Baadhi ya wanachama wa Simba wakinyoosha mikono kukubali hoja wakati wa mkutano wao mkuu wa dharura uliofanyika kwenye ukumbi wa Starlight jijini Dar es Salaam jana
Mambo yamezidi kuwa shaghalabaghala ndani ya klabu ya Simba baada ya baadhi ya wanachama kujaribu kumpindua mwenyekiti wao Ismail Aden Rage na kuunda uongozi wa muda chini ya mjumbe aliyejiuzulu wa kamati ya utendaji ya klabu hiyo, Zakaria Hanspope na mwanachama wao tajiriri, mfanyabiashara Rahma Al Kharoos 'Malkia wa Nyuki'.
Hata hivyo, jaribio hilo la mapinduzi yaliyohusisha pia kutimuliwa kwa wajumbe wote wa kamati ya utendaji ya klabu hiyo kufuatia mkutano mkuu wa dharura uliofanyika na kwenye ukumbi wa Starlight jijini Dar es Salaam linaelekea kupata upinzani mkali baada ya Hanspoppe kukataa nafasi aliyopewa huku Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Angetile Osiah akisema kuwa hawawezi kuutambua uongozi wwowote wa kamati za muda.
Mapinduzi hayo dhidi ya uongozi wa Rage yalifikiwa katika mkutano ulioitwa "Mkuu wa Dharura" wa wanachama wa klabu hiyo, kwa kutumia ibara ya 22 ya katiba ya Simba.
Katika mkutano huo ulioanza saa 6:00 mchana na kumazikika saa 7:34 mchana ukiongozwa na mwenyekiti wa muda, Mohamed Wandi, wanachama 607 walikubaliana kuuondoa madarakani uongozi wa Rage.
Hata hivyo, Rage hakuwapo kwenye mkutano huo kwani yuko safarini nchini India alikokwenda kwa ajili ya matibabu. Ndnai ya mkutano huo wa jana hakuwapo pia mjumbe yeyote wa kamati ya utendaji ya Rage aliyepewa nafasi ya kujibu chochote kuhusiana na shutuma dhidi ya uongozi wao.
Wanachama hao waliokutana jana, wakirejea ibara ya 16(g) ya katiba ya Simba, waliwateua Malkia wa Nyuki na Hans Poppe kuwa wajumbe wa chombo maalum kitakachoisimamia timu yao katika mechi saba za Ligi Kuu ya Tanzania Bara zilizobaki na kwamba, pia wawili hao watakuwa na jukumu la kuteua wajumbe wengine wa kuwasaidia na kuitisha uchaguzi mkuu baada ya ligi kumalizika.
Aidha, wanachama hao waliokuwa wakiuponda uongozi wa Rage, walikubaliana kuibakisha madarakani sekretarieti ya klabu hiyo inayowahusisha wajumbe wa kuajiriwa .
“Ibara ya 17(1) ya katiba ya Simba inatoa madaraka kwa mkutano mkuu kuunda chombo maalum cha kuisimamia timu. Mkutano huu unawateua Hans Poppe na Malkia wa Nyuki (ambao pia hawakuwapo kwenye mkutano huo) kuiongoza Simba hadi mwisho wa msimu huu wa ligi kuu, baadaye wataitisha uchaguzi,” alisema Wandi wakati wakipitisha maamuzi yao jana.
Mwenyekiti huyo ambaye katika meza kuu alikuwa amefuatana na katibu wake Maulid Said na mjumbe, Bi. Chuma Selema, alisema uongozi wa Rage umekiuka katiba ya klabu hiyo, ibara ya 16(l) “kwa kutoitisha vikao kila baada ya miezi minne,” ibara ya 18(6) “kwa kutounda baraza la wazee la Simba” na ibara ya 28(c) “kwa kutokuwa na mjumbe mwanamke katika kamati ya utendaji aliyechaguliwa na mkutano mkuu”.
“Uongozi huu umekuwa ukitoa ahadi hewa kwa wanachama. Sasa tumechoka kudanganywa. Tunawaomba TFF na msajili waheshimu mawazo ya wanachama,” alisema Wandi.
Wandi aliendelea kueleza kuwa endapo Rage na wenzake wataamua kwenda mahakamani, watawafutia uanachama wa klabu hiyo kwa mujibu wa ibara ya 19(3) inayosema “mkutano mkuu wa Simba ndiyo wenye mamlaka ya kumpa ama kumfuta mtu uanachama.”
Mkutano wa jana ambao ulikuwa umehudhuriwa na wanachama waliodai kutoka mikoa ya Tabora, Morogoro, Lindi na Dar es Salaam ukiwa na agenda kuu mbili za kutathimini mwenendo wa timu ya Simba katika michuano inayoshiriki na kutokuwa na imani na uongozi, ulifanyika chini ya ulinzi mkali wa Jeshi la Polisi.
Katibu wa mkutano huo, Maulid Said, aliliambia gazeti hili baada ya kumalizika kwa mkutano kuwa atawasilisha barua za maamuzi yote yaliyofikiwa na wanachama katika msajili na TFF leo.
Juzi, uongozi wa Simba kupitia kwa Afisa Habari, Ezekiel Kamwaga ulikaririwa ukisema kuwa uliwasilisha barua katika Kituo cha Polisi Msimbazi ukiomba mkutano huo usifanyike kwa sababu ni batili.
HANSPOPPE AWAKANA
Alipotafutwa na NIPASHE kuzungumzia uteuzi wake jana, Hans Poppe, ambaye pia alikuwa mwenyekiti wa kamati ya usajili ya Simba kabla ya kujiuzulu kutokana na matokeo mabaya iliyoyapata timu yao katika ligi kuu na michuano ya Klabu Bingwa Afrika dhidi ya timu ya Recreativo de Libolo ya Angola, alisema kuwa kwa sasa hawezi kukubali kupewa madaraka ndani ya Simba kutokana na klabu hiyo kuonekana ikikabiliwa na rundo la migogoro.
“Siwezi kukubali uteuzi huo kwa sababu Simba inakabiliwa na migogoro. Ndiyo maana nikaamua kujiondoa mapema. Sijahusishwa katika uteuzi huo na hadi sasa sijui kama ule mkutano ni hahali kikatiba ama la,” alisema Hans Poppe.
Katiba ya Simba inatamka wazi kuwa mwenyekiti wa klabu hiyo akishirikiana na kamati ya utendaji ndiye mwenye mamlaka ya kuitisha mkutano mkuu na mkutano mkuu wa dharura.
Ibara ya 22 ambayo inatajwa na wanachama walioitisha mkutano wa jana, inatamka kuwa wanachama wa Simba wasiopungua 500 wanaweza kuitisha mkutano mkuu ama mkutano mkuu wa dharura kama mwenyekiti na kamati ya utendaji haitakuwa tayari kuutisha ndani ya siku 30 baada ya kuombwa na wanachama hao.
TFF WANENA
Akizungumza na NIPASHE baada ya kutolewa kwa maamuzi ya kuupindua uongozi wa Rage, Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah alisema kuwa katiba ya shirikisho hilo haitambui uongozi wa muda, hivyo kuteuliwa kwa Malikia wa Nyuki na Hans Poppe ni kama kujifurahisha wanachama waliokutana jana kwani uongozi wowote wa muda hautakuwa na fursa ya kufanya kazi na TFF.
"Katiba ya TFF na taratibu zilizopo za uendeshaji wa soka haziruhusu kabisa kamati za muda... naomba niishie hapo," alisema Osiah.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment