ANGALIA LIVE NEWS

Friday, April 19, 2013

KOSA KUBWA KUMFANYA MKEO KUWA WA FAMILIA

KAMA ilivyo ada tumekutana tena, kabla ya yote napenda kumshukuru Mungu kwa kutukutanisha tena siku ya leo.
Katika maisha kuna makosa ambayo huwa tunafanya bila kujua matokea yake yanaleta migogoro katika uhusiano. Nimekuwa nikipokea malalamiko mengi kutoka kwa wanawake wanaolalamika kukosana na familia ya mumewe kuwa hawampendi kutokana na vitu anavyo fanyiwa na mumewe.

Wanaume wameingia katika matatizo ya kukimbiwa na wake zao baada ya kugombana na familia yake au mtu kukosana na familia yake kutokana na kumjali mkewe.
Baada ya wote kuwabana na maswali niligundua tatizo ni moja ambalo ndiyo chanzo cha mambo yote.
Watu wengi tumekuwa tunaanza uhusiano wetu tukiwa tunaishi kifamilia kitu kinachosababisha kuishi na wenza wetu nyumba moja na familia zetu. Hii imefanya baadhi ya mambo mengi kushea wote kama chakula na mambo mengine.
Vitu hivi huwa kero kwa mwanamke ambaye kaolewa ili aishi maisha ya kujitawala matokeo yake anakuwa yupo ndani ya utawala mwingine ambao humfanya akose amani.
Wanawake wengine hujikuta akifanya kazi zote kama msichana wa kazi na si muolewaji. Pia matatizo mengine huwa katika hali ya maisha utakayoishi na mkeo. Kuna vitu ni lazima avipate kama mkeo ambavyo vinaweza kuitengeneza chuki kati yako na familia yako.
Inawezekana wewe ndiye unategemewa na familia yako. Ombi la mkeo lazima ulifanye kwa haraka kuliko la mama yako, dada au mdogo wako. Vitu hivi hujenga chuki kuonekana kama mkeo amekutawala na wao umewadharau.
Unaweza kuona kitu kidogo lakini ni tatizo kubwa linalojenga chuki kati ya mkeo na familia yako, vilevile mkeo hawezi kukubali usaidie familia yako kwa kiasi kikubwa kama ndiyo mnayaanza maisha. Inawezekana ana haki kwa kutaka mjijenge kwanza ndipo mtoe msaada.
Siku zote unapokaa na familia yako yapo mambo hutaka kuona yanatimizwa lakini ukiyaacha na kumfanyia mkeo huwa tatizo linalojenga chuki kati ya mkeo na familia yako.


Nini kifanyike?

Siku zote kila mwanadamu anapenda uhuru hasa katika maisha ya ndoa, mwanamke anapoolewa uhitaji kufanya mambo yake kwa uhuru na kupanga mambo yake na mumewe, si mtu wa tatu ambaye huwa mama au dada ambao huwa chanzo cha matatizo kati yao na mwanamke.
Japokuwa si wote wenye tabia hizo lakini asilimia kubwa ndoa nyingi zimeingia kwenye matatizo kwa mwanamke kuolewa na kukaa katika nyumba ya familia na kugeuzwa mke wa familia kwa kufanyishwa kazi zote kama msichana wa kazi huku wifi zake wakimtazama.
Raha ya ndoa unapotaka kuoa unatakiwa ukae mbali na familia yako, kama wanakutegemea unatakiwa kuisaidia ikiwa kwao. Inawezekana kabisa mkeo ana tabia ya uchoyo ukimweleza kuhusu kuisaidia familia yako ananuna, kama mkiwa mbali ni nafasi nzuri ya kuisaidia bila kumshirikisha kwa vile haonyeshi ushirikiano katika familia yako.
Ukitaka kumnunulia chochote mkeo au mle chakula mkipendacho hakuna mtu wa kuwachunguza. Kama mngekuwa ndani ya familia msingeweza kufanya kitu kama hicho kwa vile ili kutosha familia yote lazima uwe na fedha nyingi.
Kuwa mbali na familia inajenga pia mapenzi kati ya mkeo na familia yako, kwa vile vitu vingi vinafanyika bila mtu yeyote kujua kati ya mkeo na familia yako.
Kama unataka kuichukua familia yako hata ikija unakuwa chini yenu bila kuidharau lakini utawala unabakia kwako na mkeo hata hao watakao kuja wanatakiwa kuheshimu.

Ikiwa utafanya hivyo utaondoa matatizo kati ya mke na familia. Kwa hayo machache tukutane wiki ijayo.

Global Publishers

No comments: