwe na hofu na watulie tu. Mkutano utafanyika."

Si mara ya kwanza kutoa ahadi kama hiyo, hata hivyo.

Awali aliahidi kutekeleza ombi la wanachama hao baada ya mechi za kimataifa za Simba mwezi uliopita ambapo timu hiyo ilifungwa jumla ya mabao 5-0 na timu isiyojulikana Afrika ya Recreativo Libolo ya Angola.

Aidha, alipoulizwa kama atakuwa tayari kujiuzulu nafasi hiyo kama ambavyo baadhi ya wanachama wamekuwa wakitaka, Rage alisema hawezi kuzungumzia jambo hilo kwa kuwa anachokifikiria kwa sasa ni kuitisha mkutano huo wa wanachama.

Wakati Rage akitoa ahadi nyingine ya siku ya kutangaza tarehe ya mkutano huo mkuu, Makamu Mwenyekiti Geofrey Nyange ambaye pia alikuwa Mwenyekiti wa Kamati fedha ya klabu alishaachia ngazi.

Mwingine aliyejiuzulu ni Mwenyekiti wa kamati ya usajili, Zacharia Hanspope.

Viongozi hao walijiuzulu kwa madai ya kutoridhishwa na hali ya mambo ndani ya klabu hiyo, na kuna uwezekano mkubwa Rage akang'olewa kwa kura ya kutokuwa na imani katika mkutano huo unaosubiriwa kwa hamu na wanachama wengi wa Simba.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

No comments: