ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, March 27, 2013

SAKATA LA ARDHI LOLIONDO:Mbunge naye atishia kuachia ngazi


Mbunge wa Ngorongoro, Kaika Saning’o Ole Telele (CCM), ameunga mkono maazimio ya wakazi  wa Loliondo, wenyeviti wa vijiji na baraza la madiwani, kupinga hatua ya serikali kumega eneo lao la ardhi la kilomita za mraba 1,500 na kulifanya kuwa eneo la mapito ya wanyama (ushoroba).

Taarifa ya maazimio ya mkutano huo, iliyosomwa na Diwani wa Kata ya Ololosokwani, Yannick Ndoinyo, na NIPASHE kupata nakala yake, ilisema: “Endapo serikali itatumia mamlaka yake ya kumega maeneo ya vijiji vyetu ili kuanzisha pori tengefu, sisi viongozi wote wa kisiasa kuanzia vitongoji hadi udiwani tutajiuzulu na kutafuta haki zetu kwa njia nyingine.”


“Kama kiongozi wenu, nawaambia jambo moja…kama sasa ni wakati mwafaka wa kujiuzulu nafasi za kisiasa, mimi nawaunga mkono lakini msije mkanitoa kafara kama awali nikipigania haki zenu wakati maboma yenu yalipochomwa moto.

“Kama sasa mnaona kuwa ni wakati mwafaka wa kujiuzulu kwa viongozi wote wa kisiasa, mimi nawaunga mkono…lakini naomba msije mkaniacha peke yangu, naomba wote tujiuzulu. Naunga mkono maazimio yenu ya kutetea ardhi yenu na endeleeni na kikao,” alisema.

Hata hivyo, aliongeza azimio moja la kuunda timu ya watu itakayokwenda kuonana na Rais Jakaya Kikwete, kuzungumzia suala hilo la ardhi yao.

Hata hivyo, wakati Telele akisema hayo, Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kushirikiana na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, zimesema zitatenga sehemu ya ardhi ya pori  tengefu la Loliondo la kilometa za mraba 1,500  kati ya kilometa za mraba 4, 000 ili kutatua migogoro huo.

Uamuzi huo wa Telele ambao aliutoa wakati akizungumza katika mkutano wa hadhara uliowakutaisha wakazi hao wakiwemo viongozi wao wa mila (malaigwanani), madiwani, wenyekiti wa vitongoji na vijiji na Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro, Elias Wawa Lali, ulikwenda tofauti na kauli ya Lali, ambaye aliwataka wananchi hao kutofanya mkutano huo kwa kuwa suala waliokukwa wakilizungumzia lilikuwa bado halijatolewa tamko na serikali.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Ngorongoro, Elias Ngorisa, alisema, “Tupo pamoja na wananchi kuhakikisha ardhi yetu haipokonywi kwa namna yoyote ile. Kipaumbele kwa mimi ni kuwatumikia wananchi hawa, hawa ndio walioniajiri mimi na katika hilo sipati kigugumizi kutetea ardhi ya wananchi,” alisema na kuunga mkono maazimio ya kikao hicho.

Kama hiyo haikutosha, madiwani waliokuwapo kwenye mkutano huo waliungana na mwenyekiti wao na kutamka kwamba wote watajiuzulu kama serikali itatekeleza azma yake ya kumega eneo lao.

Wakati sakata hilo likiendeleza, jana Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kushirikiana na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, zilitangaza kutenga sehemu ya ardhi ya pori  tengefu la Loliondo la kilometa za mraba 1,500  kati ya kilometa za mraba 4, 000 ili kutatua migogoro uliopo.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Waziri wa Maliasili na Utalii,  Khamis Kagasheki, alisema pamoja na kutatua migogoro iliyopo katika pori hilo,  lakini pia ni kunusuru ikolojia ya hifadhi za Serengeti, Ngorongoro na pori tengefu la Loliondo.

Pia alisema ni  kulinda mazalia ya wanyamapori, mapito ya vyanzo vya maji kwa ajili ustawi wa hifadhi hizo.

Kagasheki alisema wizara hizo mbili zinatarajia kufuatilia na kuona uhalali wa  kumiliki ardhi katika eneo hilo kwa baadhi ya kampuni na endapo itabainika kwamba kampuni hizo  hazikufuata hatua stahiki  katika kupata  hati milki  za ardhi,  hatua kali zitachukuliwa ikiwamo kufuta hati miliki zao.

Mbali na hilo,  pia alisema serikali itasimamia eneo litakalobaki kuwa pori  tengefu ambalo  litasimamiwa na vijiji vinavyozunguka hifadhi hiyo.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments: