Mchezaji huyo nyota wa ‘Wanamsimbazi’, pia ametakiwa kuandika barua ya kujieleza ni wapi alikokuwa wakati wachezaji wengine wakiendelea kujifua kwa ajili ya mechi zao mbalimbali za Ligi Kuu ya Tanzania Bara.
Hatua hiyo dhidi ya Sunzu ilichukuliwa jana asubuhi na kocha wa Simba, Mfaransa Patrick Liewig, imemkumba pia mshambuliaji Abdallah Juma
Habari zilizopatikana jana kutoka ndani ya timu hiyo zilidai kuwa, Liewig alimuondoa Sunzu katika mazoezi yao ya asubuhi na kumzuia asijifue na wenzake kwa sababu hayuko katika programu yake.
Chanzo kilidai kuwa awali, Liewig alimfokea Sunzu mbele ya wachezaji wengine katika mazoezi yao yaliyofanyika Ijumaa kutokana na kitendo chake cha kushika mpira na Mzambia huyo hakufurahishwa na hatua hiyo; akiamini kwamba kocha amemdhalilisha kwani alipaswa afanye hivyo kwa kumwita pembeni na kumueleza kosa lake kama ambavyo hufanyika mara kwa mara.
Sunzu na Juma hawakupatikana jana kuzungumzia taarifa za kutimuliwa mazoezini jana asubuhi na kutakiwa wajieleze kwa maandishi.
Hata hivyo, akizungumza na NIAPSHE jana, kocha msaidizi wa timu hiyo, Jamhuri Kihwelu 'Julio', alikiri kuwa ni kweli wachezaji hao waliondolewa katika mazoezi yao ya jana asubuhi na kilichowaponza ni kutojulikana walipokuwa kuanzia Ijumaa kabla ya mechi yao ya ligi waliyoshinda 2-1 dhidi ya Coastal Union kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Julio alisema kuwa wachezaji hao (Sunzu na Juma) ndiyo ambao taarifa zao hazikuwa zikifahamika lakini wengine ambao hawakuonekana pia jana, uongozi unafahamu sababu za kutofika kwao, baadhi wakiwa ni majeruhi Mwinyi Kazimoto, Haruna Moshi 'Boban', Amir Maftah na Ramadhan Chombo 'Redondo'. Juma Nyosso anayetumikia adhabu ya kadi nyekundu na hivyo kukosa mechi yao ya Machi 27 dhidi ya Kagera Sugar mjini Bukoba, pia hakuwapo katika mazoezi yao ya jana.
Julio alisema kwamba Simba inaendelea vyema na mazoezi kwa kutumia wachezaji wake wengi wa Simba B ambao waliwapatia ushindi katika mechi dhidi ya Coastal.
Aliongeza kwamba uongozi uko katika maandalizi ya safari ya kuelekea mikoa ya kanda ya kati na ikikamilika wataondoka jijini Dar es Salaam keshokutwa na wataanzia mkoani Dodoma watakapocheza mechi ya kirafiki.
Simba ambao ni mabingwa watetezi wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara, wanashika nafasi ya tatu katika ligi hiyo wakiwa na pointi 34 huku mahasimu wao wa jadi, Yanga wakiongoza kwa kuwa na pointi 45, nane zaidi ya Azam wanaokamata nafasi ya pili.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment