ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, March 2, 2013

THAMINISHA...... DJ LUKE JOE

Dj Luke Joe alipokuwa akizungumza siku ya uzinduzi wa blog ya Vijimambo. 

Na Mubelwa Bandio
Maisha ni mchakamchaka. Na kwa nchi za ugenini, yaonekana kuwa mchakamchaka zaidi. Ni ugenini huku ambako wengine hawapati muda wa kuwasiliana, kutembeleana, kupigiana simu na hata kufanya ibada, kwa kuwa WAMEBANWA NA KAZI NA MAISHA.
Labda kuna kweli ndani ya hili, na pengine yawezekana ni fikra zetu zinazotufanya tuamini hilo. Lakini kama wengi wanavyosema, KILE UWAZACHO KINAWEZA KUKUTABIRIA MAISHA YAKO YAJAYO. Kwa maana nyingine, kujipanga na kuamua kutekeleza kitu, unaweza kuona mafanikio ambayo hukuyaona awali. Kama nilivyosema HAPA, MAISHA NI TASWIRA.
Leo katika kipengele hiki cha THAMINISHA, nimeona ni vema kutambua mchango wa DJ Luke Joe wa Blog ya Vijimambo. Nakumbuka katika hotuba hii ya Mhe Balozi Maajar siku yauzinduzi wa blogu ya Vijimambo alihusia matumizi ya mtandao kwa manufaa ya wanajamii walio ndani na nje ya Washington DC. Hii ilikuwa moja ya CHANGAMOTO ambazo alitoa kwa Dj Luke Joe na wote wenye blogu.

Punde baada ya uzinduzi huo, nilipokuwa katika maongezi ya kawaida na Dj Luke, alisema kuwa anahisi anaanza kupunguza jitihada zake kwenye kupiga muziki na kuwekeza zaidi katika blogu. Na sasa mwaka mmoja baadae, naamini ni wengi wanaoishi maeneo ya Washington DC na vitongoji vyake wanaweza kuamini kuwa Vijimambo imekuwa kama chanzo cha habari na matukio mengi yanayotukia ama kutarajia kutukia eneo hili. Ni kiunganishi chema na MUHAMASISHAJI mwema kwa jamii ya hapa.
Nimesema MUHAMASISHAJI (tena kwa herufi kubwa) kwa kuwa sote tuishio vitongoji vya DC tunatambua namna ambavyo chombo ambacho kilikuwa kikihusika na kutukusanya na kutuhamasisha na hata kutuhabarisha kuhusu Tanzania, uTanzania na waTanzania hapa DC kilivyo kwenye mgogoro. Na kwa kukosekana kwake, hakika ilikuwa kama kundi zima limetawanywa bila mchungaji. Na siku za karibuni, jamii yetu imepatwa na misiba mitatu iliyofuatana, na kutokana na wengi kutokuwa na ratiba inayoruhusu kuwa mahala pa msibani ama mawasiliano ya msibani, blogu ya Vijimambo ilikuwa zaidi ya "makutano" kwetu. Ni hapa tulipojua kilichotokea, kilichokuwa kikiendelea na kwa wale ambao kwa namna moja ama nyingine hawakuweza kuhudhuria, waliweza kushiriki kupitia blogu hii. Tumekuwa tukipata habari (toka msibani ambako Dj Luke amekuwa akishiriki), picha na hata video za matukio mbalimbali.
Narejea katika aya yangu ya kwanza, kwamba MAISHA YA HAPA NI MCHAKAMCHAKA, NA NI KWA UGUMU HUO, KUNA HAJA YA KUTHAMINI MUDA WA DJ LUKE ambaye licha ya kuwa na kazi kama tulivyo wengine wengi, bado anaweza kutenga muda wa ziada kufanya haya yote.
Hii imekuwa CHACHU kwangu, na naamini kwa wengine wengi.
Na ndio maana katika kipengele hiki cha THAMINISHA, tumeona tutoe (japo) TUZO HII YA KAULI kwa Dj Luke, ambaye aliyoyafanya (hasa katika kipindi hiki cha misiba) ilikuwa zaidi ya wajibu wa pamoja wa Ubalozi na Jumuiya yetu. Alikuwa kwenye misiba yote, katika matukio yote muhimu na kutuhabarisha maendeleo yote ya vifo, michango, ibada na hata maziko.
HILI SI LA KUPITA BILA KUTHAMINIWA (labda kama hujui ugumu wa aliyoyafanya).
Kwa Kaka Luke, NATHAMINI SANA MCHANGO WAKO. Najua ugumu wa ratiba za maisha ya hapa, najua ugumu wa ku-blog, na najua ugumu na gharama za kusafiri katika kona zote ulizofanya na kushiriki katika matukio yote uliyoshiriki ili kutujuza yote yanayotokea. Ni kwa kutambua ugumu huo, napenda kusema ASANTE.
Na ndio maana naona ni vema kuweka thamani yako nikianimi kuwa WASOMAO HAPA, NAO WATATHAMINISHA UWAFANYIALO
Wimbo huu hapa chini ni maalum kwa ajili ya yale mema ututendeayo. Kwangu mimi, YOU ARE A HERO.
 


HAPPY BIRTHDAY DJ LUKE JOE

1 comment:

baraka daudi said...

Kaka Mubelwa nakubaliana na wewe 110%,kwa kweli Dj Luke anafanya kazi nzuri sana kwa wenzetu Waingereza wanasema"what he has done,he went beyond extra miles". Ni vizuri jamii yetu ya Ughaibuni ikatambua mchango wa blogu ya Vijimambo,na ndio maana naungana na wewe kaka Mubelwa kwa kusisitiza kwamba ni vizuri kumuunga mkono kwa kushirikiana na Dj Luke katika sherehe ya miaka mitatu ya vijimambo na tamasha la utamaduni wa kiswahili Marekani julai 6,2013.Kaka Luka kazi nzuri sana na Mungu akubariki uendelee na hii kazi uliyoianzisha.