ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, March 27, 2013

Shibuda amshupalia Membe

Mbunge wa Maswa (Chadema), John Shibuda, ametishia kupeleka hoja binafsi bungeni dhidi ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, kwa kile alichodai kuna udhaifu katika usimamizi na utekelezaji wa Mpango wa Kujitathmini Kiutawala Bora kwa nchi za Afrika (APRM).

Shibuda alitoa kauli hiyo jana kwenye ofisi ndogo za Bunge, jijini Dar es Salaam wakati kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa ilipokutana na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, John Haule, na wajumbe wa Bodi ya APRM.

Alizijata kasoro zilizoonekana kwenye usimamizi kuwa ni Waziri Membe kushindwa kuonana na Wajumbe wa Bazara la Wawakilishi Zanzibar kwa ajili ya kuwaeleza umuhimu wa mpango huo na ushiriki wao kwenye suala hilo linalogusa maeneo mengi.


 Aidha, alisema kuwa kasoro nyingine ni Waziri Membe kushindwa kupeleka waraka wa kuomba kuwapo kwa bajeti kwa ajili ya APRM.

 Alisema Zanzibar ni sehemu ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, hivyo lazima iwe na uwakilishi wa kimantiki kwenye chombo hicho, lakini alisema kuwa Waziri Membe ameshindwa kutoa kipaumbele kwenye ushirikishwaji.

“Sisi ndio tunahamasisha masuala ya ushirikiano wa kimataifa, kwenye hili Zanzibar haijawakilishwa vyema, inatokana na Waziri kutoona umuhimu wa kuwashirikisha,” alisema.

Shibuda ambaye ni Mwakilishi wa Bunge katika APRM, aliitaka kamati hiyo kupeleka hoja kwa Spika wa Bunge, Anne Makinda, kumtaka kumuita Membe na kueleza ni lini atakwenda kuzungumza na Baraza la Wawakilishi, ili kuonyesha ushiriki wao kivitendo badala ya kinadharia kama ilivyo sasa.

“APRM ni suala mtambuka, Zanzibar wameomba kujiunga hadi wamechoka, tunataka tamko la Waziri ni lini ataenda, vinginevyo nitapeleka hoja binafsi ili Bunge limhimize rasmi kwenda Zanzibar kukutana na Baraza hilo ili lipate uwakilishi,” alisema Shibuda.

“Miaka mitatu sasa hakuna fungu kwenye bajeti kwa ajili ya mpango huu, utekelezaji wa shughuli zake unakuwa mgumu kila wakati, kupata fedha kunategemea huruma ya Waziri mwenye dhamana,” alisema na kuongeza:

“Walikuwa wapi siku zote wasipeleke waraka wa APRM kuwa na fungu lake, leo ndiyo tunaelezwa wapo kwenye mchakato wa kupeleka bungeni suala hilo.”

Aidha, Shibuda alisema hata uendeshaji wa mpango huo umekuwa wa kusuasua kwa maelezo kuwa katika siku za hivi karibuni wataalamu kutoka makao makuu ya mpango huo, Afrika Kusini walipofika kukagua mpango huo nchini, kiongozi wa nchi (Rais Jakaya Kikwete) hakuwa na taarifa.

Alisema ni aibu kwa Rais kushindwa kupewa taarifa ya kinachoendelea kwenye mpango huo, na hata walipohitaji ripoti hawakuipata hadi walipotumia mbinu za ziada ikiwamo kwenda Ikulu na kuletwa mbele ya kamati Januari, mwaka huu.

“Wakati mwingine tuwe wakweli, zipo kasoro za kimsingi katika usimamizi wa majukumu ya APRM, iweje wakaguzi wafike Tanzania Rais hana taarifa?” alihoji na kuendelea:
“Mimi siyo msemaji wake, lakini niliguswa sana kama mwakilishi wa Bunge.”

 Aliitaka kamati hiyo iagize Wizara hiyo itoe tathmini ya kasoro zilizokuwapo kuhakikisha hazijirudii katika siku za usoni.


Alisema kinachoonekana APRM haipewi uzito unaostahili kwenye Wizara hiyo, na kuonekana ni suala la ziada, huku umuhimu na mahitaji yake yanajulikana, lakini hakuna anayejali.

 Naye Mbunge wa Mji Mkongwe (CUF), Mohamed Ibrahim Sanya, alisema kwenye mpango huo Zanzibar imetengwa na hakuna ushirikishwaji wa karibu.

 Alisema katika kupima utawala bora, ni vyema uongozi wa APRM kuyafikia makundi ya wafungwa magerezani na kuwahoji, ikiwa ni pamoja na kuongeza ushirikishwaji wa wananchi kwenye masuala ya kiuchumi.

 Mbunge wa Mkwajuni (CCM), Hamad Yusuf Masauni, alisema Wizara haijaipa APRM kipaumbele kuonekana inapopewa fedha ni jambo la hisani.

“Ni lazima kuwe na kipaumbele kwenye hili, wananchi waelimishwe juu ya mpango huu, inawezekana iwapo kutakuwa na bajeti kwa ajili ya mpango huo,” alisema Masauni.
Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mussa Hassan Zungu, aliipongeza serikali kwa kukubali kuingia kwenye mpango huo kwani haikulazimishwa kutathminiwa na mataifa ya nje, jambo linaloonyesha uwazi kwenye utendaji kazi.

Zungu ambaye ni Mbunge wa Ilala (CCM), alisema kuingia kwa mpango huo kumesaidia katika mambo mengi likiwamo kupendekeza Tanzania kuandika Katiba Mpya.

Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Haule alisema suala la ushirikishwaji wa Baraza la Wawakilishi atalifikisha kwa Waziri Membe kwa ajili ya kufanyiwa kazi.

Haule alisema mpango huo ulianzia mbali na kwamba kasoro zilizojitokeza zitarekebishwa.

 
CHANZO: NIPASHE

No comments: