ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, April 11, 2013

Kagasheki amvaa 'waziri'


  Amtaja kuwa chanzo cha mgogoro Loliondo
Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki.
Joto la mgogoro wa ardhi eneo la Loliondo limeongezeka na sasa Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki, amemshushia tuhuma nzito mmoja wa mawaziri waliomtangulia katika wizara hiyo kuwa chanzo cha mzozo unaofukuta sasa wilayani Ngorongoro ambako wakazi wake wameapa kukiadhibu Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kuituhumu serikali kuwa inawapora ardhi yao.

Bila kumtaja jina moja kwa moja ila tu kusema “kuna waziri huko nyuma” ndiye chanzo cha kuwapo mgogoro wa ardhi eneo la Loliondo kati ya mwekezaji wa Otterlo Bussness Corporation (OBC) na wakazi wa eneo, Balozi Kagasheki anaelekeza lawama ya yanayotokea kwa ama Ezekiel Maige, Shamsa Mwangunga, Anthony Diallo, Profesa Jumanne Maghembe ama Zakia Meghji, ambao walikuwa mawaziri wa wizara hiyo kabla yake.

Balozi Kagasheki aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam alipozungumza na waandishi wa habari na kusisitiza kwamba serikali itatoa kilomita za mraba 2,500 kati ya 4,000 zinazomilikiwa na mwekezaji na kuwapatia wanavijiji wa Loliondo kwa matumizi yao mbalimbali.

Alisema waziri huyo alitoa vibali 'feki' vya umiliki wa ardhi kwa wanajiji kinyume cha sheria.

Hata hivyo, Balozi Kagasheki alipotakiwa na waandishi wa habari kumtaja waziri huyo ili Watanzania wamfahamu, aligoma ingawa alisisitiza kwamba kitendo alichokifanya kiongozi huyo ni kibaya na kinyume cha sheria kwa kuwa mwenye mamlaka ya kutoa kibali cha kutwaa ardhi ni Rais wa nchi.

"Waziri aliyepita alitoa kibali juu ya kibali huku akijua hastahili kufanya hivyo na jambo hili ni baya kwa kuwa mwenye uwezo huo ni Rais wa nchi na siyo mtu mwingine," alisema.

Alipoulizwa kama serikali ina mpango wowote wa kumchukulia hatua za kisheria Waziri huyo, Balozi Kagasheki hakutoa majibu ya moja kwa moja badala yake naye alijibu kwa kuuliza swali badala ya kutoa jibu. “Ukiuziwa kiwanja chenye hati halafu mwenye hati halali akaja, anayetambuliwa ni nani?” Balozi Kagasheki alimhoji mwandishi aliyemuuliza swali.

Hata hivyo, Maige ambaye pia ni Mbunge wa Msalala, alipoulizwa kuhusiana na tuhuma hizo, hakukanusha wala kuthibitisha na badala yake alisema hawezi kuzungumza chochote kwa kuwa yupo nje ya serikali.

Maige ni miongoni mwa mawaziri wanane waliotemwa na Rais Jakaya Kikwete mwaka jana baada ya wabunge kuwasha moto mkali bungeni wakiwatuhumu kwa madudu mbalimbali ya kushindwa kuwajibika na kuisaidia serikali kiasi cha kuiacha ikilaumiwa na wananchi kwa sababu wa ubinafsi wa baadhi ya viongozi wake.

Diallo alipoulizwa na Nipashe alisema yeye hausiki na maamuzi hayo, na kutaka Waziri Kagasheki amtaje mhusika.

Mwangunga, Profesa Maghembe na Meghji hawakupatikana jana kwa njia ya simu kuzungumzia tuhuma hizo.

Aidha, Balozi Kagasheki alisema serikali kwa kusikiliza kilio cha wanavijiji hao imekubali kumega eneo la ukubwa wa kilomita za mraba 2,500 sawa na asilimia 62.7 ya eneo zima ya Pori Tengefu kati ya kilomita za mraba 4,000 na kuwapa wanavijijiji.

Mbali na kumtuhumu mtangulizi wake, Balozi Kagasheki pia alisema suala la Loliondo linakuzwa na asasi zisizokuwa za serikali (NGO) na kwamba muda wowote Rais akiridhia wananchi hao watapewa eneo la kufanyia shughuli zao na kukanusha kwamba serikali inawanyang'anya.

Waziri huyo alizishambulia NGO 37 ziliyopo eneo la Loliondo kwa madai kwamba zinachangia kuchochea mgogoro huo kwa maslahi yao binafsi ya kiuchumi na kibiashara. Balozi Kagasheki aliweka bayana kwamba kuna baadhi ya Wamasai waliojazana Loliondo ambao wanatoka nchi jirani ya Kenya na kuingia huko kwa ajili shughuli za kufuga na kwamba NGOs zinawajumlisha wote na kuwaita Watanzania.

Waziri huyo alisema mwenye mamlaka ya kumaliza mgogoro wa Loliondo ni Rais Jakaya Kikwete kwa kuwa ndiye ana uwezo wa kugawa eneo lolote la nchi kwa mujibu wa sheria za nchi.

NCHEMBA NA WENZAKE
Kuhusu viongozi wa juu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), akiwamo Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho Bara, Mwigulu Nchemba, kwenda Loliondo kuchunguza mgogoro huo, Balozi Kagasheki alisema hawakwenda kuutatua na kwamba Rais ndiye msimamizi wa ardhi yote ya nchi na ndiye ana uwezo wa kuigawa kwa matumizi yoyote.

Alisema Nchemba alikwenda Loliondo kukutana na viongozi wa CCM kwa ajili ya kupata taarifa sahihi juu ya mgogoro huo na kwamba awamu ya pili atakwenda serikalini kwa kazi hiyo kabla ya kukamilisha taarifa kamili.

Aliongeza kuwa baada ya Nchemba kukamilisha taarifa kamili kuhusu mgogoro wa Loliondo, CCM itatoa tamko rasmi la chama kuhusiana na mgogoro huo.

Wakati Balozi Kagasheki akisema hayo jana, wiki iliyopita Kamati ya CCM, inayoongozwa na Nchemba, ilisema itapeleka mgogoro huo kwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, baada ya kujiridhisha kuwa uamuzi wa serikali wa kutwaa ardhi yenye ukubwa wa kilometa za mraba 2,500 unakiuka sheria.

Wajumbe wa tume hiyo, iliyoundwa na Katibu Mkuu wa CCM, Abdurahman Kinana pia yumo Chiristopha Ole Sendeka (Mbunge-Simanjiro), Lekule Laizer (Longido) na Mary Chatanda ambaye ni Katibu wa CCM Mkoa wa Arusha.

Akizungumza na wananchi wa Loliondo katika Kijiji cha Olorien Magaiduru, Nchemba alisema baada ya kupokea maelezo kutoka kwa wajumbe wa Kamati ya Siasa ya Wilaya hiyo, viongozi wa mila na serikali wa ngazi mbalimbali wamejiridhisha kuwa hoja za wananchi kupinga uamuzi wa serikali zina nguvu.

Katika mkutano huo, Umoja wa Wanawake wa Ngorongoro, ulimkabidhi Nchemba mfuko wa kadi za wanachama wa CCM zaidi ya 2,000 ambazo waliamua kuzirejesha kutokana na kupinga uamuzi wa serikali kutwaa ardhi yao.

Kwa mujibu wa madiwani katika eneo la Loliondo, wanavijiji wapatao 64,000 wapo hatarini kugeuka wakimbizi kwa kuwa serikali inakusudia kuchukua ardhi yao.

Diwani wa Kata ya Ololosokwan, Yannick Ndoinyo, kwa niaba ya viongozi wenzake na wakazi wa Ngorongoro, aliyasema hayo juzi alipozungumza na waandishi wa habari kuhusu mgogoro wa wananchi Loliondo.

Ndoinyo alisema siyo kweli serikali inawaachia ardhi hiyo bali inakusudia kuwapokonya ardhi yenye ukubwa wa kilomita 1,500 za mraba na kumpatia mwekezaji.

Taarifa zinaonyesha mwaka 1974 Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii, na kupitia Tangazo la Serikali No 269, na kwa kuzingatia Sera ya uhifadhi ilitangaza kwamba kilomita za mraba 4,000 katika eneo la Loliondo mkoani Arusha litakuwa Pori Tengefu (Game Controlled Area) hivyo kulifanya kuwa sehemu ya mtandao wa maeneo yaliyohifadhiwa nchini.

Mbali na maeneo tengefu, asilimia 25 ya eneo la nchi kavu la Tanzania limehifadhiwa, maeneo haya ni pamoja na Hifadhi za Taifa 15, Hifadhi ya Ngorongoro ambayo ni mahsusi kwa ajili ya matumizi yasiyo ya uvunaji wa rasilimali za wanyamapori, Mapori ya Akiba (Game Reserves) 28 na Mapori Tengefu (Game Controlled Areas) 44.

Mapori ya Akiba na Mapori Tengefu ni kwa ajili ya matumizi ya uvunaji wa wanyamapori, kama vile uwindaji.

Sehemu ya 17 ya Sheria ya Uhifadhi wa Wanyamapori No 5 ya mwaka 2009 inakataza shughuli za binadamu kufanyika katika maeneo hayo. Hata hivyo, kwa kuwa idadi ya watu imeongezeka, mahitaji ya ardhi nayo yaneongezeka katika miaka ya hivi karibuni.
CHANZO: NIPASHE

No comments: