ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, March 16, 2013

Waliobakwa sasa wajielezea kiundani


Marekani,Washington. Waathirika  wa vitendo vya unyanyasaji wa ngono waliobakwa na kunajisiwa walipokuwa wakihudumu katika jeshi la Marekani walitoa wito wa kufanyika mabadiliko ya kimsingi katika mahakama za kijeshi za nchi hiyo.
Askari watatu wa kike na mwanaume mmoja jana walihudhuria katika Baraza la Seneti la nchi hiyo wakieleza jinsi walivyonyanyaswa na kunajisiwa jeshini na masikitiko yao kwamba wahalifu waliofanya ukatili huo bado hawajachukuliwa hatua yoyote.
Sajenti wa zamani katika jeshi la Marekani Rebekah Havrilla aliliambia Baraza la Seneti kwamba mfumo wa mahakama zinazoshughulikia jinai za kijeshi wa Marekani zimesambaratika.
Havrilla alieleza jinsi alivyobakwa na kunajisiwa na askari mwenzake alipokuwa katika huduma za jeshi nchini Afghanistan na baadaye askari huyo akasambaza picha za kitendo chake kiovu katika mtandao wa intaneti.
Alisema licha ya kuripoti ukatili huo kwa maofisa wa jeshi la Marekani lakini mtuhumiwa hakuchukuliwa hatua yoyote.
Askari huyo wa zamani wa Marekani alisema alipomwambia kasisi wa jeshi la Marekani maafa aliyotendewa aliambiwa kuwa “ubakaji huo umefanyika kwa mapenzi ya Mungu” ambaye anataka kumrejesha kanisani.
Askari hao walionajisiwa walitoa wito wa kufanyika marekebisho makubwa katika sheria za mahakama za kijeshi.
Ripoti zilisema kuwa askari wa Marekani ambao wanakuwa katika jitihada za kubakia hai katika medani za vita kama Afghanistan huishi na wasiwasi mkubwa wa kubakwa na kunajisiwa na wakubwa wao au askari wenzao.
Mwananchi

No comments: