ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, April 13, 2013

Bandari ya Forodha Mchanga kuhamishwa

ZANZIBAR: Serikali inakusudia kuihamisha bandari ya Forodha Mchanga iliyopo Forodhani mjini Unguja.

Naibu Waziri wa Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano, Issa Ussi Haji Gavu, aliliambia baraza la wawakilishi jana wakati akijibu swali lililoulizwa na Jaku Hashim Ayoub (Muyuni) aliyetaka kujua iwapo hakutokuwa na athari kama bandari hiyo itaondoshwa katika eneo hilo na kupelekwa mahala pengine.

Naibu Waziri huyo, alisema serikali imelizingatia suala hilo na kuona kuwa hakutokuwa na athari za kiuchumi zitakazotokana na kuhamishwa vyombo hivyo kutoka Forodha Mchanga kwani vyombo hivyo vitahudumiwa katika bandari kuu ya Malindi ambayo kuna usalama zaidi sambamba na udhibiti mkubwa wa mapato.

Alisema eneo linalotegemewa kutoa huduma hiyo ni kwenye rampu mpya ambayo ni kubwa na itakidhi mahitaji hayo.

“Hakuna hasara yoyote itakayotokana na kuhamishwa vyombo hivyo kutoka Forodha Mchanga isipokuwa faida zake ni nyingi ikiwemo usalama wa nchi na udhibiti wa mapato ya Serikali, kuondoa msongamano wa magari katika barabara za Mjimkongwe, uhifadhi wa Mjimkongwe kutokana na uzito wa magari yanayosafirishwa kupitia eneo hilo na kuepuka uchafuzi wa mazingira ya eneo hilo,” alisema.

Hata hivyo, Naibu Waziri huyo alisema kuwa Forodha mchanga sio bandari rasmi kwa mujibu wa sheria ya kuanzishwa shirika la bandari na hivyo ufukwe hutumika kwa dharura kushusha na kupakia mizigo pamoja na magari na ufinyu wa nafasi za kufunga gati meli hizo katika bandari ya Malindi.

No comments: