ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, March 23, 2013

Serikali yafanyia kazi ombi la msamaha kwa ving’amuzi

Katibu Mkuu wa Wizara ya Sayansi na Teknolojia, Dk Florence Turuka, amesema Wizara ya Fedha, inalifanyia kazi ombi la makampuni yaliyopata zabuni ya uuzaji wa ving’amuzi nchini ili nayo yaweze kupata msamaha wa kodi.

Kauli hiyo imekuja baada ya swali lililoulizwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Miundombinu, Peter Serukamba, muda mfupi baada ya kamati yake kutembelea Mamlaka ya Mawasiliano nchini (TCRA).

Kamati hiyo pamoja na mambo mengine ilifika hapo kwa lengo la kujifunza mambo mbalimbali ikiwemo hatua ya serikali ya kutoka kwenye mfumo wa analogia na kuingia digitali.
Serukamba katika swali lake, alitaka kupata ufafanuzi kama kampuni ya Startimes hailipi kodi kama baadhi ya vyombo vya habari vilivyoripoti.

Akijibu swali hilo, Dk. Turuka alisema sio kweli kampuni hiyo hailipi kodi bali kilichotokea ni kwamba awali walipoomba kivutio cha uwekezaji walipewa kwa sababu maombi yao yalipitia Kituo cha Uwekezaji cha Taifa (TIC).

Alisema taarifa alizonazo, kivutio hicho kilimalizika mwezi Desemba mwaka jana na kampuni nyingine zinazouza ving’amuzi ziliomba kupata kivutio hicho ambapo Hazina inalifanyia kazi.

“Kampuni nyingine ziliandika barua kuomba hili na Hazina inalifanyia kazi kuona namna gani nao wataweza kupata kivutio hichi,” alisema.

Alisema katika harakati za kupunguza bei, serikali imeondoa kodi ya kuingiza ving'amuzi kutoka nje ya nchi.

Baada ya majibu hayo, Serukamba alisema lazima kampuni nyingine zipewe kivutio hicho ili kuwepo kwa ushindani wa kibiashara na kushuka kwa bei za ving’amuzi nchini.

Akijibu swali lingine la Serukamba ambalo lilitaka kujua ni nchi ngapi za Afrika Mashariki ambazo zimezima mawasiliano kama Tanzania inavyoendelea kufanya, Mkurugenzi Mkuu TCRA, Profesa John Nkoma, alisema Kenya walikuwa wafanye hivyo lakini kutokana na uchaguzi walisitisha.

“Tunaamini uchaguzi umeisha na baada ya kesi watatekeleza hili, ila wamekuja hapa wao na Uganda kujifunza tumefanyaje...tumewezaje,” alisema.

Aliongeza kuwa, siku zote waliondani huwa wanaangalia changamoto lakini watu wa nje wao wanakuja kujifunza jinsi gani Tanzania imeweza kutekeleza hilo.

Akifafanua kuhusu kauli ya mbunge wa Jimbo la Ileje Aliko Kibona kuwa upo ubishi baina ya chama cha Wamiliki wa Vyombo vya Habari nchini (MoaT), Wizara ya Habari na wadau wengine kuhusu kuhama kwenye mfumo wa analogia kwenda digitali, profesa Nkoma alisema, kamwe hilo halitaweza kurudisha nyuma kile walichokikusudia.

Katika ziara hiyo, baadhi ya wabunge walitaka kujua vigezo vilivyotumika kuvichagua vituo vya televisheni vitano nchini kurusha matangazo yake bure kwenye ving’amuzi ambapo Mkurugenzi wa TCRA, Profesa John Nkoma alisema hilo limefanyika kutokana na vituo hivyo kuwa na leseni ya Taifa.

MOAT CHASIKITISHWA NA MAJIBU YA SERIKALI
Katika hatua nyingine MOAT kimesikitishwa na majibu ya serikali kupitia kwa Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO), Asah Mwambene, yanayopotosha ombi lao kuhusu urushaji wa matangazo ya analojia sambamba na digitali kwa muda.

Taarifa iliyotolewa na Mwenyekiti wa MoaT, Dk. Reginald Mengi, ilisema “sisi kama Watanzania na wadau katika sekta ya habari tumetimiza wajibu wetu wa kutaarifu mamlaka husika na kuishauri kuhusu hali hii na namna bora ya kuimudu. Kwa masikitiko makubwa, majibu ya serikali yameelekea kujenga malumbano na kulazimisha kuwa hali iko shwari.”

Taarifa hiyo iliongeza kuwa Watanzania walio wengi wanajua hali halisi na ukweli wa jambo hilo na wataamua kulingana na utashi wao. Mwambene akumbuke kwamba pamoja na yale aliyosema ukweli utabaki pale pale.

Wakati huo huo, Mbunge wa kuteuliwa, James Mbatia, ameitaka serikali kushughulikia changamoto ya kuhama kutoka analogia kwenda digitali ili wananchi wapate haki ya kupata habari kwa mujibu wa sheria.

Mbatia aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuwa serikali inatakiwa kuacha kufanya ubabe katika suala hilo na kutatua changamoto zilizopo.

Aliitaka serikali iangalie uwezekano wa kutoa mikopo kwa vyombo vya habari ili kuwawezesha kununua mitambo ya moja kwa moja.

CHANZO: NIPASHE

No comments: