ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, April 3, 2013

Balozi Kagasheki kuongoza mazishi ya Wakili Mawalla

Moshi. Vigogo mbalimbali wakiwamo mawaziri na wabunge wanatarajiwa kushiriki mazishi ya Wakili mashuhuri nchini, Nyaga Mawalla yatakayofanyika leo jijini Nairobi, Kenya.
Miongoni mwa vigogo hao ni Waziri wa Utalii na Maliasili, Balozi Khamis Kagasheki, Naibu wake, Lazaro Nyalandu na Mwenyekiti wa Chadema ambaye pia ni Mbunge wa Hai, Freeman Mbowe.
Taarifa ya Wakili Albert Msando ambaye ni miongoni mwa mawakili wa marehemu iliyotumwa kwa gazeti hili kutoka Nairobi, ilisema katika orodha hiyo wamo wabunge na wakuu wa kampuni mbalimbali.
Wabunge watakaohudhuria mazishi hayo ni mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nasari, Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema na Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa.
Watu wengine mashuhuri watakaohudhuria mazishi hayo ni Jaji Mark Bomani, Sir George Kahama, Balozi wa Tanzania nchini Kenya, Dk Batilda-Salha Buriani na familia ya marehemu wakiwamo wazazi.
Licha ya viongozi na watu mashuhuri kuthibitisha kuhudhuria mazishi hayo, wapo ndugu, jamaa na marafiki na waandishi wa habari watakaoondoka kwa magari maalumu ya kukodi leo alfajiri.
Wakati vigogo hao wakithibitisha kushiriki mazishi hayo, uchunguzi uliofanywa na madaktari (postmoterm) jijini Nairobi, umebainisha mwili ulikuwa na majeraha makubwa ya ndani.
Kwa mujibu wa Wakili Msando aliyepo Nairobi, uchunguzi huo uliofanyika Jumatatu iliyopita na kubaini Wakili Nyaga alipasuka ini na mapafu na kuvunjika mbavu kutokana na kuanguka.
Marehemu anayetajwa kuwa na utajiri wa kutisha hadi kuitwa ‘Bilionea Kijana’, alifariki dunia Ijumaa Februari 22, mwaka huu hospitali alikolazwa jijini Nairobi kwa kile kinachodaiwa kujirusha kutoka ghorofani.
Hata hivyo taarifa nyingine zinadai huenda aliuawa kwa kusukumwa kutoka ghorofa ya kwanza, ambako wodi yake ilikuwapo na kutokana na utata huo, polisi nchini Kenya wameanzisha uchunguzi.
Kuhusu ratiba ya mazishi, Wakili Msando alisema mazishi yake yatafanyika leo saa 8:00 mchana katika makaburi ya Lang’ata, Nairobi Kenya. Mawalla aliacha wosia ambao umefuatwa na familia.
Mwananchi

No comments: