ANGALIA LIVE NEWS

Monday, March 4, 2013

Utata wa kifo kigogo UVCCM Arusha


Benson Mollel (kwanza kulia) akiwa katika moja ya shughuli za UVCCM mkoani Arusha. Picha kwa hisani ya Issa Michuzi

MJUMBE wa Baraza Kuu la Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) taifa, kupitia Mkoa wa Arusha, Benson Mollel (26) amekutwa amefariki dunia ndani ya Hoteli ya Lush Garden Business, iliyopo Mtaa wa Jacaranda katikati ya Jiji la Arusha.

Mashuhuda wa tukio hilo walisema Mollel alikutwa akiwa amekufa jana mchana na kwamba tukio hilo limezua hofu kwa wakazi wa Jiji la Arusha, huku wakijiuliza chanzo cha kifo chake.Kifo cha mwanasiasa huyo mchanga ambaye pia alikuwa ni mfanyabiashara wa madini mkoani hapa, kimezusha maswali mengi wakati wengine wakihusisha tukio hilo na masuala ya kisiasa na upande mwingine wakidai ni masuala la kibiashara.

Hisia hizo zinatokana na ukweli kwamba Arusha ni jiji lenye hekaheka za kisiasa hasa ndani ya CCM ambapo Mollel alikuwa mmoja wa vinara wake.

Polisi waliwasili hotelini hapo saa 8.00 mchana na kuupakia mwili wa marehemu kwenye gari na kisha kuupeleka Hospitali ya Mount Meru kwa ajili ya kuhifadhiwa.

Mkuu wa Polisi wa Wilaya wa Arusha (OCD), Gilles Muruta akizungumza katika eneo la tukio alisema: “Tunachunguza tukio hili ambalo ni la ghafla.”

Akizungumzia kifo hicho, Katibu Mkuu wa UVCCM, Martin Shigela alisema: "Tumepokea kwa masikitiko kifo cha Mollel japokuwa sifahamu nini hasa kimejiri huko."

"Kuna rafiki yake alinipigia simu kuniarifu kuhusu kifo hicho na nikawaambia kama UVCCM Taifa tupate maelezo kamili na tujue nini cha kufanya. Iwapo familia itakuwa na mipango yoyote watutaarifu," alisema Shigela.

Baadhi ya wanasiasa na wafanyabiashara wa madini mkoani Arusha walionekana nje ya hoteli hiyo baada ya taarifa za kifo hicho kusambaa na wengine walishindwa kujizuia kisha kuangua vilio.

Miongoni mwao ni kada wa Chadema, James ole Millya na diwani wa CCM Kata ya Mlangarini, Mathias Manga. Katibu Mwenezi wa CCM wa Mkoa wa Arusha, Isaack Kadogoo ambaye pia alifika eneo hilo alisema kwamba wamepokea taarifa za tukio hilo kwa mshtuko mkubwa.

Uongozi wa hoteli hiyo haukuwa tayari kulizungumzia kwa madai kwamba limefikishwa katika vyombo vya usalama.

Hata hivyo, kwa mujibu wa vyanzo vya habari ndani ya hoteli hiyo vilidai marehemu aliwasili usiku, juzi Jumamosi hotelini hapo akiongozana na mwanamke aliyetambulika kwa jina la Nancy na kuchukua chumba namba 208.

No comments: