ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, April 2, 2013

Kikwete: Misikiti mitatu imenisomea itikafu nife

  Asema wadai anawapendelea Wakristu
  Atahadharisha nchi sasa yaelekea kubaya
  Ashauri Watanzania waishi bila kubaguana

Rais Jakaya Kikwete, amesema kuna misikiti mitatu ya jijini Dar es Salaam imemsomea itikafu ili afe, ikimshutumu kwamba anawapendelea Wakristu.

Amesema katika itikafu hiyo wamewajumuisha Inspekta Jenerali wa Polisi, Said Mwema na Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Kamishna Msaidizi Mwandamizi  Suleiman Kova.


Rais Kikwete aliyasema hayo juzi usiku kwenye hotuba yake ya mwisho wa mwezi wakati akizungumzia uhusiano wa Wakristu na Waislamu nchini ambao alisema umeanza kulegalega.

“Wanasema nchi inaendeshwa kwa mfumo wa Kikristo. Mimi binafsi wananishutumu kuwa napendelea kushiriki zaidi kwenye shughuli za Wakristo kuliko za Waislamu kama vile harambee za kujenga makanisa na shule za makanisa,” alisema.

Alisema waliomsomea itikafu wanamshutumu kuwa mwepesi kushiriki maziko ya maaskofu kuliko masheikh wanapofariki.

SERIKALI HAIPENDELEI
Rais Kikwete aliwahakikishia Watanzania kuwa serikali haipendelei upande wowote na haifurahishwi na kitendo cha mtu kudhalilisha dini ya mwenzake ndiyo maana wapo wahadhiri wa dini ya Kiislamu na wahubiri wa dini ya Kikristo wamekamatwa na kufunguliwa mashtaka kwa nyakati mbalimbali. 

Alisema yeye habagui, hushiriki shughuli za Waislamu na Wakristo kila anapoalikwa labda akose nafasi kwa sababu nyinginezo.

“Nimeshafanya shughuli nyingi za Waislamu kama vile Maulid ya Mtume Muhamad (S.A.W), safari za Hijja, ujenzi wa misikiti na madrasa na mengineyo mengi.  Nimeshashiriki mazishi ya Masheikh kama nifanyavyo kwa Maaskofu na watu mbalimbali Waislamu na Wakristo,” alisema. 

Alisema pale ambapo hakushiriki mazishi ya Sheikh au Askofu itakuwa ni kwa sababu ya kubanwa na shughuli nyingine ambazo lazima zifanywe na yeye, au taarifa ilikuwa ya muda mfupi. 

“Kwa upande wa Waislamu desturi yetu ya kuzika mara mtu anapofariki mara nyingine huwa kikwazo kwangu kushiriki baadhi ya shughuli hasa ikiwa ni nje ya Dar es Salaam kwa sababu ya taratibu za kumsafirisha Rais kutoka mahali pamoja kwenda pengine siyo nyepesi.   Wakristo hawana utaratibu huo, huwa wanaweza kusubiri hivyo huniwia rahisi kushiriki,” alisema.

Alisema kama waumini wa Kiislamu na Wakristu hawatakubali kubadili mwelekeo wa sasa taifa linaelekea kubaya.

Alisema sifa ya miaka mingi ya Waislamu na Wakristo kuishi pamoja kidugu, kwa upendo, ushirikiano na kuvumiliana itatoweka.

“Nchi yetu nzuri tutaivuruga na sifa yake ya miaka mingi. Tanzania itaacha kuwa kisiwa cha amani na kuingia katika orodha ya nchi zenye migogoro na hata vita vya wenyewe kwa wenyewe, nyaraka na kauli kali kali zinazotolewa na viongozi wa dini za Kikristo na Kiislamu zinanishawishi kuamini haya niyasemayo,” alisema.

Aidha, alisema nyaraka na kauli hizo zina mambo mawili makuu ambapo kila upande unatuhumu, kushutumu na kulaumu upande mwingine kwa kufanya vitendo viovu dhidi ya dini nyingine.

Alisema kauli na mihadhara ya kudhalilisha dini za wengine, kunajisi vitabu vitakatifu, kuchoma moto nyumba za ibada, mzozo kuhusu nani achinje na kuuawa kwa viongozi wa dini ni baadhi ya mambo yanayotolewa mifano wa hali ya mahusiani ya kidini kuporomoka.

Alisema kila upande unailaumu serikali kwa kupendelea upande mwingine,  Wakristo wanalaumu kwamba mihadhara ya kudhalilisha Ukristo inaendeshwa na serikali haichukui hatua.

Alisema Wakristo wanalalamika kwamba wanateswa na viongozi wao kuuawa na Waislamu, lakini serikali haichukui hatua.

“Kwa ajili hiyo wanadai kuwa Serikali imeshindwa kulinda uhai wa raia wake.  Wanasema pia kwamba Serikali inapendelea upande wa Waislamu lakini Waislamu nao wanadai kuwa kitabu chao kitakatifu, yaani Quran Tukufu kinadhalilishwa kwa kuchanwa, kuchomwa moto na kukojolewa na Wakristo na serikali haichukui hatua yoyote ya maana,” alisema.

Rais Kikwete alisema  Waislamu wanalalamika kwamba wananyanyaswa katika nchi yao, wanakamatwa ovyo, hawapewi fursa sawa na kwamba serikali inawapendelea Wakristo.

“Nawasihi sana ndugu zangu Wakristo na Waislamu kuwa tusiyachakulie matukio ya kuuawa kwa Mchungaji Mathayo Kachila kule Buseresere, Geita, na Padri Evaristus Mushi kule Zanzibar au kumwagiwa tindikali Sheikh Fadhili Soroga, Naibu Mufti wa Zanzibar, kupigwa risasi Padri Ambrose Mkenda na kuchomwa moto kwa makanisa Zanzibar na Mbagala, Dar es Salaam kuwa ni kielelezo na ushahidi wa serikali kushindwa kutimiza wajibu wake,” alisema.

Rais Kikwete alisema kila tukio lina mazingira yake na hakuna ushahidi wa vyombo vya serikali kuzembea wala hakuna ushahidi wa matukio hayo kuunganika.

Alisema mpaka sasa serikali haijapata ushahidi wa kuwapo kikundi cha Waislamu wanaopanga kuua viongozi wa Kikristo na kuchoma moto makanisa hapa nchini.

Alisema serikali haijapuuzia kila palipotokea matukio ya uhalifu na kwamba watu 76 wanaotuhumiwa kuharibu na kuchoma moto makanisa kule Mbagala na kufanya fujo kituo cha polisi wamekamatwa na kesi zao zinaendelea mahakamani.

SAKATA LA KUCHINJA
Aidha, Rais Kikwete alisema mzozo kuhusu kuchinja kule Geita iwe fundisho kwa watu wote na kisha kuazimia kwamba yaliyopita si ndwele, tugange yajayo.

Alisema lazima Watanzania wafikiri maisha yatakuwaje kwenye shughuli za kijamii kama vile sherehe, harusi, ngoma na misiba iwapo wataanza kuwa na chakula tofauti kwa Waislamu na Wakristo.

“Fikiria itakuwaje kwenye hospitali, shule na  vyuo pawe na majiko mawili au labda hata mabwalo mawili ya chakula kwa Waislamu na Wakristo. Jeshini nako kuwe na majiko na mabwalo ya Waislamu na Wakristo. 

Hali iwe hivyo hivyo kwenye migahawa na maeneo mengine yenye huduma ya chakula,” alisema.
“Ndugu zangu, tunataka kuipeleka wapi nchi yetu? Tunataka kujenga nchi ya namna gani? Mimi naamini tukifanya hivyo huo utakuwa ndiyo mwanzo wa kubaguana kwa kila kitu na kila jambo na kuligawa taifa kwa namna ambayo hatutakuwa wamoja tena.

Huko tunakoelekea siko, ni kubaya. Tubadilike, na wakati ni huu. Viongozi wa dini waongoze njia wawaepushe waumini wao na taifa letu na janga hili,” alisema.

 Alisema kuna haja kwa  viongozi wa dini hizo mbili kubwa kukutana na kuizungumzia hali hiyo na kuipatia ufumbuzi kwani wao ndio wenye  majawabu ya matatizo hayo.

KUPOROMOKA GHOROFA DAR

Katika hotuba yake hiyo, Rais Kikwete pamoja na mambo mengine, pia alizungumzia ajali ya jengo la ghorofa 16 jijini Dar es Salaam na kusema imemuhuzunisha sana lakini ameridhishwa na juhudi kubwa za uokoaji zilizokuwa zinafanywa na wanajeshi wakishirikiana na taasisi, mashirika binafsi na wananchi.

“Napenda kutumia nafasi hii kutoa shukrani maalum kwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Saidi Meck Sadick kwa uongozi wake madhubuti.  Pia nampongeza Mkuu wa Wilaya ya Ilala,  Raymond Mushi, na Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam,  Suleiman Kova pamoja na maafisa na askari wa JWTZ, na wale wote walioshiriki na wanaoendelea kushiriki katika juhudi za uokoaji,” alisema. 

Aliwapongeza pia madaktari na wauguzi wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na hospitali nyingine kwa jitihada zao za kuokoa maisha ya waliojeruhiwa.

Rais aliwapa pole wale wote waliofiwa na wapendwa, ndugu na jamaa zao katika ajali hiyo na aliwaomba wawe na moyo wa subira huku wananchi wote wakiungana nao kuwaombea marehemu  wapate mapumziko mema peponi. 

Aidha, alisema maneno mengi yamesemwa kuhusu chanzo cha ajali hiyo lakini aliagiza vyombo na mamlaka husika wachukue hatua zipasazo kuchunguza sababu za ghorofa hilo kuanguka na watakaothibitika kusababisha maafa hayo  wachukuliwe hatua zinazostahili.
  “Wakushtakiwa mahakamani washitakiwe na wa kufutiwa leseni za kufanya shughuli za ujenzi au taaluma zao wafutiwe bila ajizi” alisema na kuongeza:

“Jambo la msingi la kusisitiza ni kuwa mamlaka zinazohusika na usimamizi wa ujenzi lazima zitimize ipasavyo wajibu wake.  Naamini kama mamlaka hizo zingetimiza ipasavyo wajibu wake ajali hii ingeepukika.”

Alisema ni matumaini yake kuwa Bodi ya Usajili wa wakandarasi na Bodi ya Usajili wa Wahandisi itakamilisha mapema uchunguzi wake ili ukweli ujulikane. 

Alisema  Bodi ya Usajili wa Wasanifu Majengo na Wakadiriaji Majenzi na Baraza la Taifa la Ujenzi nao washirikishwe kwa ukamilifu ili ukweli upatikane na hatua stahiki zichukuliwe na pia aliomba washauri namna bora ya kukomesha ajali za aina hiyo siku za usoni.
CHANZO: NIPASHE

No comments: