.jpg)
Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo,Amos Makalla
Kikao hicho ni maalumu kwa ajili ya kufikia mwafaka kuhusiana na sakata la katiba ya TFF ambayo imetenguliwa na serikali kwa madai kuwa haikufuata taratibu wakati wa kuisajili.Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah, alisema kwamba wanaomba kukutana na Waziri Mukangara kesho Alhamisi na endapo itashikanda kikao hicho kifanyike baada ya Machi 15 mwaka huu.
Osiah alisema kwamba wameamua kumkataa Makalla katika kikao hicho kutokana na Naibu Waziri huyo kuonyesha kwamba yuko katika upande mmoja wa mgogoro huo hivyo wana wasiwasi kuwa haki haitatendeka.
Alisema kuwa tatizo lililopo sasa linamgusa kila mdau wa soka nchini na ni lazima ieleweke kwamba kila mmoja ana wajibu wa kuhakikisha mpira wa miguu unaendelea.
"Tumeomba kikao ili waziri asikie upande wetu, ajue ukweli, ajue madhara yake na kitakachotokea baada ya hapo," alisema Osiah.
Alieleza kwamba lengo la TFF ni kutaka kuona haki inatendekea baada ya naibu waziri kuonekana kuwa ni sehemu ya mgogoro.
Alisema kuwa TFF ni ya wapenzi wote wa soka na nia iliyopo ni ya kumuelekeza waziri mustakabali wa mgogoro huo ambao umesababisha kusimamishwa kwa mchakato wa uchaguzi wa shirikisho hilo.
Hata hivyo, Makalla aliiambia NIPASHE jana kwamba yeye ndiye mshauri wa Waziri Mukangara katika eneo la michezo na kauli ya TFF kumkataa asishiriki kwenye kikao hicho ni sawa na kutapatapa.
Alisema kuwa anashangaa kuona TFF inataka kumtenga katika suala hilo na haamini kama hiyo ni kauli ya shirikisho au ni ya Osiah binafsi.
"Wakija hiyo Alhamisi watanikuta, mimi ndiye ninayekaimu nafasi kwavile Waziri yuko nje ya nchi kwa siku kumi, ninavyoona mimi ni kwamba Osiah hana hoja, mimi naifuata kauli ya Tenga ya Machi 2 kwamba wanataka kukutana na waziri na naibu ambaye ni mimi... (Osiah atambue kwamba) huwezi kuchagua nesi siku ya kujifungua," alimaliza Makalla.
Sakata la katiba mpya ya TFF ya mwaka jana iliyobadilishwa kwa njia ya waraka ilichukua sura mpya Februari 25 baada ya serikali kutangaza kutoitambua na kulielekeza shirikisho hilo kufanya uchaguzi wake kwa kutumia katiba ya mwaka 2006.
Lakini TFF imeonya kuhusu Serikali kuingilia masuala ya michezo kwa sababu adhabu yake ni kufungiwa na Shirikisho la Soka Duniani (FIFA).
Ujumbe kutoka FIFA unatarajiwa kutua nchini katikati ya mwezi huu kwa ajili ya kushughulikia mgogoro huo.
CHANZO: NIPASHE
1 comment:
naibu waziri aweke mbele maslahi ya soka la tanzania kuliko ya kwake binafsi.hili ni suala la kisheria,tff wanataka kuonana na waziri,sheria ya BMT inamtambua waziri tu na sio kaimu waziri au naibu waziri.kwanini ang'ang'anie kushiriki kikao hicho na watu wasiokuwa na imani naye?kwa utaratibu wa serikali mshauri mkuu wa waziri ni katibu mkuu wa wizara siyo naibu waziri kwani naibu anapangiwa kazi na waziri,ni msaidizi wa waziri
Post a Comment