ANGALIA LIVE NEWS

Sunday, March 10, 2013

REDD’S ORIGINAL YAWAFUNDA MAWAKALA WA SHINDANO LA REDD’S MISS TZ 2013


Mwandaaji wa shindano la Urembo la Redd's Miss Kanda ya Kati, Mama Salome Kiwaya akichangia Mada katika Semina hiyo iliyofanyika mwishoni mwa wiki kwenye Ukumbi wa Jetty, uliopo ndani ya Hoteli ya Girrafe, Mbezi Beach Jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi wa Ukuzaji Sanaa kutoka Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA), Vivian Shalua akisisitiza jambo wakati wa ufunguzi wa Semina ya Mawakala wa Mashindano ya Urembo ya Redd's Miss Tanzania 2013 iliyofanyika kwenye Ukumbi wa Jetty, uliopo ndani ya Hoteli ya Girrafe, Mbezi Beach Jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki. Kulia ni Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni Lino International Agency ambao ni Waandaaji wa Shindano la Miss Tanzania, Hashim Lundenga na Kushoto ni Afisa Habari Mkuu wa Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA), Agnes Kimuage.
Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni Lino International Agency ambao ni Waandaaji wa Shindano la Miss Tanzania, Hashim Lundenga akitoa Mada kwenye Semina ya Mawakala wa Mashindano ya Urembo ya Redd's Miss Tanzania 2013 iliyofanyika kwenye Ukumbi wa Jetty, uliopo ndani ya Hoteli ya Girrafe, Mbezi Beach Jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki. Wengine pichani ni Mrembo wa Redd's Miss Tanzania 2012/13, Brigit Alfred na Mrembo aliyeshika nafasi ya tatu, Eda Sylvester.
Meneja Masoko wa Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) ambao ni Wadhamini Wakuu wa Redd's Miss Tanzania, Fimbo Butallah akitoa ufafanuzi juu ya Mada ua Udhamini na Wadhamini wakati wa Semina ya Mawakala wa Mashindano ya Urembo ya Redd's Miss Tanzania 2013 iliyofanyika kwenye Ukumbi wa Jetty, uliopo ndani ya Hoteli ya Girrafe, Mbezi Beach Jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki.

MSIMU mwingine wa shindano la kumpata malkia wa Tanzania 'Redd's Miss Tanzania 2013' umeanza hapa nchini kwa mawakala kutoka sehemu mbalimbali kuja jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki na kushiriki semina maalumu iliyoandaliwa na waratibu wa ngazi ya taifa kampuni ya Lino International Agency.
Waratibu hao kwa kushirikiana na maafisa kutoka katika Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) waliendesha semina kwa mawakala wote walioteuliwa kuandaa mashindano ya urembo kuanzia ngazi ya vitongoji hadi kanda na semina hiyo ilikuwa na lengo la kuwapa mafunzo kwa kuzingatia taratibu, kanuni na sheria za shindano hilo.
Shindano hilo ndilo pekee lenye nafasi ya kutoa mwakilishi wa nchi katika fainali za dunia kila mwaka ambapo mrembo hupata nafasi ya kutangaza jina la nchi na vivutio mbalimbali vya utalii na utamaduni vilivyoko hapa nchini.
Hata hivyo uzinduzi rasmi wa shindano hilo unatarajiwa kufanyika mwishoni mwa wiki hii kwa mdhamini mkuu Redd's Original kutangaza udhamini wake na mchakato utakavyoendeshwa kuanzia ngazi ya vituo hadi taifa.
Akizungumza kwenye semina ya mawakala, Mkurugenzi wa Ukaguzi wa Sanaa wa Basata, Vivian Shalua, alisema kuwa mawakala wanatakiwa kuzingatia nidhamu za washiriki kwa sababu nidhamu ndio msingi wa kila jambo.
Shalua alisema kwamba nidhamu ya shindano hilo iliposhuka ilipoteza mvuto wa sanaa hiyo kuanzia kwa jamii inayotuzunguka hadi kwa taasisi na makampuni mbalimbali ambayo hujitokeza kudhamini mashindano ya urembo hapa nchini.
Afisa huyo alisema kwamba ni vyema mawakala wa ngazi za chini kushirikisha warembo wenye nidhamu na kutoona aibu kuwaengua washiriki ambao kuanzia hatua ya awali wanaonekana kutoheshimu sanaa hiyo na kutowapa nafasi ya kuichafua.
"Napenda kuwaambia kwamba kwa sasa nidhamu imeanza kuimarika na wazazi na walezi wamekuwa wanakubali kutoa ushirikiano katika ushiriki wa mabinti zao, hata mimi binti yangu (hakumtaja jina) alishawahi kushiriki mashindano haya," alieleza kiongozi huyo.
Aliwataka pia mawakala kuhakikisha wanakuwa na vibali kutoka kwenye ofisi husika pamoja na kutumia kampuni zilizosajiliwa kisheria katika kuendesha mashindano yao.
Naye Mratibu wa taifa, Hashim Lundenga, aliwataka mawakala hao kuhakikisha wanatafuta washiriki wenye vigezo ili hatimaye ngazi ya fainali kuwa na warembo wenye ushindani.
Lundenga alisema kwamba anataka kuona ushindani uliokuwepo miaka ya nyuma unarejea katika sanaa hiyo ambapo hadi siku ya fainali ilikuwa ni vigumu kujua nani atakayeibuka mshindi wa taji hilo.
Alisema kwamba ni vyema mwaka huu mawakala wakasaka warembo wenye vigezo vya ushindani na kamwe wasiangalie kiwango cha elimu peke yake.
"Nataka irejee hali kama ushindani ilivyokuwa wakati wa Mbiki Msumi na Angella Damas au Wema Sepetu na Jokate Mwegelo," alitoa mfano Lundenga.
Mkurugenzi wa Masoko wa kampuni ya bia Tanzania (TBL), Fimbo Butalla, aliwaambia mawakala hao kwamba ni lazima wazingatie makubaliano yaliwekwa kati yao na waandaaji wa taifa.
Butalla alisema kwamba ili kutangaza kinywaji cha Redd's Original ambacho ndiyo TBL imekiteua kudhamini mashindano hayo ili kufanikisha malengo yaliyowekwa na kukuza soko la kinywaji hicho maalum kwa wanawake.
Aliwatakia mawakala wote mafanikio kuelekea mashindano yao ya mwaka huu.
Mrembo kutoka katika kitongoji cha Sinza, kanda ya Kinondoni, jijini, Brigitte Alfred, ndiye mrembo anayeshikilia taji hilo la taifa aliyelitwaa kutoka kwa Salha Israel wa Ilala.
Mwaka jana kalenda ya mashindano hayo ilibadilika ambapo Kamati ya Miss Tanzania ilieleza kuwa mshindi Brigitte ataiwakilisha nchi katika mashindano ya dunia mwaka huu na mrembo atakayeshinda taji hilo baadaye mwaka huu atashiriki fainali hizo za dunia mwakani.
Lundenga alisema kuwa lengo la mabadiliko hayo ni kumpa mshindi nafasi ya kujiandaa vyema kushiriki fainali hizo zinazoshirikisha warembo kutoka nchi zaidi ya 100.
Nancy Sumary kutoka Kinondoni jijini Dar es Salaam ndiye mrembo anayeshikilia rekodi ya kufanya vizuri katika fainali za Miss World ambapo mwaka 2005alitwaa taji la Afrika.

No comments: