ANGALIA LIVE NEWS

Friday, March 1, 2013

Walimu wengine 978 waajiriwa

Na Thobias Mwanakatwe
Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi imeamua kuwaajiri walimu wengine 978 waliokosa nafasi ya kuajiliwa katika ajira mpya zilizotangazwa mwaka huu kutokana na makosa yaliyofanywa na maofisa wa wizara hiyo kwa kuingiza majina ya walimu walioajiriwa tangu mwaka jana.

Naibu waziri wa wizara hiyo, Philipo Mulugo, alisema hayo jana wakati akizungumza na NIPASHE kuhusu hatua zilizochukuliwa na wizara kufuatia idadi kubwa ya walimu kukosa nafasi ya kuajiriwa na kusababisha malalamiko.

Mulugo alisema wizara yake imechukua hatua ya kuondoa majina ya walimu walioajiriwa mara ya pili katika orodha ya majina ya walimu walioajiriwa mwaka huu na kuingiza walimu 978 waliokosa nafasi hiyo kutokana na makosa hayo.“Walimu walioajiriwa mara ya pili waliokuwa masomoni ambao walikuwa wameajiriwa mwaka jana wametolewa kwenye ajira mpya na sasa wanatakiwa kurudi kwenye vituo vyao vya awali vya kazi walivyoajiriwa tangu mwaka jana,” alisema Mulugo.

Hivi karibuni, walimu waliokosa ajira katika ajira mpya 26,000 zilizotangazwa mwaka huu waliandamana kwenda ofisi za Wizara hiyo wakilalamika kukosa ajira.

No comments: