ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, April 4, 2013

HATA KAMA KAKUKOSEA, KUMKARIPIA MBELE ZA WATU NI KUMDHALILISHA!-2

NAMSHUKURU Mungu kwa kunikutanisha nanyi tena kupitia ukurasa huu namba moja kwa kuandika makala nzito zinazogusa maisha yetu ya kimapenzi.
Wiki iliyopita utakumbuka nilianza kuzungumzia tabia ya baadhi ya watu kuwakaripia wapenzi wao mbele za watu bila kujua kuwa kufanya hivyo madhara yake ni makubwa sana.

Ninachokizungumzia ni wapenzi kuheshimiana na kutovunjiana heshima kwa kusemana vibaya mbele za watu.
Katika hilo naomba nisisitize kwamba, kukaripiana ovyo kunapunguza mapenzi pia kunatoa mwanya kwa vidudu watu kupenyeza maneno yatakayomkera mmoja wenu na mkajikuta kila siku ni watu wa kuwapa watu sinema ya bure.
Tunapokuwa kwenye uhusiano tunatakiwa kujenga picha nzuri kwa wanaotuzunguka. Tusiwafanye watuone sisi kama wahuni tunaopelekana kama watu waliovuta bangi.
Itakuwa si jambo jema kama mpenzi wako au mkeo kakuudhi ukaanza kumsema mbele ya mashoga zako tena wakati mwingine na matusi juu. Ukifanya hivyo kwanza utaonekana mshamba lakini pia utawafanya watu wahisi kuwa uhusiano wenu upo upo tu.
Wanaopendana kwa dhati wanachagua wapi pa kusema nini kwa mpenzi, wanajua umuhimu wa kufichiana upungufu wao. Hivi leo hii mkeo akukute upo na marafiki zako kisha aanze kukusema jinsi ambavyo jana yake hukumfurahisha faragha, inaingia akilini kweli?
Hapo mwanamke atakuwa anatatua tatizo au analiongeza? Kwa kifupi atakuwa analiongeza kwani atakuwa amezidi kumuathiri mumewe kisaikolojia.
Ndiyo maana nasema, wapenzi walio kwenye uhusiano thabiti, hawasemani ovyo. Hawa wanajua sehemu maalumu ya kuwekana sawa na hata lugha inayofaa kutumika kurekebishana kwani lengo ni kujenga na si kubomoa.
Kwa maana hiyo tujiepushe sana na tabia mbaya ya kukoromeana mbele za watu tukiamini kwamba kufanya hivyo ni kuboresha uhusiano wetu lakini pia tunajenga misingi ya kuheshimiana na kupendana kwa dhati.
Pale ambapo inatokea mmoja kamkosea mwenzake ni vyema akaomba msamaha kwa unyenyekevu na kuonyesha kujutia kosa lake kisha kuyaacha maisha yenu ya furaha na amani yaendelee kuwepo. Usione ugumu kumwambia mpenzi wako; ‘samahani mpenzi wangu….’
Ukifanya hivyo hata yeye atakapokukosea atakuomba msamaha na hiyo itawafanya mzidi kupendana na kuheshimiana. Tatizo ni kwamba kuna baadhi ya watu wanapowakosea wapenzi wao hawataki kuonekana ni wakosaji.
Ukiwa hivyo usishangae ukawa mtu wa kubalaswa na mpenzi wako kila mara na kweli anaweza kufikia hatua ta kukuvunjia heshima mbele za watu akidhani ndiyo dawa yako.
Naomba nihitimishe mada hii kwa kusema kwamba, unapoingia kwenye uhusiano jitahidi sana kutomkera mpenzi wako mara kwa mara. Ni kweli kuna wakati unaweza kufanya jambo bila kudhamiria na likamtibua lakini isiwe kila mara.
Hakikisha unakuwa mstari wa mbele katika kuliboresha penzi lenu. Kuwa mtu wa kumfanyia mpenzi wako mambo ya kumfurahisha, pale unapobaini umemkera jirudi haraka ili usiharibu hali ya hewa.

Kwa leo ni hayo tu, tuonane wiki ijayo.

Global Pulishers

No comments: