ANGALIA LIVE NEWS

Friday, April 12, 2013

Kipre Tchetche alifunga mara mbili na Khamis Mcha akaongeza goli jingine moja wakati Azam FC ilipotoa kipigo cha 3-1 dhidi ya timu "nyanya" ya African Lyon kwenye Uwanja wa Azam Complex jijini Dar es Salaam jana na kupiga hatua kubwa kuifuata Yanga kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara.
 
Ushindi ulimaanisha kwamba Azam sasa imefikisha pointi 46, tatu tu nyuma ya vinara Yanga, ambayo hata hivyo ina mechi moja mkononi. Yanga itacheza mechi yake ya mkononi dhidi ya JKT Oljoro kwenye Uwanja wa Taifa kesho, mechi ambayo ilipangwa kufanyika juzi Jumatano lakini ikasogezwa mbele ili kuwezesha kurushwa moja kwa moja na kituo cha televisheni cha Supersport. 
 
Kinara wa mabao, Kipre Tchetche, raia wa Ivory Coast, alifunga magoli yake ya jana katika dakika ya 28 na 61 na kumfanya kufikisha jumla ya mabao 14 katika mbio za kuwania tuzo ya kiatu cha dhahabu, akifuatiwa na Didier Kavumbagu wa Yanga mwenye magoli 9. 
 
Goli pekee la Lyon lilifungwa na Adam Kingwande katika dakika ya 36.
 
Kipigo hicho kilizidi kuisukuma Lyon kwenye "kaburi" la kushuka daraja ikiwa na pointi 19, sawa na timu inayoshika mkia ya Polisi Morogoro huku zikiwa zimesalia mechi tatu ligi kumalizika.
 
Huku safari ya kuelekea ubingwa ikiwa imebaki kuwa mbio za farasi wa wawili, Azam itakuwa na mtihani mgumu zaidi Jumapili wakati itakapowakabili mabingwa Simba, ambao wana hasira za kuachwa mbali mno katika mbio za kutetea taji lao wakiwa na pointi 34, ambazo ni pointi 15 nyuma ya mahasimu wao wa jadi Yanga.
 
Vikosi katika mechi ya jana vilikuwa; Azam: Aishi Manula, Himid Mao, Wazir Salum, Luckson Kakolaki, Joackins Atudo, Jabir Azizi, Kipre Tchetche, Abubakar Salum, Abdi Kassim/Seif Abdallah, Ibrahim Mwaipopo/Humphrey Mieno na Khamisi Mcha/Brian Umony.
 
African Lyon: Noel Lucas, Ibrahim Isaac, Sunday Bakari, Yussuf Mlipili, Obinna Salamusasa, Juma Seif/Hamadi Manzi, Jackob Massawe, Mohamed Samatta, Adam Kingwande, Freddy Lewis/Alphonce Lucas na Ndela Kashakala/Bright Ike.
CHANZO: NIPASHE

No comments: