ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, April 2, 2013

Familia ya Nyaga yakubali yaishe

Dar es Salaam. Familia ya Wakili Nyaga Mawalla imeridhia ndugu yao azikwe jijini Nairobi, Kenya na kumaliza mvutano wa suala la mazishi ya wakili huyo.Mawalla alifariki dunia jijini Nairobi baada ya kuanguka kutoka kwenye ghorofa katika hospitali alikokuwa akitibiwa Machi 23, mwaka huu.

Hata hivyo, kulizuka mvutano wa mazishi yake baada ya Wakili Fatuma Karume kupeleka wasia wa marehamu uliokuwa umeelekeza kuwa ikitokea amefia nje ya nchi azikwe huko au akifia ndani ya nchini basi azikwe kwenye shamba la Momella, Arusha wakati wazazi wake walitaka azikwe kwao Marangu mkoani Kilimanjaro.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi Dar es Salaam jana msemaji wa familia hiyo, Joseph Nuwamanya alisema wameamua kuheshimu wasia wa marehemu.

“Familia na ndugu wote wa mpendwa wetu Mawalla wameamua marehemu azikwe Jumatano jijini Nairobi kwani kabla ya kifo chake yeye mwenyewe alitaka azikwe sehemu atakayofia ikitokea amefia nje ya nchi,”alisema Nuwamanya. Alisema licha ya ndugu yao kuzikwa huko taarifa zaidi kuhusiana na sehemu, muda wa mazishi zitatolewa pindi utaratibu utakapokamilika.

Akizungumzia sababu za kifo chake alisema taarifa rasmi ya sababu za kifo chake bado hazijatolewa na uongozi wa Hospitali ya Nairobi kutokana na kutokamilika kwa uchunguzi unaoendelea.
“Kumekuwa na taarifa zinazopotosha kuhusiana na kifo chake lakini nataka niseme kwamba taarifa rasmi bado haijatolewa kwani uchunguzi unaendelea na zitakapokuwa tayari kila kitu kitaelezwa,”alisema.

Nuwamanya aliwashukuru watu wote walioshirikiana nao katika kipindi chote cha msiba na kwamba alivitaka vyombo vya habari kushirikiana na familia pamoja na ndugu katika kipindi hiki kigumu.Alisema baada ya mazishi, Alhamisi itafanyika misa ya shukrani sehemu ambayo itatangazwa badaye.

Kifo cha Mawalla kilitikisa kutokana na ukweli kuwa wakili huyo alijitengenezea jina kubwa kutokana na shughuli zake mbalimbali.

Mawalla pia alikuwa anasimamia kampuni mbalimbali zilizokuwa zinawekeza nchini na hasa katika sekta ya upangishaji nyumba na ofisi. Wakili huyo pia alikuwa mdau katika sekta ya uwindaji, ambayo usimamizi wake mara nyingi umekuwa na utata mwingi na hasa katika ugawaji wa vitalu.

Alikuwa pia mshiriki wa sekta ya utalii na alikuwa miongoni mwa watu waliokuwa wanaunga mkono ujenzi wa Uwanja wa Mugumu huko Serengeti.
Mwananchi

2 comments:

Anonymous said...

ana uhusianao wa kindugu na ndoo mawalla kwa sababu nimesoma naye ndoo mawala jamani wadau nijulisheni, hakini binadamu hatuna kitu mungu amlaze pema peponi amin

Anonymous said...

Ni mdogo wake Ndoo Mawalla.