Kuna njia mbalimbali za kupunguza unene, lakini wakati wa kufanya njia hizo, ni vizuri kujua aina ya vyakula ambavyo huchangia kuongezeka kwa uzito ambavyo mtu anatakiwa kuviepuka. Itakuwa ni kupoteza muda na kujitesa iwapo utakuwa na bidii ya kupunguza uzito kwa kufanya mazoezi huku ukila vyakula vinavyochangia kuongeza uzito.
Vifuatavyo ni baadhi ya vyakula maarufu ambavyo mtu anapaswa kuviepuka kuvila kabisa kwani huongeza uzito wa mwili:
SODA
Usinywe soda ya aina yoyote ikiwemo soda zinazodaiwa kuwa hazina sukari (diet soda). Badala yake kila mara usikiapo kiu ya maji au hamu ya kunywa soda, pendelea kunywa maji safi na salama kwa afya yako. Maji husaidia kuondoa mafuta na sumu mwilini.
Usinywe pombe hata kwa kiasi kidogo iwapo upo kwenye zoezi la kupunguza uzito wa mwili. Kimsingi pombe nayo ina kiwango cha sukari ambacho huchangia ongezeko la unene wa mwili kirahisi.
‘SNACKS’
Jiepushe na ulaji wa vitafunwa ‘snacks’ vilivyotengenezwa kwa kuchanganywa na mafuta, sukari au chumvi. Mfano wa vitafunwa hivyo ni pamoja na chips, popkoni zenye sukari, biskuti, keki, askrimu, chokoleti, n.k.
Kwa kawaida vitafunwa hivi huwa havishibishi bali hutia hamu ya kula, hivyo utajikuta umekula kiasi kingi cha sukari au chumvi ambacho kinaenda kuongeza uzito mwilini bila kujijua.
Vitafunwa hivi huwa na tabia moja ya kumfanya anayependa kuvila aendelee kupenda kuvila kila siku bila kukosa, hivyo kumfanya awe ‘mlevi’ (addicted) wa vyakula hivyo. Kwa staili hii ya ulaji, ukifanya mazoezi ya kupunguza uzito huku unaendelea na ulaji huu, huwezi kupungua hata kidogo, zaidi utashangaa kuona unanenepa zaidi badala ya kupungua.
VYAKULA VILIVYOKOBOLEWA
Epuke ulaji wa vyakula vilivyopikwa kutokana na unga uliokobolewa, iwe unga wa mahindi, ngano, n.k., kwani vyakula vya namna hii vilivyoondolewa virutubisho vyake muhimu huchangia kulifanya zoezi la kupunguza uzito kuwa gumu, kwa sababu navyo vinachangia unene. Lakini ukila vile ambavyo havijakobolewa (whole grain), matokeo yake huwa mazuri, kwani husaidia kupunguza unene.
Listi ya vyakula unavyotakiwa kuviepuka kabisa wakati wa kufanya zoezi la kupunguza unene ni ndefu, lakini kwa ufupi ni pamoja na vyakula vyote vya kukaanga kwa mafuta, vyakula vya kwenye makopo, mkate mweupe, chips za viazi vitamu vilivyopikwa kwa mafuta na vingine vingi.
Badala yake pendelea kula matunda ya aina mbalimbali na mboga za majani kwa wingi na vyakula vya kubanika au kuoka badala kukaanga kwa mafuta na kula vyakula asilia. Suala la kunywa maji kwa wingi kila mara na kila siku linarahisisha kwa asilimia nyingi zoezi la kupunguza uzito.
Global Publishers
No comments:
Post a Comment