Kwa maana rahisi ni kwamba mishahara wanayolipwa wafanyakazi nchini haiwezi kumudu gharama za maisha kwa mwezi, hivyo wengi wanaishi katika maisha ya dhiki na kubahatisha.
Kibaya zaidi, tatizo hili la nyongeza ya mshahara kutoendana na hali halisi ya maisha linaathiri zaidi wafanyakazi wa ngazi ya chini ambao ndio wengi hivyo kuwapotezea ari ya kufanya kazi kwa bidii kwa manufaa ya nchi yetu.
Hivyo basi, wakati tunajiandaa kusherehekea Siku ya Wanyakazi Duniani kesho, ni vyema mgeni rasmi wa maadhimisho hayo nchini ambaye ni Rais Jakaya Kikwete ajibu kero mbalimbali zinazowakumba watumishi hawa ambao waliitikia wito wa kuitumikia nchi kwa uaminifu.
Tunatambua kwamba Serikali haiwezi kuwa na uwezo mkubwa wa kumaliza tatizo la viwango vidogo vya mshahara kwa mara moja, lakini tuna imani kwamba kwa kiasi fulani inao uwezo wa kupunguza tatizo hili kwa zaidi ya nusu hivyo kutoa matumaini mapya kwa wananchi.
Sote tunambua kwamba katika miaka ya hivi karibuni mfumuko wa bei umepanda kwa kasi ya ajabu hivyo kufanya bidhaa kuuzwa kwa bei ghali. Kupanda huku kwa mfumuko wa bei, kumefanya watu wengi wakiwamo wafanyakazi kushindwa kununua baadhi ya bidhaa ambazo hapo awali walikuwa wakizinunua kwa mahitaji yao ya kila siku.
Ndiyo maana tunasema kwamba kima cha chini cha mshahara ambacho ni Sh180,000 hakilengi kumsaidia mfanyakazi kuishi maisha ya kawaida ya binadamu bali kinamfanya aendelee kudhalilika kwa dhiki isiyo na kifani.
Lakini pia wakati tukiiasa Serikali kupandisha kima cha chini cha mshahara, upande wa sekta binafsi nako hali ni mbaya sana, kwani mishahara ni midogo na tunaambiwa kwamba kuna waajiri wengine hasa wa sekta ya ulinzi wanawalipa watumishi wao kiasi cha Sh40,000 hadi Tsh 60,000 kwa mwezi.
Kweli hii si haki, hivyo hatua kali lazima zichukuliwe dhidi ya unyama wa aina hii. Sote tunajua kwamba Serikali imeweka viwango vya mshahara katika sekta binafsi hivyo ni kosa kwa waajiri hawa kutofuata miongozo halali.
Mbali na mishahara, madai mengine ambayo wafanyakazi nchini wamekuwa wakilalamika kila mwaka ni kodi kubwa inayotozwa kwenye mishahara. Hivyo basi tunaona ni wakati mwafaka kwa tatizo hili kufanyiwa kazi, ikiwa ni pamoja na Serikali kutafuta maeneo mengine ya kukusanya kodi badala ya kutegemea kwenye mishahara midogo ya watu wa chini.
Ndiyo maana kama taifa ni lazima sasa tukae chini na kumaliza tatizo la mishahara nchini.
Kwa bahati nzuri, katika hotuba yake kwenye kilele cha sherehe hizo zilizofanyika kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga, Rais Kikwete alisema Serikali inatambua mazingira magumu ya kazi waliyonayo wafanyakazi na kwamba Serikali ipo tayari kuyaboresha.
Kutokana na kauli hiyo ya Rais Kikwete, bado tunaamini kwamba Serikali yake ina dhamira ya dhati ya kusaidia wafanyakazi nchini nao waishi kama wengine wanaofaidi rasilimali za nchi yetu.
Tunaamini kwamba kilio cha wafanyakazi kikisikilizwa na migongano ya hapa na pale na Serikali itakuwa historia kwa lengo la kusukuma mbele maendeleo yetu.
Vilevile, tunatambua juhudi mbalimbali za Serikali za kukabiliana na tatizo la mfumuko wa bei na kwamba ziendelee kwani zitasaidia wafanyakazi waishi katika mazingira bora ya kuwafanya wajitume ipasavyo.
Mwananchi
No comments:
Post a Comment