ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, April 2, 2013

Wanajeshi wamtisha Brandts

Dar es Salaam. Kocha wa Yanga, Ernest Brandts ameingiwa na mchecheto baada ya kutamka kuwa mechi za Yanga dhidi ya JKT Oljoro, Mgambo na JKT Ruvu hazitabiriki.
Yanga inayoongoza Ligi Kuu ikiwa na pointi 49, imesaliwa na mechi tano ikiwamo dhidi ya Simba, Coastal Union pamoja na timu za Oljoro, Mgambo na Ruvu ambazo zote zinamilikiwa na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT).
Kati ya mechi hizo inahitaji kushinda michezo mitatu mfululizo na sare moja ili kuweza kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu msimu huu.
Akizungumza na gazeti hili jijini Dar es Salaam, Brandts alisema kuwa, anafahamu ugumu wa kucheza mechi na timu za jeshi hivyo anaamini anatakiwa kukiandaa kikosi chake kikamilifu ili kupata matokeo mazuri.
“Ninazifahamu vizuri tu timu zote zinazomilikiwa na jeshi kwani nilichezanazo mzunguko wa kwanza, siyo lelemama, wanacheza kwa nguvu. Kimsingi tunahitaji kujizatiti kwelikweli ili tuweze kupata matokeo mazuri ukizingatia ligi inaenda ukingoni na kila timu haitaki kupoteza mchezo,”alisema Brandts.
Alisema kuwa amewatahadharisha wachezaji wake watunze miili yao ili kuepukana na marejuhi ambayo yanaweza kuwaathiri katika mechi zao zilizosalia.
“Ukiangalia mashabiki wetu wana matumaini makubwa kwamba ubingwa ni wao na kweli ukiangalia nafasi tulipo utaona ni kama tumemaliza kazi, lakini siyo hivyo, bado tunatakiwa kupambana hadi mwisho kwa kuwa katika soka lolote linawezekana,”alisema Brandts.
Yanga inayofukuzia taji la 24 la Ligi Kuu Tanzania Bara itashuka dimbani kesho kuvaana na JKT Oljoro katika pambano litakalopigwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Ofisa Habari wa Yanga, Baraka Kizuguto ameliambia gazeti hili kuwa wachezaji wa timu hiyo waliokuwa katika mapumziko mafupi ya Pasaka wataingia kambini kuendelea kujiandaa na mechi zao za Ligi Kuu zilizobakia.
“Lengo ni kuhakikisha makosa hayajitokezi tena katika mechi zilizobakia, sababu Azam wanakuja kwa kasi nyuma yetu hivyo hatupaswi kuzembea,” alisema Kizuguto.
Mwananchi

No comments: