Akitoa madai hayo, Edna Mjema, (pichani), aliyekuwa amelazwa katika hospitali hiyo Jumapili iliyopita, alidai kucheleweshewa matibabu na kupigwa wakati alipopelekwa katika chumba cha upasuaji.
Alisema alikuwa na ujauzito wa miezi sita na kuwa baada ya kufika hospitalini hapo walimpa dawa na kumtaka arudi Machi 18 kwa ajili ya kufanyiwa kipimo cha ultra sound.
“Nilipofika nyumbani nilikunywa dawa nilizopewa ila hali yangu ilizidi kuwa mbaya na ndipo saa 11 ya alfajiri ilinibidi nirudi hospitalini hapo kwa ajili ya kuwajulisha hali yangu,” alisema.
Alisema kabla ya kwenda katika hospitali hiyo, Machi 13, mwaka huu alikuwa akitokwa na maji na kwenda katika zahanati ambapo alipewa dawa.
Mjema alisema Machi 16, akiwa anamaliza dawa alizopewa alipatwa na maaumivu na kumlazimu kurudi katika kituo cha afya.
Alisema pale alipewa rufaa ya kwenda hospitali ya Amana na alipofika hospitalini hapo alienda katika wodi ya wazazi ambapo manesi walimtaka aende wodi namba nne kwa kuwa alikuwa hajafikia miezi ya kujifungua.
Hata hivyo, alisema alipofika kwenye wodi namba nne hakuna aliyempokea na kuamua kujitafutia kitanda mwenyewe na kulala.
“Nikiwa nimelala kwenye kitanda hicho, alikuja nesi na kuniondoa na kunieleza kuwa kitanda hicho ni special (maalumu) kwa watu wanaotoka chumba cha upasuaji, ikanibidi niondoke na kwenda katika kitanda kingine ambacho kilikuwa kipo wazi,” alisema.
Alisema akiwa kwenye kitanda hicho hakupata huduma yoyote na kila alipowaita wauguzi hakuna aliyemjali.
Mjema alisema hali yake iliendelea kuwa mbaya hadi saa 9 alasiri aliposhindwa hata kugeuka na kwamba mpaka muda huo hakuna huduma yoyote aliyoipata.
Alisema ndugu zake walimjulisha ndugu yao ambaye ni daktari wa Tumbi kuhusu hali ya ndugu yao ya kutopata matibabu ambaye aliwasiliana na madaktari wa hapo na kuanza kupewa matibabu.
Hata hivyo, alisema daktari baada ya kufika alimtaka asukume kumtoa mtoto ambapo anadai hakuweza kufanya hivyo kutokana na kukosa nguvu na ndipo daktari huyo alipokivuta kiumbe hicho.
Alisema mtoto alitoka akiwa amefariki lakini kondo lilikuwa limekataa kutoka na ndipo daktari alipomuacha huku kondo likiwa limebanwa na mkasi.
Alisema wakati anajifungua ilikuwa ni saa 9 mchana na aliendelea kukaa na kondo hilo hadi saa 2 usiku alipopelekwa chumba cha upasuaji kwa ajili ya kuondolewa kondo hilo.
Mjema alisema wakati akiwa kwenye chumba cha upasuaji, daktari aliyemtaja kwa jina moja Dk.Kajura alimtaka aeleze kama alikuwa ametoa mimba huku akimpiga kwenye tumbo.
“Aliniambia sema ukweli wako kama umetoa mimba huku akinishindilia ngumi kwenye tumbo kila nikimueleza ukweli namuona hasira zake anazishushia kwenye tumbo langu. Daktari akasema kama haujatoa mimba basi utakuwa umeathirika,” alisema Mjema.
Alisema alifanyiwa upasuaji mkubwa kwa ajili ya kutoa kondo hilo na alielezwa kuwa kondo hilo lilikuwa limeingia hadi kwenye kizazi na kukipasua kizazi ambapo ilibidi kishonwe wakati akifanyiwa upasuaji.
Alidai kuwa baada ya kutoka chumba cha upasuaji majira ya saa 6 usiku aliwekewa damu pamoja na maji.
Alisema alipoamka aligundua kuwa damu haisogei na wala maji hayasogei na ndipo alipoomba msaada wa manesi ambao hawakumjali.
Alisema akiwa hospitalini hapo alikuwa na ndugu yake aliyekwenda kumsaidia na kuona tatizo hilo na kuanza kumrekebeshia dripu ili damu pamoja na maji ili yaweze kupita.
Alisema wakati ndugu zake wakilalamika kuhusu hospitali hiyo kuwanyima huduma kwa wakati, waliambiwa kuwa wanaweza hata wakaenda mahakamani.
“Daktari alituambia kama mnataka muende mahakamani na wao wana uwezo wa kubadilisha faili la mgonjwa na kuandika jambo lingine na kwamba wao hawasimami mahakamani kwani wana wakili,” alisema.
Alisema ndugu zake walikuwa wakilalamika kutoridhishwa na huduma na baada ya kuwasilisha malalamiko yao ndipo walipotishiwa kuwa watawafungulia kesi kwa ajili ya kutoa mimba.
Hata hivyo, alisema baada ya kuona hakuna huduma, ndipo ndugu zake walitaka kumuondoa katika hospitali ya Amana na kumpeleka katika hospitali nyingine ambapo suala hilo lilizuilika na kujulishwa kuwa watafunguliwa kesi ya utoaji mimba.
Mjema alisema tangu akiwa na ujauzito wa miezi miwili alikuwa akisumbuliwa na matatizo ya kutokwa na damu ya hedhi.
Mgonjwa huyo ambaye aliruhusiwa kurudi nyumbani Machi 21, mwaka huu, anaeleza kuwa bado hali yake haipo vizuri kwani anapata maumivu makali kwenye tumbo.
Mama Mzazi wa mgonjwa huyo, Nafadhai Kituma alisema ameshangazwa na kitendo cha hospitali hiyo baada ya kutoa malalamiko yao na kuwabadilikia kwa kumtuhumu binti yake kuwa ametoa mimba. “Baada ya kulalamika huduma kuwa mbovu, wanatutishia watatufungulia kesi kuwa mwanangu katoa mimba kwanini tangu mwazo hawajasema hilo hata sisi hatuogopi kufunguliwa hiyo kesi wale madaktari wanatuona sisi ni wakuja tunajua haki zetu eti anatueleza wana uwezo wa kubadilisha kile alichoandika katika faili na kuandika jambo jingine kwa kuwa wana uwezo huo,” alisema
Kituma alisema mwanae tangu muda mrefu alikuwa anatamani kupata mtoto kwani mtoto wake wa kwanza kwa sasa ana miaka 9, sio hospitali ilazimishe kuwa ametoa mimba.
Alisema hawajafurahishwa na vitendo alivyofanyiwa mtoto wake ikiwamo kupigwa na daktari pamoja na kucheleweshewa kutolewa kwa kondo.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Hospitali ya Amana, Dk. Meshack Shimwela, alipoulizwa kwa njia ya simu juu ya tukio hilo alikanusha mgonjwa huyo kupigwa.
Alisema kile walichokiona ndani ya upasuaji na kile alichokieleza ni tofauti na kwamba hospitali yake imefanya jitihada kubwa kuokoa hali ya mgonjwa huyo.
“Akithibitisha kwa maandishi nitakueleza kile ambacho tumekiona kwani kuna miiko ya kazi ambayo hainiruhusu kuzungumzia labda mgonjwa mwenyewe akubali,” alisema.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI
No comments:
Post a Comment