ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, April 30, 2013

UTAMU AU MATESO YA MAPENZI HUTOKANA NA MTINDO WAKO WA MAISHA - 4


Nilipokuwa namaliza makala haya wiki iliyopita, niliuliza: Wewe unamsoma halafu unaficha kucha, naye anakusoma lakini naye hataki ajulikane. Unadhani mafanikio gani yatapatikana? Tatizo hili ndilo ambalo husababisha watu wengi kuingia kwenye uhusiano wa kimapenzi wakiwa hawajuani, hivyo kuleta migogoro baadaye

Baada ya uhusiano kufikisha umri fulani, kila mtu humzoea mwenzake. Ile hofu ambayo ilikuwa mwanzoni huondoka, sasa zile kucha zilizofichwa, kila mmoja huanza kuzichanua. Ni hapo ndipo lawama za “siku hizi umebadilika” huibuka. Ukweli ungezingatiwa, lawama hizo zisingetokea.
Kumbe sasa, kama ni mabadiliko, basi alibadilika mwanzoni mwa uhusiano kwa sababu alificha kucha. Baadaye anapoonesha tabia zake halisi, huonekana amebadilika. Ni kazi nzito sana kudumu na uhusika wa bandia. Unaweza kuuvaa kwa kipindi kifupi lakini baadaye utakushinda. Siku zote wewe utabaki kuwa wewe.
Vilevile, lazima ukubali kufungaka na ukishakubali kuwa utamu au mateso ya mapenzi ni wewe mwenyewe, utazingatia kipengele cha wasiwasi. Hupaswi kabisa kuwa mtu wa shakashaka. Jaribu kujitengeneza kila siku iendayo kwa Mungu, kuepeka mawazo mabaya ambayo yatakufanya uwe mwenye wasiwasi.
Fikiria chanya. Mpe mwandani wako fursa ya kujiamini ili aweze kufikiria mazuri kwa ajili yako. Endapo atabaini humwamini na una wasiwasi juu yake, utamsababishia awe na hali hiyohiyo kwako. Mambo hayo huchanua kwa kasi ya moto wa kifuu kikavu na kusababisha kupotea kwa uaminifu.
Wasiwasi wako huzaa wasiwasi wake. Matokeo ya jumla kila mmoja kutomwamini mwenzake. Hayawezi kuwa mapenzi matamu kama hamuaminiani. Maisha ya uaminifu huanza na wewe mwenyewe. Shakashaka zisizo na maana unatakiwa uziweke mbali nawe. Ishi kwa uhuru, epuka wasiwasi.
Mwingine anaweza kukaa peke yake na kuanza kufikiria kwamba mwenzi wake anataka kumfanyia kitu kibaya. Wasiwasi huo hukua taratibu mpaka kutawala kichwa. Kwa maana hata kipindi unazungumza naye, anaweza kutamka mambo chanya, wewe ukayapokea hasi kwa sababu ya imani iliyopo ndani yako.
Wakati mwingine marafiki ndiyo chanzo cha wasiwasi ulionao. Zingatia kwamba mtu anayekupenda, hawezi kukufanya uwe na wasiwasi. Sasa hebu mtazame kwa jicho la angalizo huyo anayekuja kukwambia maneno ambayo yanakufanya uwe na wasiwasi dhidi ya mwenzi wako.
Zingatia; Usikae na maumivu moyoni kwa tabia yako ya kujifanya malaika wakati kuna mengi yanakutatiza. Penda kuufungua moyo kwa maana kufanya hivyo kutakuweka huru. Kufichaficha vitu na kuvitunza moyoni, athari yake huwa kubwa kuliko maelezo. Ni suala la umakini katika mapenzi.

LINAPOTOKEA TATIZO, JITAZAME WEWE KWANZA
Unapojisikia huna furaha, mara nyingi inakuwa rahisi kuwaza kuna tatizo kwenye uhusiano wako. Utamlaumu mwenzako kuwa yeye ni sababu ya wewe kutokuwa na furaha. Bahati mwbaya zaidi ni kwamba unaweza kudhani kuwa suluhisho lipo ndani yake.
Hilo ni kosa kubwa. Kwanza, unapowaza kuwa mwenzi wako ndiye suluhisho, unamfanya ajione ana mamlaka makubwa sana juu yako. Pili, hutapata ufumbuzi wa majanga yanayokusibu kwa sababu unakuwa hujapata mzizi wa tatizo. Penda kuusaka mzizi wa tatizo!

Itaendelea wiki ijayo.

Global Publishers

No comments: