ANGALIA LIVE NEWS

Sunday, March 3, 2013

Wakulima na wafugaji wazichapa Pangani

Mapigano makubwa yameibuka katika vijiji vitatu wilayani Pangani baina ya wakulima na wafugaji wa kabila la Wamang'ati kutoka mkoani Manyara na kusababisha baadhi ya wakulima kujeruhiwa na wengine kulazwa hospitalini.

Mgogoro huo umetokana na madai kuwa wafugaji walivamia mashamba ya wakulima katika vijiji vya Masaraza, Mivumo na Kigurusimba Kata ya Bushiri huku wakiwa na mishale kufuatia hali ya ukame inayoukabili mkoa wa Tanga na mingine ya jirani.

Wakizungumza katika kikao kilichoitishwa na Mkuu wa mkoa wa Tanga, Chiku Gallawa, baadhi ya wakulima wamewashutumu baadhi ya viongozi wa serikali ngazi ya wilaya kwa kuwakaribisha wafugaji hao kwa makubaliano yao binafsi bila kuwashirikisha wananchi katika utoaji wa maamuzi.

Walisema kutokana hali hiyo, wafugaji wamekuwa wakijichukulia sheria mikononi na bila kujali wamekuwa wakivamia maeneo yao na kulisha mifugo hivyo kuharibu mazao mashambani.

“Wao ni wavamizi lakini wanajiona ndio wamiliki halali wanaingiza mifugo yao kila mahali na hakuna wa kuwahoji kimsingi hali hii imetuchosha sana," alisema Saimon Luoga mkulima wa Kijiji cha Kigurusimba.

Wafugaji hao huharibu pia vyanzo vya maji hivyo wakazi wa vijiji hivyo wanaiomba serikali kuingilia kati mgogoro kwani ipo hatari ya kukosa kabisa maji kwa matumizi ya binadamu.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Pangani, Neneka Rashid alisema kuwa wameunda tume ya kuchunguza tatizo hilo lakini bado wafugaji wamekuwa wakikaidi agizo la mkuu wa wilaya la kuwataka waondoke katika vyanzo vya maji.

Kufuatia hatua hiyo Mkuu wa mkoa wa Tanga Chiku Gallawa, amewaagiza wafugaji wote walioingia kinyume cha utaratibu kuondoka mara moja kabla serikali haijatumia nguvu kuwaondoa.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

No comments: