Papa Francis I aliteuliwa hivi karibuni kuliongoza kanisa hilo baada ya Papa Benedict XVI kutangaza kujiuzulu kwa sababu za kiafya.
Enzi ya ujana wake aliwahi kufanya kazi mbalimbali ikiwamo ya mlinzi wa mlangoni (baunsa) katika Bar, ili kujipatia fedha.
Papa Francis aliteuliwa hivi karibuni kuliongoza kanisa hilo baada ya Papa Benedict XVI kutangaza kujiuzulu kwa sababu za kiafya.
Aidha, Papa Francis anatarajia kuongoza misa yake ya kwanza kesho katika Kanisa la Mtakatifu Peter, mjini Vatican.
Katika wasifu wake ulioandikwa mwaka 2010 na Francesca Ambrogetti na Sergio Rubin wa Shirika la Jesuit, Papa Francis I alikiri kuwa aliwahi kufanya kazi kama mlinzi wa mlangoni katika moja ya baa za Jimbo la Buenos, Argentina, ili kujipatia ada ya shule.
Papa huyu mpya ambaye jina lake halisi ni Jorge Mario Bergoglio, alisema kuwa rafiki yake wa kike alikuwa ni miongoni mwa kundi la marafiki aliokuwa akicheza nao muziki wa tango.
“Lakini baada ya kubaini kuwa natakiwa kuenenda kiroho, nilisitisha urafiki,” alisema alipohojiwa.
Papa Francis I amezaliwa katika familia yenye maisha ya kawaida, ambapo baba yake alikuwa mfanyakazi wa shirika la reli na mama yake alikuwa mama wa nyumbani.
Vilevile kuna taarifa zinaeleza kuwa Papa Francis, aliwahi kumpenda msichana mmoja na kutaka kuoa kabla ya kuingia katika utumishi wa Mungu.
Mwanamke huyo Amalia Damonte alisema kuwa aliwahi kutaka kuolewa na Papa, lakini alikataa.
“Nampa hongera Papa Francis, lakini nilikataa ombi lake la kutaka kunioa,” alisema Damonte.
Alisema Bergoglio alionyesha nia ya kumwoa akiwa na miaka 12 na alikataa kwa sababu wazazi wake wasingekubali akiwa katika umri huo.
“Nadhani nilichangia yeye kuwa Padri kwa kukataa ombi lake la kutaka kunioa,” alisema Damonte.
Damonte ambaye ana miaka 77 sasa, alisema kuwa Papa Francis I alimweleza nia ya kutaka kumwoa kwa njia ya barua kati ya mwaka 1948 au 1949.
Anategemea pafu moja
Mara tu baada ya kuteuliwa, wachambuzi wa masuala yanayojiri Vatican walisema kuwa pengine Papa huyo hataweza kushika nafasi hiyo kwa kipindi kirefu kwa sababu ya kuondolewa pafu moja alipokuwa kijana.
Robert Mickens, mchambuzi wa matukio wa gazeti la kikatoliki la kila wiki, alisema akihoji:
“Iwapo Benedict XVI alijiuzulu kwa sababu za kiafya, tutegemee nguvu gani kwa huyu mwenye miaka 76 na anayetegema pafu moja?”
Kwa nini alichagua jina Francis
Bregoglio alichagua jina la Francis akimwadhimisha Mtakatifu Francis wa Assisi, ambaye licha ya kuwa tajiri, aliishi mitaani katika vibanda pamoja na watu wenye ukoma na maskini.
Msemaji wa Vatican, Thomas Rosica alisema Papa Francis anajulikana kwa ukaribu wake na watu wenye Virusi vya Ukimwi, wasiojiweza kifedha na wanawake waliotelekezwa na waume zao na kuachiwa watoto.
Hata hivyo, Rosica alisema kuwa Papa Francis hataitwa Francis, bali Francis hadi atakapotokea mtu mwenye jina hilo baadaye.
Fundi wake apatikana
Mara baada ya Papa Francis kuteuliwa, fundi cherehani kutoka Columbia alipewa taarifa ya kuwa fundi maalumu wa kushona mavazi ya Papa huyo.
Luis Delgado, mkazi wa Cali, nchini Columbia alichaguliwa kabla hata ya Papa mpya kupatikana ili kutengeza vazi atakalolivaa Papa huyo baada ya kuchaguliwa.
Delgado alipata vitambaa vya vazi jipya la Papa kutoka Roma na alitengeneza nguo zenye saizi tatu tofauti, ndogo, ya kati na kubwa.
Delgado pia aliwahi kushona nguo za Papa John Paul II na miaka mitano iliyopita alishona nguo za Papa Benedict XVI.
Ni mnyenyekevu
Kiongozi wa Kanisa nchini Argentina, Eduardo Mangiarotti alikiri na kusema kuwa Papa Francis ni zaidi ya mnyenyekevu.
“Anapanda mabasi ya abiria kila siku,” alisema Mangiarotti.
Alisema Papa Francis alichagua kuishi katika nyumba ndogo, badala ya kuishi katika nyumba za kifahari za makadinali.
“Alijipikia mlo wake mwenyewe, alipenda kulipa bili zake, badala ya kusubiri kanisa limlipie,” alisema mchambuzi wa Vatican, CNN, John Allen.
Papa Francis I anakabiliwa na kazi nzito ya kuliongoza kanisa lenye waumini zaidi ya bilioni moja duniani likiwa na changamoto mbalimbali.
Mwananchi
No comments:
Post a Comment