Timu ya uchunguzi wa matukio ya wanafunzi wa Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM) waliodai kufanyiwa vitendo vya ulawiti wakati wakiwa hosteli ya Kigamboni, imetoa matokeo ya ripoti yake jana na kubaini kuwa madai ya wanafunzi hao hayakuwa ya kweli.
Timu hiyo iliundwa baada ya wanafunzi wa chuo hicho kufanya maandamano Januari 14, mwaka huu kuelekea makao makuu ya jeshi la polisi nchini kupeleka malalamiko yao dhidi ya uhalifu na ulawiti uliokithiri maeneo yao.
Kufuatia maandamano hayo ambayo yalitulizwa kwa mabomu ya machozi, Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, aliunda timu ili kuchunguza madai ya wanafunzi hao.
Timu hiyo ilihusisha wapelelezi kutoka Polisi Kati, Temeke, Kigamboni, wanafunzi wanne, watendaji wa kata na wadau wengine.
Akitoa taarifa ya timu hiyo jana jijini Dar es Salaam, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Temeke, Engelbert Kiondo, alisema imebaini hakuna hosteli katika maeneo wanaoishi wanafunzi hao bali wanaishi nyumba za kawaida zenye wapangaji wengine.
Kamanda Kiondo alisema licha ya juhudi zilizofanywa na timu hiyo lakini hawajapokea taarifa zozote za kulawitiwa kwa wanafunzi hao.
Alisema katika suala hilo, timu ililazimika kutumia dawati la jinsia kama sehemu ya kupata taarifa za wanafunzi waliodai kufanyiwa vitendo vya kulawitiwa lakini hakuna aliyeripoti.
"Tunaamini suala hili lilipewa kipaumbele wakati wa maandamano ili kuleta mvuto na hamasa kwa jamii ili kuyafanikisha maandamano hayo," alisema.
Akifafanua kuhusu nyumba ambazo wanafunzi hao wamepanga, Kiondo alisema hazina usalama kwao na kwamba sio hosteli kama walivyokuwa wakiziita.
"Sehemu walizopanga ni makazi ya watu wengi, na sio nyumba moja ambayo imepangisha wanafunzi wa IFM bali wamechanganyika na wananchi, kwa hiyo ulinzi haupo," alisema.
Alisema kutokana na hilo vitendo vya wizi wa mali mbalimbali ambazo wanafunzi waliviripoti vimekuwa vikiitokea katika jamii nzima na sio wanafunzi peke yao.
Pia alisema timu hiyo imebaini kuwa wenye nyumba hizo hawajachukua hatua za usalama wa wapangaji wao.
Kuhusu kesi ambazo zimeripotiwa polisi, kamanda alisema mbili kati ya zote ndizo zilizofikishwa mahakamani na nyingine upepelezi wake umekuwa mgumu kufanyika kutokana na mazingira ya tukio lenyewe.
Mapendekezo ya nini kifanyike, Kiondo alisema IFM inapowadahili wanafunzi wake inatakiwa kuwahakikishia usalama wa mahali wanapoishi (hosteli).
Alisema tayari jeshi la polisi limefanya kazi ya kuhakikisha ya kutoa elimu kwa wanafunzi hao na jamii iliyowazunguka kuhusu ulinzi shirikishi na wameipokea.
Alisema wamewashauri wamiliki wa nyumba hizo kuweka ulinzi kwa sababu jeshi la polisi haliwezi kupeleka ulinzi kwa sababu kiutaratibu walitakiwa wawe na walinzi wao.
Pia alisema wametoa elimu kwa wanafunzi kuacha tabia ya kutembea mmoja mmoja badala yake wanapokuwa na mali watembee kwa vikundi ili usalama uwepo.
Kuhusu timu alisema kazi waliyoifanya itakuwa ni endelevu mpaka hapo chuo hicho kitakapokuwa na hosteli kwa wanafunzi wake.
Timu hizo zilikuwa zikifanyakazi ya kuchunguza madai ya wanafunzi ya kuvamiwa mara kwa mara na kuporwa mali na vibaka.
Nyingine ni madai ya vitendo vya ulawiti kwa wanafunzi hao ambavyo vilifanywa na vibaka hao na taarifa kuwa jeshi la polisi limeshindwa kuwachukulia hatua wahalifu hao.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI
No comments:
Post a Comment