Mshambuliaji wa Yanga, Hamis Kiiza (katikati) akipiga tiktak mbele ya beki Salmin Kissy wa Polisi Moro(kulia) na Athuman Idd (kushoto) katika mchezo uliofanyika kwenye Uwanja wa Jamhuri, Morogoro jana. Timu hizo zilitoka suluhu. Picha na Juma Mtanda.
Azam sasa ipo nyuma ya Yanga kwa tofauti ya pointi sita ikiwa imebaki michezo mitano.
Azam imesogelea kileleni baada ya vinara Yanga kulazimishwa suluhu ya 0-0 na Polisi Morogoro, huku mabingwa watetezi Simba wakiporomoka hadi nafasi ya nne baada ya kutoka sare 2-2 na Toto African.
Mshambuliaji wa kimataifa wa Ivory Coast alifunga bao lake la 13 msimu huu wakati Azam ikiichapa Ruvu Shooting bao 1-0 kwenye Uwanja wa Mabatini, Mlandizi.
Kwa matokeo hayo Azam imefikisha pointi 43 ikiwa nyuma ya Yanga yenye pointi 49, huku mabingwa watetezi Simba wakiporomoka hadi nafasi ya nne wakiwa na pointi 35 baada ya Kagera Sugar kuichapa Mtibwa Sugar 3-1 na kufikisha pointi 37 katika mchezo ambao kadi mbili nyekundu zilitolewa kwa wachezaji wa Mtibwa, Shaaban Nditi na Vicent Barnabas.
Nditi alipewa kadi nyekundu baada ya kugomea penalti wakati Barnabas alipewa kadi nyekundu baada ya kumchezea rafu mbaya Themi Felix.
Nditi alipewa kadi nyekundu baada ya kugomea penalti wakati Barnabas alipewa kadi nyekundu baada ya kumchezea rafu mbaya Themi Felix.
Simba walishuka kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza wakiwa na kumbukumbu ya kuchapwa bao 1-0 na Kagera Sugar, lakini jahazi la mabingwa hao lilianza kuyumba baada ya wenyeji Toto kupata bao la kuongoza dakika ya 24 ambalo lilifungwa na Mussa Saidi kwa shuti kali lililomshinda kipa Juma Kaseja.
Dakika moja baadaye, Simba walisawazisha bao hilo mfungaji akiwa Rashid Mkoko aliyeunganisha vizuri mpira uliopigwa na Haruna Chanongo baada ya Simba kufanya shambulizi la kushtukiza na mabeki wa Toto kushindwa kuondoa hatari golini kwao.
Kipindi cha pili, Simba ilionyesha ilikuwa na nia ya kushinda mechi hiyo kwani Mrisho Ngassa aliyeingia akitokea benchi aliipatia Simba bao la pili kwa shuti la umbali wa mita 25 katika dakika 62, lakini uzembe wa mabeki wa Simba ulitoa zawadi kwa Ramadhan Kibuta aliyeisawazishia Toto bao hilo katika dakika ya 72 baada ya mabeki wa Simba kushindwa kuokoa mpira uliokuwa ukizagaa golini kwao.
Matokeo hayo yanazidi kuiweka Simba katika nafasi finyu ya kucheza michuano ya Afrika mwakani kama watashindwa kumaliza msimu katika nafasi mbili za juu.
Morogoro; Baada ya mchezo kumalizika kwa suluhu kwenye Uwanja wa Jamhuri, kocha wa Yanga aligoma kuzungumza na wanahabari kwani alipanda gari lake na kuondoka uwanjani hapo ilhali Kocha wa Polisi, Adolf Richard aliwasifu wachezaji wake kwa kucheza vizuri na kujituma.
“Nashukuru kwa kupata pointi hii moja kwa sababu tulicheza na timu bora inayoongoza katika ligi, lakini vijana wangu walicheza vizuri na kufuata maelekezo yangu,” alisema kocha Richard.
Polisi Morogoro walianza mchezo huo kwa kasi na kufanikiwa kufika langoni kwa Yanga kupitia kwa washambuliaji wake Salum Machaku na Muzamir Yassin, lakini mashuti yao hayakulenga goli.
Yanga ilijibu mapigo dakika ya 26 na 27 kupitia kwa Nadir Haroub na Hamis Kiiza.
Kagera; Kagera waliutumia vizuri Uwanja wa Kaitaba kwa kuwachapa Mtibwa Sugar mabao 3-1, ambapo mabao yao yalifungwa na Maregesi Mwangi (2) na Temi Felix aliyefunga kwa mkwaju wa penalti huku bao la kufutia machozi la Mtibwa likifungwa na Vicent Barnabas.
Arusha; Wenyeji Oljoro walitumia vizuri uwanja wao wa Sheikh Amri Abeid baada ya kuwachapa JKT Ruvu mabao 2-0 ambayo yalifungwa na Karage Gunda katika dakika ya 5 na Swalehe Idd dakika ya 8, huku African Lyon ikipata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Coastal Union.
JULIO APIGANA
Kocha msaidizi wa Simba, Jamhuri Kihwelu alirushiana makonde na mchezaji wa Toto African, Erick Kyaruzi akimtuhumu kuchukua mpira wao baada ya mechi kumalizika. Kitendo hicho kilizusha vurugu kubwa uwanjani hapo na kusababisha polisi kuingilia kati kunusuru tukio hilo. Awali Julio alikwenda kwenye basi la Toto na kuchomoa funguo ya gari hilo kitendo kilichowaudhi wachezaji wa Toto.
Kocha msaidizi wa Simba, Jamhuri Kihwelu alirushiana makonde na mchezaji wa Toto African, Erick Kyaruzi akimtuhumu kuchukua mpira wao baada ya mechi kumalizika. Kitendo hicho kilizusha vurugu kubwa uwanjani hapo na kusababisha polisi kuingilia kati kunusuru tukio hilo. Awali Julio alikwenda kwenye basi la Toto na kuchomoa funguo ya gari hilo kitendo kilichowaudhi wachezaji wa Toto.
Imeandaliwa na Juma Mtanda (Morogoro), Vicky Kimaro (Mwanza), Msafiri Sanjito (Kibaha), Mosses Mashala (Arusha).
Mwananchi
No comments:
Post a Comment