ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, March 20, 2013

TANEXA YALALAMIKIA WINGI WA BERIA MPAKANI MWA TANZANIA NA UGANDA

Mkurugenzi wa Programu na Miradi toka Shirikisho la Wasafirishaji Bidhaa Nje ya nchini (TANEXA), Nyandallo Mboyi akiwa katika semina hiyo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirikisho la Wasafirishaji Bidhaa Nje ya nchini (TANEXA), Mtemi Naluyaga (kulia) akiwa kwenye semina ya wadau wa biashara Bukoba.
Moja ya beria zilizopo eneo la Kyaka
Moja ya gari la mizigo likifanyiwa ukaguzi wa nyaraka kwenye beria kabla ya kuingia Tanzania

SHIRIKISHO la Wasafirishaji Bidhaa nje ya nchi (TANEXA) wamelalamikia kukithiri kwa vituo vya ukaguzi wa magari (beria) na mizigo vilivyopo barabarani, unapoingia na kutoka Tanzania kupitia mpaka wa Tanzania na Uganda (Mtukula). Eneo lilalolalamikiwa zaidi ni kutokea Mtukula hadi Bukoba mjini ambapo kuna wingi wa vituo njiani.
Akizungumza katika semina ya wadau wa biashara juzi mjini Bukoba, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirikisho la Wasafirishaji Bidhaa Nje ya nchini (TANEXA), Mtemi Naluyaga alisema wingi wa beria umekuwa kikwazo cha wafanyabiashara huku baadhi ya wafanyakazi wasio waaminifu wanaohudumia katika vituo hivyo wakijenga mazingira ya rushwa kwa wanachama wao.
Akifafanua zaidi alisema baadhi ya wafanyakazi wa Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) wanaohudumu katika vituo hivyo nao wamekuwa wakivitumia vituo hivyo vibaya kwa kutoza faini za juu pale wasafirishaji wa bidhaa na abiria wanapobainika kuwa na makosa, jambo ambalo humlazimu mtozwa faini kutafuta mbadala wa kukwepa faini hivyo kujengeka mazingira ya rushwa kirahisi.
Aliishauri Serikali kuifanya Mtukula kuwa kituo Kikuu cha Ukaguzi wa Bidhaa zinapoingia na kutoka nchini na kukifuta kile cha Kyaka ambacho kwa sasa kinafanya kazi moja na inayofanywa na kile cha Mtukula mpakani, jambo ambalo alisema ni usumbufu kwa wafanyabiashara wanaotumia mpaka huo.
"Kutokea Mtukula hadi Bukoba Mjini kuna beria 9 upande wa Tanzania, lakini ukiingia Uganda hadi mjini kuna beria moja...na kibaya zaidi ukiangalia beria hizi nyingine zinafanya kazi sawa na beria zingine huu ni usumbufu kwa wafanyabiashara. Alishauri Serikali kupitia mamlaka husika kujipanga na kuweka beria moja eneo la Mtukula na kuimarisha uteandaji ili kituo hicho kifanye kazi ya beria zote.
Kwaupande wake Mwenyekiti wa Wafanyabiashara Wanawake Mpakani mwa Tanzania na Uganda (IWCBTA), Mtukula, Jane Charles alisema akinamama wamekuwa wakinyanyaswa na kutishiwa na baadhi ya watendaji katika beria hizo jambo ambalo limekuwa vikwazo katika ufanyaji biashara zao.
Akizungumza katika semina hiyo, Mjumbe wa Chama cha Wamiliki wa Mabasi ya mikoani (TABOA), Wilaya ya Bukoba, Eliud Rumanyika alipinga kitendo cha wafanyakazi wa TRA kuyashikilia baadhi ya magari ya wanachama wao kwa makosa ya abiria pindi inapotokea abiria kaingia na mzigo ambao umekuwa na tatizo mpakani. "...Sisi tunaona si haki kwa baadhi ya watendaji wa TRA kwenye vituo vya ukaguzi kuamua kuyashikilia magari yetu kwa kosa la abiria, abiria anapokutwa na kosa mpakani atozwe faini mwenyewe na si kushikilia gari la abiria hii ni usumbufu kwa wengine na wamiliki," alisema Mjumbe Rumanyika.
Akijibu baadhi ya hoja katika semina hiyo, Katibu Tawala wa Mkoa wa Kagera, Nassoro Mnambila alisema Serikali ya Mkoa wa Kagera haiungi mkono hoja ya baadhi ya wafanyabiashara wanaotaka kuhamishwa kwa beria ya Kyaka kwenda Mtukula kwani uamuzi wa awali ulizingatia masuala mengi ya muhimu katika nyanja anuai.
"Serikali ya Mkoa wa Kagera haishauri kabisha kuvunjwa kwa kituo cha Kyaka...sisi tunaona ipo haja ya kuangalia namna ya kufanya marekebisho kimaboresho zaidi. Watu wachache wasituharibie maana ya kuweka kituo kile (Kyaka) eneo lile," alisema Mnambila.

Chanzo: www.thehabari.com

No comments: