KUNDI LA NNE
Kundi hili ambalo nimeliteua kuwa la mwisho, linawahusu wanawake ambao kila mwanaume anaota kuwa nao. Inawezekana nao wakawa wanakutana na misukosuko ya kimapenzi ya hapa na pale, yaani nao wanaumizwa na wanaachwa, hilo lisikushangaze, kwani dunia ni tambara bovu.
Upo msemo mwingine kuwa palipo na miti mingi hakuna wajenzi. Kwamba wakati asilimia kubwa ya wanaume wanaota wangekuwa na wake mithili ya wanawake wanaounda kundi hili, kuna wengine wanawachezea, hawajui thamani yao.
Bado nasisitiza kuwa hutakiwi kushangaa, kwani kuna anayejuta hivi leo baada ya kugundua kuwa alipiga teke almasi wakati alipokuwa ‘bize’ kukusanya mawe. Wanawake wa kundi hili, huwa na faida kubwa pale wanapokutana na wanaume sahihi zaidi katika maisha ya kimapenzi.
Ukipenda unaweza kuwaita ‘wife materials’, kwa maana hawa ni wanawake ambao wanakuwa wameshapevuka kimawazo na mtazamo kuhusu mapenzi na maisha kwa jumla. Hawaangalii sura, mavazi, fedha wala starehe, bali huzingatia yule ambaye anaweza kumfanya ajione yupo salama, vilevile atakayejenga naye maisha.
Zingatio lao ni amani, furaha, upendo, usalama na maisha. Mwanaume anayeshindwa kumpa mwanamke vitu hivi, hujiwekea doa bila mwenyewe kujua. Jambo zuri zaidi kwa wanawake wanaounda kundi hili ni kwamba wao ni walimu, halafu ni wavumilivu wakubwa.
Kwa kawaida ni wagumu kuingia kwenye uhusiano lakini wakishanasa ni ngumu sana kuchomoka. Wakishaingia wameingia, hata wanaume wakiwa majanga, wao huvumilia. Ukiona wameacha, ujue ama wameona pale walipo hakuna sura njema ya kimaisha au wamepata ushawishi wenye matarajio ya faraja.
Wanawake wa kundi hili huhitaji wanaume ambao kipaumbele chao ni maisha. Mara nyingi ni wachapakazi na hupigania kushirikiana na waume zao katika kujaza pato la familia. Ni walezi wazuri wa watoto, inapotokea waume zao kushindwa kuwajibika ipasavyo kwa namna yoyote ile.
Inawezekana mwanaume ametelekeza familia, anasumbuliwa na maradhi yanayomfanya ashindwe kutafuta riziki, amefariki dunia au amekumbwa tu na msukosuko wa kiuchumi, mwanamke wa kundi hili hubaki imara na kuhakikisha familia inaendelea kupata mahitaji muhimu.
Wanawake wa kundi hili, siyo kila mara wanaweza kuwa wafanyakazi au wafanyabiashara. Wengine ni akina mama wa nyumbani lakini uwezo wao ni mkubwa katika kudhibiti matumizi, kupanga maendeleo na kusimamia familia, kuanzia kwa baba mpaka watoto.
Hawa ndiyo huipa nguvu ile tafsiri kwamba nyuma ya kila mwanaume aliyefanikiwa, yupo mwanamke imara, aliyetia msukumo wa hayo mafanikio. Mara nyingi si watu wa kujikweza na kukimbilia mahitaji ya gharama kubwa, huonekana wa kawaida kwa faida ya familia zao.
TATHMINI YAO KIMAPENZI
Kama ilivyoelezwa hapo kabla ni kwamba wao siyo watu wa kutekwa na ‘malavidavi’, isipokuwa kipaumbele chao ni kupata wanaume ambao watawafanya wawe na furaha, amani lakini juu ya yote hayo, hutaka wale watakaoshirikiana kujenga maisha.
Mara nyingi wao siyo watu wa nakshinakshi ili kuyapamba maisha ya kimapenzi, badala yake huyaacha yaende kama yalivyo. Anaweza asihoji zawadi, wala kuuliza ni kwa nini haambiwi anapendwa kama mwanzoni mwa uhusiano. Kwake kitu cha muhimu ni uhusiano kuwa imara.
Ukitaka kumhukumu kwa vigezo fulanifulani, kama vile ni kwa nini hakununulii zawadi, hakumbushii haki yake ya ndoa na mambo mengineyo, utakuwa unakosea. Jiulize kwamba mbona ukihitaji wewe unapata? Sasa jibu unalo kuwa yupo tayari ila haamini katika kuanza.
Itaendelea wiki ijayo.
Global Publishers
No comments:
Post a Comment