Na Moshi Lusonzo
Kashfa imeibuka katika hospitali moja jijini Dar es Salaam ambapo daktari wa wanawake anadaiwa kuwalazimisha wajawazito kutoa mimba ili kujipatia fedha.
Daktari huyo (jina linahifadhiwa), anayefanya kazi katika Hospitali ya Vijibweni, Manispaa ya Temeke, anadaiwa kufanya kazi hiyo kwa muda mrefu sasa bila kujulikana.
Siri hiyo iliibuliwa na Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Wilaya ya Temeke, Yahaya Sikunjema, wakati wa mkutano wa CCM, alipoomba serikali kumuondoa haraka daktari huyo ili kunusuru maisha ya watoto wachanga na mama zao.
Kwenye mkutano huo uliohudhuriwa na Mbunge wa Kigamboni, Dk. Faustine Ndugulile, Mwenyekiti huyo alisema daktari huyo amekuwa kero kubwa baada ya wanawake wengi wajawazito kushawishiwa kufanya hivyo na baadhi yao kukataa.
Alidai kuwa daktari huyo huwaambia kinamama hao kwamba ujauzito wao una matatizo na inahitaji kutolewa ili kuokoa maisha yao, wanaokubali kisha wanatoa kiasi kikubwa cha fedha kwa ajili ya kazi hiyo.
Sikunjema, alisema wanawake wengi wanaikimbia hospitali hiyo baada ya daktari huyo kulazimisha kutoa mimba hata kama mama mjamzito hana matatizo.
Alisema tatizo hilo limedumu kwa muda mrefu na amekuwa akifanya kazi ya utoaji mimba kwa wanafunzi wa shule za msingi, sekondari na vyuo mbalimbali na kujipatia fedha nyingi.
Mara kadhaa amekuwa akiwashawishi baadhi ya wanawake wajawazito wanaofika hapo kwa kuwalazimisha kutolewa mimba kwa kudai zina matatizo.
"Sijui tunakwenda wapi ikiwa daktari tunayemuamini kwa kutibu watu, leo ameigeuza hospitali kama kiwanda cha utoaji mimba, tunaiomba serikali kumuondoa haraka kwani tumemchoka," alisema Sikunjema kwenye kikao hicho.
MKE WA KIGOGO ANUSURIKA
Hata hivyo, habari zilizopatikana na kuifikia NIPASHE zinasema chanzo cha siri hiyo kubainika ni baada ya mke mmoja wa kiongozi wa Serikali (Jina linahifadhiwa) kunusurika kuingia kwenye mtego wa daktari huyo.
Habari zinasema, mke wa kiongozi huyo alipokwenda hospitalini hapo katika tarehe zake za upimaji wa afya, alikutana na daktari huyo na baada ya kumfanyia vipimo alimwambia ujauzito wake una matatizo.
Inadaiwa siku hiyo mwanamke huyo alikwenda hospitalini hapo kwa ajili ya kupima afya yake, ndipo alipokutana na daktari huyo.
Baada ya kumpatia vipimo, daktari alijifanya kuwa na huzuni sana, kisha alimwambia kwenye vipimo inaonyesha ujauzito wake una matatizo na anaweza kuhatarisha maisha yake.
"Alimshawishi kumpatia pesa ili afanye kazi ya kutoa mimba, kitu ambacho mama yule hakukubali hadi akamshauri mume wake," kilisema chanzo hicho.
Hata hivyo, aliporudi nyumbani mumewe hakukubaliana na jambo hilo na waliamua kwenda Hospitali nyingine kwa ajili ya kufanya vipimo. Huko baada ya kufanyiwa vipimo upya, majibu yalionyesha mwanamke huyo hakuwa na matatizo yanayoweza kuhatarisha mtoto aliyekuwa tumboni.
Kutokana na utata huo, mwanaume alikwenda kuwaeleza wananchi wenzake, hapo ndipo wananchi hao walipoandamana hadi nyumbani kwa mwenyekiti huyo kushinikiza daktari huyo aondolewe.
MBUNGE ASIKITIKA
Kwa upande wa Mbunge, Dk. Ndugulile alisema jambo hilo limemsikitisha na atafanya juhudi kwenda Halmashauri ya Temeke kwa ajili ya kuliangalia kwa makini.
Alisema katika kipindi chake cha ubunge amefanya kazi ngumu ya kuboresha Hospitali hiyo pamoja na ile ya Zahkhem ili wananchi wapatiwe huduma bora na sio kunyanyaswa.
"Tatizo hili siwezi kulitolea maamuzi, wenyewe Halmashauri wapo na nitakwenda kuwaambia ili walipatie ufumbuzi," alisema Dk. Ndugulile
Hata hivyo. alisema dhamira yake ya kuona jimbo hilo linakuwa na zahanati na vituo vya afya vingi inabaki palepale, ambapo anaamini atakapomaliza kipindi chake eneo hilo litakuwa na huduma nzuri ya afya.
MGANGA MKUU ASEMA
Akizungumzia suala hilo, Mganga Mkuu wa Manispaa ya Temeke, Dk. Sylvia Mamkwe, alisema Manispaa yake imeanza kumchunguza daktari huyo ili kuthibitisha jambo hilo.
Dk. Mamkwe, alisema kiutaratibu jambo hilo ni gumu kupata uthibitisho kutokana na kufanywa kwa siri, lakini watajitahidi kulifuatilia ili haki itendeke kwa kila upande.
"Nimepata taarifa hizo, nazifanyia kazi ipasavyo, kitu cha msingi jambo hili ni kama mtu anayechukua rushwa, mtu hafanyi kwa uwazi kwa kuhofia kukamatwa," alisema Dk. Mamkwe.
Dar es salaam yetu
No comments:
Post a Comment